Mazungumzo Mafupi Kuhusu “Ufalme wa Milenia Umewadia”
Mnafikiri nini kuhusu maono ya Ufalme wa Milenia? Watu wengine wana fikira nyingi kuuhusu, na wanasema: “Ufalme wa Milenia utadumu kwa miaka elfu moja duniani, kwa hivyo ikiwa washiriki wenye umri mkubwa wa kanisa hawajaoa au kuolewa, je, ni lazima waoe au waolewe? Familia yangu haina pesa, je, ninapaswa kuanza kutafuta pesa? …” Ufalme wa Milenia ni nini? Je, mnajua? Watu hawawezi kung’amua hili na wanapitia usafishaji mkubwa. Kwa kweli, Ufalme wa Milenia bado haujawadia rasmi. Wakati wa hatua ya kuwafanya watu kuwa watimilifu, Ufalme wa Milenia bado uko katika umbo la kiinitete; wakati wa Ufalme wa Milenia uliozungumziwa na Mungu, mwanadamu atakuwa amefanywa kuwa mtimilifu. Hapo awali, ilisemwa kwamba watu watakuwa kama watakatifu na watasimama imara katika nchi ya Sinimu. Watu wanapofanywa kuwa watimilifu, wanakuwa watakatifu waliozungumziwa na Mungu, na ni hapo tu ndipo Ufalme wa Milenia utakuwa umewadia. Mungu anapowafanya watu kuwa watimilifu, Anawatakasa, na kadiri wanavyozidi kutakaswa, ndivyo wanavyozidi kufanywa kuwa watimilifu na Mungu. Wakati uchafu, uasi, upinzani, na mambo ya mwili ndani yako vinapoondolewa na kutakaswa, basi utampendeza Mungu (yaani, utakuwa mtakatifu); unapokuwa umefanywa kuwa mtimilifu na Mungu na kuwa mtakatifu, utakuwa katika Ufalme wa Milenia. Sasa ndiyo Enzi ya Ufalme. Katika Enzi ya Ufalme wa Milenia watu watategemea maneno ya Mungu ili kuishi, na mataifa yasiyohesabika yatakuja chini ya jina la Mungu, na wote watakuja kusoma maneno ya Mungu. Wakati huo, wengine watapiga simu, wengine watatuma telegramu … watatumia kila mbinu kupata maneno ya Mungu, na ninyi, pia, mtakuja chini ya maneno ya Mungu. Haya yote ndiyo yanayotokea baada ya watu kufanywa kuwa watimilifu. Katika wakati wa sasa, watu wanafanywa kuwa watimilifu, wanasafishwa, wanatiwa nuru, na wanaelekezwa kupitia maneno; hii ni Enzi ya Ufalme, ni hatua ya watu kufanywa kuwa watimilifu, na bado haina uhusiano wowote na Enzi ya Ufalme wa Milenia. Wakati wa Enzi ya Ufalme wa Milenia, watu tayari watakuwa wamefanywa kuwa watimilifu na tabia potovu ndani yao zitakuwa zimetakaswa. Wakati huo, maneno ambayo yamenenwa na Mungu yatawaelekeza watu hatua kwa hatua, na kufunua siri za kazi yote ya Mungu tangu wakati wa uumbaji hadi katika wakati wa sasa, na maneno Yake yatawaambia watu kuhusu matendo ya Mungu katika kila enzi na kila siku, jinsi Anavyowaelekeza watu kwa ndani, kazi Anayofanya katika ulimwengu wa kiroho, na yatawaambia kuhusu mienendo ya ulimwengu wa kiroho. Ni hapo tu ndipo itakuwa kweli Enzi ya Neno; sasa iko tu katika umbo la kiinitete. Ikiwa watu hawatafanywa kuwa watimilifu na kutakaswa, hawatakuwa na njia ya kuishi miaka elfu moja duniani. Mwili hauwezi kuepuka kuharibika. watu wakitakaswa kwa ndani, na kuwa huru kutokana na mambo ya Shetani na ya mwili, basi wataendelea kuwa hai duniani. Bado huwezi kung’amua mambo haya katika hatua hii, na yote ambayo mnapaswa kupitia ni kumpenda Mungu na kuwa na ushuhuda Kwake kwa kila siku mnayoishi duniani.
