Tatizo Zito Sana: Usaliti (1)

Kazi Yangu iko karibu kukamilika. Miaka mingi ambayo tumekuwa pamoja imekuwa kumbukumbu isiyoweza kuvumilika. Nimeendelea kurudia maneno Yangu na Sijakoma kuendelea katika kazi Yangu mpya. Bila shaka, ushauri Wangu ni sehemu muhimu katika kila sehemu ya kazi Ninayoifanya. Bila ushauri Wangu, ninyi nyote mtapotea, na kuchanganyikiwa hata zaidi. Kazi Yangu sasa inakaribia kukamilika na ipo katika hatua yake ya mwisho; bado Nataka kufanya kazi fulani katika kutoa ushauri, yaani, kutoa baadhi ya maneno ya ushauri ili muyasikilize. Natumai tu kwamba hamtapoteza juhudi Zangu zenye maumivu na zaidi ya hayo, kwamba mnaweza kuelewa utunzaji wote na fikira ambazo Nimetumia, mkiyachukulia maneno Yangu kama msingi wa jinsi mnavyotenda kama binadamu. Iwe ni maneno ambayo mko tayari kuyasikiliza au la, iwe ni maneno ambayo mnafurahia kuyakubali au mnayakubali bila raha, lazima muyachukulie kwa uzito. Vinginevyo, tabia na mienendo yenu ya kawaida na isiyojali itanifadhaisha sana na, hata zaidi, itanichukiza Mimi. Natumai sana kwamba nyote mnaweza kuyasoma maneno Yangu tena na tena—mara elfu kadhaa—na hata kuyakariri. Ni kwa njia hiyo tu ndiyo hamtayaacha matarajio Yangu kwenu. Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishi namna hiyo sasa. Badala yake, nyote mmezama katika maisha ya anasa ya kula na kunywa hadi kushiba, na hakuna yeyote kati yenu anayeyatumia maneno Yangu kuusitawisha moyo na nafsi yake. Kwa sababu hii Nimefikia hitimisho kuhusu uso wa kweli wa mwanadamu: Mwanadamu anaweza kunisaliti wakati wowote, na hakuna yeyote anayeweza kuwa mwaminifu kabisa kwa maneno Yangu.

“Mwanadamu amepotoshwa sana na Shetani kiasi kwamba hana sura ya mwanadamu tena.” Watu wengi sasa wamepata utambuzi kiasi kuhusu msemo huu. Ninasema hivi kwa sababu “utambuzi” ambao Ninaurejelea hapa ni aina ya ukiri wa juu juu tu, ni kinyume na maarifa ya kweli. Kwa kuwa hakuna yeyote kati yenu anayeweza kujitathmini kwa usahihi wala kujichanganua kikamilifu, daima mnaamini nusu nusu, mnayashuku maneno Yangu. Lakini kwa wakati huu Ninatumia ukweli kuelezea tatizo kubwa zaidi mlio nalo, na hilo ni usaliti. Ninyi nyote mnajua neno “usaliti” kwa sababu watu wengi wamefanya jambo ambalo limemsaliti mwingine hapo awali, kama vile mume kumsaliti mke wake, mke kumsaliti mume wake, mwana kumsaliti baba yake, binti kumsaliti mama yake, mtumwa kumsaliti bwana wake, marafiki kusalitiana, jamaa kusalitiana, wauzaji kuwasaliti wanunuzi, na mengineyo. Mifano hii yote ina asili ya usaliti. Kwa kifupi, usaliti ni aina ya tabia ambayo inavunja ahadi, inakiuka kanuni za maadili, au kwenda kinyume na maadili ya binadamu, na ambayo inaonyesha kupoteza ubinadamu. Kwa ujumla, kama mwanadamu ambaye umezaliwa katika ulimwengu huu, utakuwa umewahi kufanya jambo ambalo linajumuisha ukiukaji wa ukweli, bila kujali kama unakumbuka kuwa umewahi kufanya jambo fulani ili kumsaliti mtu mwingine, au kama tayari umewasaliti wengine mara nyingi hapo awali. Kwa kuwa una uwezo wa kuwasaliti wazazi au marafiki zako basi una uwezo wa kuwasaliti wengine, na zaidi ya hayo una uwezo wa kunisaliti Mimi na kufanya mambo ambayo Ninayadharau. Kwa maneno mengine, usaliti si aina ya utovu wa maadili tu kwa nje, lakini ni kitu ambacho kinapingana na ukweli. Hiki ndicho hasa chanzo cha upinzani na uasi wa wanadamu dhidi Yangu. Hii ndiyo sababu Nimeifupisha katika maelezo yafuatayo: Usaliti ni asili ya mwanadamu. Asili hii ni adui wa kiasili kwa kila mtu anayekuwa sambamba na Mimi.

Tabia ambayo haiwezi kunitii kabisa ni usaliti. Tabia ambayo haiwezi kuwa na uaminifu Kwangu ni usaliti. Kunidanganya na kutumia uongo kunilaghai ni usaliti. Kujawa na dhana na kuzieneza kila mahali ni usaliti. Kutozilinda shuhuda na maslahi Yangu ni usaliti. Kutoa tabasamu za uongo wakati mtu ameniacha moyoni mwake ni usaliti. Tabia hizi ni mambo yote ambayo daima mna uwezo wa kuyafanya, na pia ni za kawaida kati yenu. Hakuna hata mmoja wenu anayeweza kufikiria kwamba hilo ni tatizo, lakini Mimi sifikirii hivyo. Siwezi kuchukulia usaliti wa mtu Kwangu kama jambo dogo, na zaidi ya hayo siwezi kulipuuza. Sasa, Nanapofanya kazi miongoni mwenu, mnakuwa wenye tabia ya aina hii—ikiwa siku itafika ambapo hakuna mtu wa kuwalinda, je, hamtakuwa kama wezi ambao wamejitangaza kuwa wafalme katika milima yao midogo? Hayo yatakapotokea na mkasababisha maafa, ni nani atakayekuwepo ili kusafisha baada yako? Unaweza kufikiri kwamba baadhi ya matendo ya usaliti ni matukio ya mara moja moja tu, si tabia yako endelevu, na haistahili kujadiliwa kwa uzito kama huo, ikikusababisha upoteze uso wako. Ikiwa unafikiria hivyo kweli, basi huna uwezo wa kupambanua. Kadri mtu anavyofikiria kwa njia hiyo, ndivyo anavyokuwa kielelezo na mfano halisi wa kuasi. Asili ya mtu ni maisha yake, ni kanuni ambayo anaitegemea ili kuendelea kuishi, na anashindwa kuibadilisha. Chukulia asili ya usaliti kama mfano—kama unaweza kufanya kitu ili kumsaliti ndugu au rafiki, hii inathibitisha kwamba ni sehemu ya maisha yako na hali ambayo ulizaliwa nayo. Hiki ni kitu ambacho hakuna mtu anayeweza kukikana. Kwa mfano, kama mtu anapenda kuiba vitu vya watu wengine, basi hii “kupenda kuiba” ni sehemu ya maisha yake. Ni kwamba tu wakati mwingine anaiba, na wakati mwingine haibi. Bila kujali kama anaiba au la, haiwezi kuthibitisha kwamba kuiba kwake ni aina Fulani tu yaya tabia. Badala yake, inathibitisha kwamba kuiba kwake ni sehemu ya maisha yake, yaani, ni asili yake. Baadhi ya watu watauliza: Kwa kuwa ni asili yake, basi kwa nini wakati mwingine anaona vitu vizuri lakini haviibi? Jibu ni rahisi sana. Kuna sababu nyingi kwa nini haibi, inaweza kuwa bidhaa ni kubwa mno kwake kuinyakua akitazamwa na watu, au hakuna wakati mzuri wa kutenda, au bidhaa ni ghali sana, imelindwa vikali, au hajavutiwa sana na kitu kizuri kama hicho, au bado hajafikiria matumizi ya kitu hicho, na mengineyo. Sababu hizi zote zinawezekana. Lakini haijalishi ni nini, ikiwa wanaiba kitu au la, hio haiwezi kuthibitisha kuwa hilo ni wazo lililomjia akilini kwa muda tu. Kinyume chake, hii ni sehemu ya asili yake ambayo ni ngumu kuibadilisha kuwa bora. Mtu kama huyo haridhiki na kuiba mara moja tu, lakini mawazo ya kudai vitu vya wengine kama vyake huamshwa wakati wowote anapokutana na kitu kizuri au hali inayofaa. Hii ndiyo sababu Nasema kwamba wazo hili haliinuki mara moja moja tu, lakini linatokana na asili ya mtu mwenyewe.

Mtu yeyote anaweza kutumia maneno na matendo yake mwenyewe kuwakilisha sura yake halisi. Sura hii ya kweli bila shaka ni asili yake. Kama wewe ni mtu anayezungumza kwa njia ya kuzunguka, basi una asili yenye hila. Kama asili yako ni ya udanganyifu, basi unatenda kwa njia ya ujanja, na unafanya iwe rahisi sana kwa wengine kudanganywa na wewe. Kama asili yako ni ovu, maneno yako yanaweza kupendeza kusikiliza, lakini matendo yako hayawezi kuficha hila zako mbaya. Kama asili yako ni ya uvivu, basi yote unayosema yanalenga kukwepa majukumu kwa sababu ya uzembe na uvivu wako, na matendo yako yatakuwa ya polepole na ya kizembe, na utakuwa mahiri kabisa katika kuuficha ukweli. Kama asili yako ni ya kuwahurumia wengine, basi maneno yako yatakuwa yenye busara, na matendo yako, pia, yatapatana vyema na ukweli. Kama asili yako ni ya uaminifu, basi maneno yako kwa kakika ni ya kweli na jinsi unavyotenda ni sahihi, pasipokuwa na chochote ambacho kinaweza kumfanya bwana wako awe na wasiwasi. Kama asili yako ni ya tamaa mbaya au tamaa ya pesa, basi moyo wako mara nyingi utajazwa na mambo haya, na bila kujua utatenda matendo yaliyopotoka, yasiyo na maadili ambayo watu hawatayasahau kirahisi na ambayo yatawachukiza watu. Kama vile Nilivyosema, ikiwa una asili ya usaliti, basi ni ngumu kujiondoa kutoka kwayo. Msiamini kwa bahati kwamba ikiwa hamjawakosea wengine, basi hamna asili ya usaliti. Kama hivyo ndivyo unavyofikiria, basi kwa kweli, unaasi. Maneno ambayo Nimenena kila wakati yamewalenga watu wote, sio tu mtu mmoja au aina ya mtu. Kwa sababu tu hujanisaliti Mimi katika jambo moja haimaanishi kwamba hauwezi kunisaliti Mimi katika jambo jingine. Baadhi ya watu, wakati wa matatizo katika ndoa zao, wanapoteza ujasiri wao katika kutafuta ukweli. Baadhi ya watu wanaacha wajibu wao wa kuwa waaminifu Kwangu wakati wa kuvunjika kwa familia. Baadhi ya watu huniacha kwa ajili ya kutafuta wakati wa furaha na msisimko. Baadhi ya watu ni afadhali waanguke katika korongo lenye giza kuliko kuishi katika mwanga na kupata furaha ya kazi ya Roho Mtakatifu. Baadhi ya watu hupuuza ushauri wa marafiki kwa ajili ya kuridhisha tamaa zao za mali, na hata sasa hawawezi kukubali makosa yao na kubadili mienendo yao. Baadhi ya watu wanaishi tu kwa muda chini ya jina Langu ili wapate ulinzi Wangu, wakati wengine wanajitolea kidogo tu Kwangu kwa kulazimishwa kwa sababu wanashikilia uzima na kuogopa kifo. Je, haya na matendo mengine maovu, ambayo, zaidi ya hayo, hayana uadilifu, si tabia tu ambazo watu wamenisaliti nazo kwa muda mrefu ndani ya mioyo yao? Bila shaka, Ninajua watu hawapangi mapema kunisaliti; usaliti wao ni ufunuo wa kiasili wa asili zao. Hakuna mtu anayetaka kunisaliti, na zaidi ya hayo hakuna mtu aliye na furaha kwa sababu amefanya kitu kinachonisaliti. Badala yake, wanatetemeka kwa hofu, sivyo? Kwa hivyo, je, mnafikiria jinsi ya kukomboa usaliti huu, na jinsi ya kubadilisha hali ya sasa?

Iliyotangulia:  Jinsi ya Kumjua Mungu Duniani

Inayofuata:  Tatizo Zito Sana: Usaliti (2)

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger