Tatizo Kubwa Sana: Usaliti (2)

Asili ya mwanadamu ni tofauti kabisa na kiini Changu, kwa maana asili potovu ya mwanadamu inatokana kabisa na Shetani; asili ya mwanadamu imefinyangwa na kupotoshwa na Shetani. Yaani, mwanadamu anaishi chini ya ushawishi wa uovu na ubaya wa Shetani. Mwanadamu hakui katika dunia ya ukweli au mazingira matakatifu, sembuse mwanadamu kuishi katika nuru. Kwa hivyo, haiwezekani kwa mtu yeyote kuwa na ukweli ndani ya asili yake tangu wakati wa kuzaliwa, na sembuse mtu yeyote kuzaliwa na kiini kinachomwogopa na kumtii Mungu. Kinyume chake, watu wana asili inayompinga Mungu, inayomwasi Mungu, na isiyokuwa na upendo kwa ukweli. Asili hii ndiyo tatizo Ninalotaka kujadili—usaliti. Usaliti ndio chanzo cha upinzani wa kila mtu kwa Mungu. Hili ni tatizo ambalo lipo tu ndani ya mwanadamu, na si ndani Yangu. Wengine watauliza: Kwa kuwa watu wote wanaishi duniani kama vile Kristo anavyoishi, kwa nini watu wote wana asili zinazomsaliti Mungu, lakini Kristo hana? Hili ni tatizo ambalo lazima lielezwe wazi kwenu.

Msingi wa kuwepo kwa binadamu ndio roho kuingia katika mwili mpya tena na tena. Yaani, kila mtu anapata maisha ya binadamu katika mwili wakati roho yake inapoingia katika mwili mpya. Baada ya mwili wa mtu kuzaliwa, maisha yake yanaendelea hadi mwili hatimaye unapofikia kikomo chake, ambacho ndicho wakati wa mwisho, ambapo roho inaliacha gamba lake. Mchakato huu unajirudia tena na tena, huku roho ya mtu ikija na kwenda mara kwa mara, na hivyo kuwepo kwa binadamu kunadumishwa. Maisha ya mwili pia ni maisha ya roho ya mwanadamu, na roho ya mwanadamu ndiyo inayodumisha kuwepo kwa mwili wa mwanadamu. Yaani, maisha ya kila mtu yanatokana na roho yake, hayamo ndani ya mwili kiasili. Hivyo, asili ya mwanadamu inatokana na roho, si na mwili. Ni roho ya kila mtu tu inayojua jinsi ambavyo imepitia vishawishi, mateso, na upotovu wa Shetani. Mambo haya hayawezi kujulikana kwa mwili wa mwanadamu. Kwa hivyo, binadamu bila kujua wanazidi kuwa wenye giza, wanazidi kuwa wachafu, na wanazidi kuwa waovu, huku umbali kati ya mwanadamu na Mimi ukizidi kuongezeka, na maisha ya binadamu yanazidi kuwa ya giza. Shetani anashikilia roho za binadamu katika mikono yake, kwa hivyo, ni wazi kwamba mwili wa mwanadamu pia umevamiwa na Shetani. Mwili kama huo na binadamu kama hao wanawezaje kutompinga Mungu? Wanawezaje kulingana na Yeye kiasili? Sababu iliyonifanya Nimtupe Shetani hewani ni kwamba alinisaliti Mimi. Binadamu, basi, wanawezaje kuepuka kuhusika? Hii ndiyo sababu usaliti ni asili ya mwanadamu. Ninaamini kwamba punde tu mnapoelewa hoja hii, mnapaswa pia kuwa na kiasi fulani cha imani katika kiini cha Kristo. Mwili unaovaliwa na Roho wa Mungu ni mwili wa Mungu Mwenyewe. Roho wa Mungu ni mkuu kuliko vyote; Yeye ni mwenyezi, mtakatifu, na mwenye haki. Vilevile, mwili Wake pia ni mkuu kuliko vyote, mwenyezi, mtakatifu, na wenye haki. Mwili kama huo unaweza tu kufanya kile kilicho cha haki na chenye manufaa kwa binadamu, kile kilicho kitakatifu, kitukufu, na chenye nguvu; Yeye hawezi kufanya chochote kinachokiuka ukweli, kinachokiuka haki ya kimaadili, sembuse Yeye kufanya chochote ambacho kingemsaliti Roho wa Mungu. Roho wa Mungu ni mtakatifu, na hivyo mwili Wake hauwezi kupotoshwa na Shetani; mwili Wake una kiini tofauti na mwili wa mwanadamu. Kwa maana ni mwanadamu, si Mungu, anayepotoshwa na Shetani, na Shetani hangeweza kamwe kuupotosha mwili wa Mungu Mwenyewe. Hivyo, licha ya ukweli kwamba mwanadamu na Kristo wanaishi katika nafasi ile ile, ni mwanadamu tu ndiye anayeweza kukaliwa na kutumiwa na Shetani, na kudhuriwa na hila za Shetani. Kinyume chake, Kristo hawezi kamwe kupotoshwa na Shetani. kwa sababu Shetani hatawahi kuwa na uwezo wa kupaa hadi mahali pa juu kabisa, na hatawahi kumkaribia Mungu. Katika wakati wa sasa, ninyi nyote mnapaswa kuelewa kwamba ni binadamu tu waliopotoshwa na Shetani ndio wanaonisaliti Mimi. Usaliti hautawahi kuwa suala linalomhusisha Kristo hata kidogo.