“Ufalme wa Milenia Umewadia” ni unabii, ni sawa na utabiri wa nabii, unabii ambamo Mungu anatabiri kile kitakachotokea katika siku zijazo. Maneno ambayo Mungu atanena katika siku zijazo na maneno Anayonena katika wakati wa sasa si sawa: Maneno ya siku zijazo yataelekeza enzi, ilhali maneno Anayonena katika wakati wa sasa yanawafanya watu kuwa watimilifu, yanawasafisha, na kuwapogoa. Enzi ya Neno katika siku zijazo ni tofauti na Enzi ya Neno katika wakati wa sasa. Katika wakati wa sasa, maneno yote yanayonenwa na Mungu—bila kujali njia Anayotumia kunena—ni ili kuwafanya watu kuwa watimilifu, kutakasa kile kilicho kichafu ndani yao, kuwafanya watakaswe, na kuwafanya wawe watu wenye haki mbele za Mungu. Maneno yanayonenwa katika wakati wa sasa, na maneno yatakayonenwa katika siku zijazo, ni mambo mawili tofauti. Maneno yanayonenwa katika Enzi ya Ufalme yanalenga kuwafanya watu waingie katika mafunzo yote, kuwaleta watu kwenye njia sahihi katika kila kitu, na kuondoa yote yenye mchanganyiko ndani yao. Hiki ndicho ambacho Mungu anafanya katika enzi hii, Akifanya iwe kwamba maneno Yake yanatumika kama msingi ndani ya kila mtu na kama maisha ya kila mtu, yakiwatia nuru na kuwaelekeza kwa ndani kila wakati, na ili kwamba watu wasipojali nia za Mungu, maneno ya Mungu yanakuwa ndani yao ili kuwakemea na kuwatia adabu. Maneno ya katika wakati wa sasa yanapaswa kuwa maisha ya mwanadamu; yanakimu moja kwa moja yote ambayo mwanadamu anahitaji, yote unayoyakosa kwa ndani yanatolewa na maneno ya Mungu, na wale wote wanaokubali maneno ya Mungu wanatiwa nuru kwa kula na kunywa maneno Yake. Maneno yatakayonenwa na Mungu katika siku zijazo yatawaelekeza watu wa ulimwengu mzima; katika wakati wa sasa, maneno haya yananenwa tu nchini China, na hayawakilishi yale yanayonenwa kwa ulimwengu mzima. Mungu atanena tu kwa ulimwengu mzima wakati Ufalme wa Milenia utakapowadia. Jueni kwamba maneno yanayonenwa na Mungu katika wakati wa sasa yote ni ili kuwafanya watu kuwa watimilifu; maneno yanayonenwa na Mungu wakati wa hatua hii yanalenga kukimu mahitaji ya watu, si ili kukuwezesha kujua siri au kuona ishara na maajabu ya Mungu. Kwamba Yeye ananena kupitia njia nyingi ni ili kukimu mahitaji ya watu. Enzi ya Ufalme wa Milenia bado haijawadia—Enzi ya Ufalme wa Milenia inayozungumziwa ndiyo siku ambayo Mungu anapata utukufu. Baada ya kazi ya Yesu huko Yudea kukamilika, Mungu alihamisha kazi Yake hadi China bara na kuunda mpango mwingine. Yeye anafanya sehemu nyingine ya kazi Yake ndani yenu, Anafanya kazi ya kuwafanya watu kuwa watimilifu kwa maneno, na Anatumia maneno kuwafanya watu wapitie maumivu mengi na vilevile kupata neema nyingi ya Mungu. Hatua hii ya kazi itafanya kundi la washindi, na baada ya Yeye kufanya kundi hili la washindi, wataweza kuwa na ushuhuda kwa matendo Yake, wataweza kuishi kwa kuudhihirisha uhalisi, na kwa kweli watamridhisha Yeye na kuwa waaminifu Kwake hadi kifo, na kwa njia hii ndiyo Mungu atapata utukufu. Mungu anapopata utukufu—yaani, Anapokuwa amefanya kundi hili la watu kuwa timilifu—hiyo itakuwa Enzi ya Ufalme wa Milenia.
Yesu alikuwa duniani kwa miaka thelathini na mitatu na nusu, Alikuja kufanya kazi ya kusulubiwa, na kupitia kusulubiwa Mungu alipata sehemu moja ya utukufu Wake. Mungu alipokuja katika mwili, Aliweza kuwa mnyenyekevu na aliyefichika, na Aliweza kuvumilia mateso makubwa sana. Ingawa Alikuwa Mungu Mwenyewe, bado Alivumilia kila udhalilishaji na kila kashfa, na Alivumilia maumivu makubwa katika kupigiliwa misumari msalabani ili kukamilisha kazi ya ukombozi. Baada ya hatua hii ya kazi kuhitimishwa, ingawa watu waliona kwamba Mungu alikuwa amepata utukufu mkuu, huu haukuwa ukamilifu wa utukufu Wake; ilikuwa tu sehemu moja ya utukufu Wake, ambao Alikuwa amepata kutoka kwa Yesu. Ingawa Yesu aliweza kuvumilia mateso yote, kuwa mnyenyekevu na aliyefichika, na kusulubiwa kwa ajili ya Mungu, Mungu alipata tu sehemu moja ya utukufu Wake, na utukufu Wake ulipatikana katika Israeli. Mungu bado ana sehemu nyingine ya utukufu: kuja duniani kufanya kazi kwa vitendo na kulifanya kundi la watu kuwa timilifu. Wakati wa hatua ya kazi ya Yesu, Alifanya baadhi ya mambo ya miujiza, lakini hatua hiyo ya kazi haikuwa tu ili kutenda ishara na maajabu hata kidogo. Ilikuwa kimsingi kuonyesha kwamba Yesu aliweza kuteseka, na kusulubiwa kwa ajili ya Mungu, kwamba Yesu aliweza kuvumilia maumivu makubwa sana kwa sababu Alimpenda Mungu na kwamba, ingawa Mungu alimtelekeza Yeye, bado Alikuwa tayari kuyatoa maisha Yake yote kwa ajili ya mapenzi ya Mungu. Baada ya Mungu kukamilisha kazi Yake katika Israeli na Yesu kupigiliwa misumari msalabani, Mungu alipata utukufu, na Alikuwa ameshuhudia mbele ya Shetani. Ninyi hamjui wala hamjaona jinsi Mungu amekuwa mwili nchini China, kwa hivyo mnawezaje kuona kwamba Mungu amepata utukufu? Mungu amefanya kazi nyingi ya ushindi ndani yenu, na mmesimama imara. Hatua hii ya kazi ya Mungu kwa hivyo imefanikiwa, na hii ni sehemu ya utukufu wa Mungu. Ninyi mnaliona hili tu, na bado hamjafanywa kuwa watimilifu na Mungu, bado hamjampa Mungu mioyo yenu kabisa. Bado hamjauona utukufu huu kikamilifu; mnaona tu kwamba Mungu tayari ameshinda mioyo yenu, kwamba hamwezi kamwe kumwacha Yeye, na mtamfuata Mungu hadi mwisho kabisa na mioyo yenu haitabadilika, na kwamba huu ndio utukufu wa Mungu. Mnaona utukufu wa Mungu katika nini? Katika matokeo ya kazi Yake ndani ya watu. Watu wanaona kwamba Mungu anapendeza sana, wako na Mungu mioyoni mwao, na hawako tayari kumwacha Yeye, na huu ndio utukufu wa Mungu. Bidii ya ndugu na dada wa makanisa imeongezeka. Wanaweza kumpenda Mungu kutoka mioyoni mwao, na kuona uwezo mkubwa kupita kiasi wa kazi inayofanywa na Mungu, uwezo usio na kifani wa maneno Yake. Wanaona kwamba maneno Yake yana mamlaka, na kwamba Anaweza kutekeleza kazi Yake katika nchi ya mapepo ambayo ni China bara. Ingawa watu ni dhaifu, mioyo yao inasujudu mbele za Mungu na wako tayari kukubali maneno ya Mungu. Ingawa wao ni dhaifu na wasiostahili, wanaweza kuona kwamba maneno ya Mungu yanapendeza sana, na yanastahili sana kuthaminiwa nao. Huu ndio utukufu wa Mungu. Siku itakapofika ambapo watu watafanywa kuwa watimilifu na Mungu, na wataweza kujisalimisha mbele Zake, na wataweza kumtii Mungu kikamilifu, na kuacha matarajio na majaliwa yao mikononi mwa Mungu, basi sehemu ya pili ya utukufu wa Mungu itakuwa imepatikana kikamilifu. Yaani, wakati kazi ya Mungu wa vitendo imekamilika kikamilifu, kazi Yake nchini China bara itafikia kikomo. Yaani, wakati wale walioamuliwa kabla na kuchaguliwa na Mungu wamefanywa kuwa watimilifu, Mungu atakuwa amepata utukufu. Mungu alisema kwamba Ameleta sehemu ya pili ya utukufu Wake Mashariki, lakini hii haionekani kwa macho ya kawaida. Mungu ameleta kazi Yake Mashariki—tayari Amekuja Mashariki. Huu ni utukufu wa Mungu. Katika wakati wa sasa, ingawa kazi Yake bado haijakamilika, kwa sababu Mungu ameamua kufanya kazi, hakika itatimizwa. Mungu ameamua Atakamilisha kazi hii nchini China, na Ameazimia kuwafanya ninyi kuwa kamili. Hivyo, Amezuia njia zote zinazowezekana za kurudi nyuma kwenu—tayari Ameshinda mioyo yenu, na ni lazima uendelee iwe unataka au la, na mnapopatwa na Mungu, Mungu Anapata utukufu. Katika wakati wa sasa, Mungu bado Hajapata utukufu kamili, kwa sababu bado hamjafanywa kuwa kamili. Ingawa mioyo yenu imemrudia Mungu, bado kuna udhaifu mwingi katika mwili wenu, hamwezi kumridhisha Mungu, hamwezi kujali nia za Mungu, na bado mna mambo mengi hasi ambayo lazima myatupe mbali. Bado lazima mpitie majaribu na usafishaji mwingi—ni kwa njia hiyo tu ndiyo tabia zenu za maisha zinaweza kubadilika na mnaweza kupatwa na Mungu.