Roho zote zilizopotoshwa na Shetani zinashikwa utumwani katika nguvu za Shetani. Ni wale tu wanaomwamini Kristo ndio ambao wametenganishwa, wameokolewa kutoka katika kambi ya Shetani, na kuletwa katika ufalme wa wakati wa sasa. Watu hawa hawaishi tena chini ya ushawishi wa Shetani. Hata hivyo, asili ya mwanadamu bado imekita mizizi katika mwili wa mwanadamu, yaani, ingawa roho zenu zimeokolewa, asili yenu bado iko kama ilivyokuwa hapo awali, na uwezekano kwamba mtanisaliti Mimi unabaki asilimia mia moja. Hii ndiyo sababu kazi Yangu inachukua muda mrefu sana, kwa kuwa asili yenu ni ya ukaidi na ni vigumu kubadilika. Ninyi nyote sasa mnapitia magumu kwa kadiri ya uwezo wenu mnapotekeleza wajibu wenu, lakini ukweli usiopingika ni kwamba kila mmoja wenu anaweza kunisaliti Mimi na kurudi katika nguvu za Shetani, kurudi katika kambi yake na kurudi katika maisha yenu ya zamani. Wakati huo, haitawezekana kwenu kuonyesha chembe ya ubinadamu au mfano wa mwanadamu, kama mnavyofanya sasa. Katika hali mbaya kabisa, mtaangamia na, zaidi ya hayo, mtahukumiwa kwenye laana ya milele, mtaadhibiwa vikali, hamtaingia katika mwili mpya tena kamwe. Hili ndilo tatizo lililowekwa mbele yenu. Ninawakumbusha kwa namna hii, kwanza, ili kwamba kazi Yangu isiwe imefanyika bure, na pili, ili kwamba ninyi nyote mweze kuishi katika siku za nuru. Kwa kweli, iwapo kazi Yangu imefanyika bure si kiini cha tatizo. Kilicho muhimu ni kwamba mnaweza kuwa na maisha ya furaha na mustakabali mzuri. Kazi Yangu ni kazi ya kuokoa roho za watu. Ikiwa roho yako itaanguka mikononi mwa Shetani, mwili wako hautaishi kwa amani. Ikiwa Ninalinda mwili wako, roho yako pia hakika itakuwa chini ya utunzaji Wangu. Ikiwa kweli Ninakuchukia, mwili wako na roho yako vitaanguka mara moja mikononi mwa Shetani. Je, unaweza kufikiria hali yako wakati huo? Ikiwa, siku moja, maneno Yangu hayatakuwa na athari kwenu, basi Nitawakabidhi ninyi nyote kwa Shetani, na kumruhusu azidishe mateso yanayowapata hadi hasira Yangu itakapokuwa imetoweka kabisa, au Nitawaadhibu binafsi ninyi binadamu msioweza kukombolewa, kwa maana mioyo yenu inayonisaliti Mimi itakuwa haijabadilika kamwe.

Ninyi nyote sasa mnapaswa kujichunguza haraka iwezekanavyo, ili kuona ni kiasi gani cha usaliti dhidi Yangu kimesalia ndani yenu. Ninasubiri kwa hamu jibu lenu. Msiwe wa kijuujuu tu katika kushughulika na Mimi. Mimi sichezi michezo na watu kamwe. Nikisema nitafanya jambo basi hakika Nitalifanya. Natumaini kila mmoja wenu atakuwa mtu anayechukulia maneno Yangu kwa uzito, na asifikiri kana kwamba ni hadithi za kubuniwa za kisayansi. Ninachotaka ni vitendo halisi kutoka kwenu, si mawazo yenu ya kubuni. Kisha, ni lazima myajibu maswali Yangu, ambayo ni kama yafuatayo:

1. Ikiwa wewe ni mtendaji huduma kweli, je, unaweza kunitumikia Mimi kwa kujitoa, bila chembe ya kufanya mambo kijuujuu tu au ya uhasi?

2. Ukigundua Sijawahi kukuthamini, je, bado utaweza kubaki na kunitumikia Mimi maisha yako yote?

3. Ikiwa bado Ninakutendea kwa ubaridi sana licha ya wewe kutumia bidii nyingi, je, utaweza kuendelea kunifanyia Mimi kazi bila kujulikana?

4. Ikiwa, baada ya wewe kujitumia kiasi kwa ajili Yangu, Sijatimiza matakwa yako madogo, je, utavunjika moyo na kukatishwa tamaa na Mimi, au hata kuanza kujaa kinyongo na kupiga kelele za matusi?

5. Ikiwa umekuwa mwaminifu sana daima, ukiwa na upendo mwingi Kwangu, lakini unapata mateso makali kutokana na ugonjwa, matatizo ya kifedha, kutelekezwa na marafiki na jamaa zako, au misiba mingine yoyote maishani, je, uaminifu na upendo wako Kwangu bado vitaendelea?

6. Ikiwa hakuna chochote ambacho umewazia moyoni mwako kinalingana na kile ambacho Nimefanya, unapaswa kuitembeaje njia yako ya baadaye?

7. Ikiwa hupati chochote kati ya vitu ulivyotarajia kupata, je, unaweza kuendelea kuwa mfuasi Wangu?

8. Ikiwa hujawahi kuelewa kusudi na umuhimu wa kazi Yangu, je, unaweza kuwa mtu mtiifu ambaye hatoi hukumu wala kufikia hitimisho kiholela?

9. Je, unaweza kuthamini maneno yote ambayo Nimesema na kazi yote ambayo Nimefanya wakati Nimekuwa pamoja na mwanadamu?

10. Je, unaweza kuwa mfuasi Wangu mwaminifu, ukiwa tayari kuvumilia maisha ya mateso kwa ajili Yangu hata kama hutapata chochote?

11. Kwa ajili Yangu, je, unaweza kuacha kufikiria, kupanga, au kujitayarisha kwa ajili ya njia yako ya kuendelea kuishi katika siku zijazo?

Maswali haya yanawakilisha matakwa Yangu ya mwisho kwenu, na Natumaini ninyi nyote mnaweza kunipa Mimi majibu. Ikiwa umetimiza jambo moja au mawili ambayo maswali haya yanakutaka kuyafanya, basi bado unahitaji kuendelea kujitahidi. Ikiwa huwezi kutimiza hata moja ya matakwa haya, hakika wewe ni aina ya mtu ambaye atatupwa kuzimu. Kwa watu kama hao, Sina haja ya kusema chochote zaidi, kwa maana hakika wao ni watu wasioweza kulingana na Mimi. Ninawezaje kumweka mtu katika nyumba Yangu ambaye anaweza kunisaliti Mimi chini ya hali yoyote? Kuhusu wale ambao bado wanaweza kunisaliti Mimi katika hali nyingi, Nitaangalia utendaji wao kabla ya kufanya mipango mingine. Hata hivyo, wote wanaoweza kunisaliti Mimi, haijalishi katika hali gani, Sitawahi kuwasahau; Nitamkumbuka kila mmoja wao moyoni Mwangu, na kusubiri fursa ya kuwalipa kwa matendo yao maovu. Matakwa ambayo Nimeyatoa yote ni masuala ambayo ni lazima myachunguze ndani yenu wenyewe. Natumaini ninyi nyote mnaweza kuyafikiria kwa uzito na msishughulike na Mimi kijuujuu tu. Katika siku za usoni, Nitalinganisha majibu mliyonipa Mimi na matakwa Yangu. Kufikia wakati huo, Sitahitaji chochote zaidi kutoka kwenu na Sitawapa onyo tena la dhati. Badala yake, Nitatumia mamlaka Yangu: Wale wanaopaswa kubakizwa watabakizwa, wale wanaopaswa kutuzwa watatuzwa, wale wanaopaswa kukabidhiwa kwa Shetani watakabidhiwa kwa Shetani, wale wanaopaswa kuadhibiwa vikali wataadhibiwa vikali, na wale wanaopaswa kuangamia wataangamizwa. Hivyo, hakutakuwa tena na mtu yeyote wa kunisumbua Mimi katika siku Zangu. Je, unaamini maneno Yangu? Je, unaamini katika malipo? Je, unaamini kwamba Nitawaadhibu wale wote waovu wanaonidanganya na kunisaliti Mimi? Je, unatumaini siku hiyo ifike mapema zaidi au ifike baadaye? Je, wewe ni mtu anayeogopa sana adhabu, au mtu ambaye angependelea kunipinga Mimi hata kama inamaanisha kuvumilia adhabu? Siku hiyo itakapofika, je, unaweza kufikiria kama utaishi katikati ya shangwe na vicheko, au kama utalia na kusaga meno yako? Unatumaini kukutana na matokeo ya aina gani? Je, umewahi kufikiria kwa uzito kama unaniamini Mimi asilimia mia moja au unanitilia shaka Mimi asilimia mia moja? Je, umewahi kufikiria kwa makini ni matokeo ya aina gani na hatima ambayo matendo na mwenendo wako vitaleta kwako? Je, unatumaini sana kuwa maneno Yangu yote yatatimia moja baada ya jingine, au unaogopa sana kuwa maneno Yangu yatatimia moja baada ya jingine? Ikiwa unatumaini kwamba Nitaondoka hivi karibuni ili kutimiza maneno Yangu, unapaswa kuyachukuliaje maneno na matendo yako mwenyewe? Ikiwa hutumainii kuondoka Kwangu na hutumainii maneno Yangu yote kutimia mara moja, kwa nini basi unaniamini Mimi? Je, unajua kweli kwa nini unanifuata Mimi? Ikiwa sababu yako ni kupanua tu upeo wako, hakuna haja ya wewe kujisumbua hivyo. Ikiwa ni kubarikiwa na kuepuka maafa yanayokuja, kwa nini huna wasiwasi kuhusu mwenendo wako mwenyewe? Kwa nini hujiulizi kama unaweza kutimiza matakwa Yangu? Kwa nini pia hujiulizi kama una sifa za kurithi baraka zitakazokuja?

Iliyotangulia:  Tatizo Kubwa Sana: Usaliti (1)

Inayofuata:  Mnapaswa Kutafakari Matendo Yenu

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger