Mungu Ndiye Chanzo cha Uzima wa Mwanadamu

Kuanzia wakati unapokuja ulimwenguni humu ukilia, unaanza kutimiza majukumu yako. Kwa ajili ya mpango wa Mungu na amrisho Lake, unafanya wajibu wako na kuanza safari yako ya maisha. Haijalishi asili yako ilivyo, na haijalishi safari iliyo mbele yako ilivyo, kwa vyovyote vile, hakuna anayeweza kuepuka mipango na mipangilio ya Mbinguni, na hakuna anayeweza kudhibiti hatima yake mwenyewe, kwani ni Yule tu mwenye mamlaka juu ya vitu vyote ndiye anayeweza kufanya kazi hiyo. Tangu kuwepo kwa mwanadamu hapo mwanzo, Mungu daima amekuwa Akifanya kazi Yake kwa namna hii, Akiusimamia ulimwengu, na kuelekeza sheria za mabadiliko kwa vitu vyote na mwelekeo wa kusonga kwa vitu hivyo. Kama vitu vyote, mwanadamu kwa ukimya na bila kujua anasitawishwa kwa utamu na mvua na umande kutoka kwa Mungu; kama vitu vyote, mwanadamu bila kujua, anaishi chini ya mpango wa mkono wa Mungu. Moyo na roho ya mwanadamu vimo katika mfumbato wa Mungu, na kila kitu cha maisha yake kinatazamwa machoni pa Mungu. Bila kujali kama unayaamini haya yote au la, kitu chochote na vitu vyote, viwe hai au vilivyokufa, vitahamishwa, vitabadilishwa, vitafanywa vipya, na vitapotea kulingana na fikira za Mungu. Hivi ndivyo ambavyo Mungu ana mamlaka juu ya vitu vyote.

Usiku unapojongea polepole, mwanadamu hafahamu, kwa kuwa moyo wa mwanadamu hauwezi kujua jinsi usiku unavyojongea, wala kule unakotokea. Usiku unapotoweka polepole, mwanadamu anaukaribisha mwanga wa mchana, lakini kuhusu kule ambako mwanga umetokea, na jinsi ambavyo umeliondoa giza la usiku, moyo wa mwanadamu ni usiojua hata zaidi, na hata unatambua machache zaidi. Mabadiliko haya ya kurudiarudia ya mchana na usiku yanamtoa mwanadamu kutoka katika kipindi kimoja hadi kingine, kutoka katika muktadha wa enzi moja hadi mwingine, huku yakihakikisha kwamba kazi ya Mungu katika kila kipindi na mpango Wake wa kila enzi unatekelezwa. Mwanadamu ametembea katika vipindi hivi vyote tofauti akimfuata Mungu, lakini bado hafahamu kwamba Mungu ana mamlaka juu ya hatima ya vitu vyote na viumbe hai, wala jinsi Mungu anavyopanga na kuelekeza vitu vyote. Hili limemkwepa mwanadamu wa wakati wa sasa na hata mwanadamu wa wakati wa zamani. Kuhusu ni kwa nini, si kwa sababu matendo ya Mungu yamefichika sana, wala kwa sababu mpango wa Mungu bado haujakamilika, lakini ni kwa sababu moyo na roho ya mwanadamu viko mbali sana na Mungu, kiasi cha kwamba mwanadamu anabaki katika kumtumikia Shetani hata “anapomfuata Mungu”—na bado halijui hili. Hakuna anayetafuta nyayo za Mungu kwa utendaji na kuonekana kwa Mungu, na hakuna aliye tayari kuishi katika utunzaji na ulinzi wa Mungu. Badala yake, wako tayari kukubali kufisidi kwa Shetani, ibilisi mwovu, ili kubadilika kupatana na dunia hii, na kanuni za kuishi ambazo binadamu huyu mwovu hufuata. Katika hatua hii, moyo na roho ya mwanadamu vinakuwa ushuru ambao mwanadamu anamtolea shetani na kuwa chakula cha Shetani. Hata zaidi, moyo wa binadamu na roho yake zinakuwa mahali ambapo Shetani anaishi, na vile vile uwanja wake wa kuchezea unaofaa. Hivyo ndivyo mwanadamu bila kujua anapoteza ufahamu wake wa kanuni za kujiendesha, na wa thamani na umuhimu wa kuwepo kwa binadamu. Sheria za Mungu na agano kati ya Mungu na mwanadamu polepole vinakuwa vyenye ukungu katika moyo wa mwanadamu, na anaacha kumtafuta au kumsikiliza Mungu. Muda unavyopita, mwanadamu amepoteza ufahamu wake wa umuhimu wa Mungu kumuumba, wala haelewi maneno kutoka kinywani mwa Mungu na yote yanayotoka kwa Mungu. Kisha mwanadamu anaanza kupinga sheria na masharti ya Mungu, na moyo wake na roho yake vinakufa ganzi…. Mungu amempoteza mwanadamu ambaye Alimuumba hapo mwanzo, na mwanadamu anapoteza mzizi aliokuwa nao hapo awali: Hii ndiyo tanzia ya jamii hii ya binadamu. Kwa hakika, tangu mwanzo hadi sasa, Mungu ameandaa tanzia kwa ajili ya wanadamu, ambamo mwanadamu ndiye mhusika mkuu na mwathirika. Na hakuna anayeweza kujibu swali la ni nani ndiye mwelekezi wa tanzia hii.

Katika ulimwengu mpana, bahari hugeuka kuwa mashamba, na mashamba kuwa bahari, mara nyingi zisizohesabika. Isipokuwa Yeye aliye na mamlaka juu ya kila kitu kati ya vitu vyote, hakuna yeyote anayeweza kuongoza na kuelekeza mbari hii ya binadamu. Hakuna “mwenye uwezo” wa kumenyeka au kufanya maandalizi kwa ajili ya mbari hii ya binadamu, sembuse kuwepo kwa yeyote anayeweza kuiongoza mbari hii ya binadamu kusonga kuelekea hatima ya nuru na kujinasua kutoka katika ukosefu wa haki wa ulimwengu wa mwanadamu. Mungu anasikitikia mustakabali wa wanadamu, Anahuzunishwa na kuanguka kwa wanadamu, na anaumizwa kwamba wanadamu wanatembea, hatua kwa hatua, kuelekea uozo na njia isiyo na marejeo. Hakuna mtu ambaye amewahi kufikiria hili: Je, binadamu kama huyu, ambaye ameuvunja moyo wa Mungu kabisa na kumtelekeza ili kumtafuta yule mwovu, anaweza kuwa akielekea wapi? Ni kwa sababu hii hasa kwamba hakuna anayejaribu kuhisi hasira ya Mungu, kwamba hakuna anayetafuta njia impendezayo Mungu au kujaribu kumkaribia Mungu, na zaidi ya hayo kwamba hakuna anayejaribu kuelewa huzuni na maumivu ya Mungu. Hata baada ya kusikia sauti ya Mungu, mwanadamu anaendelea katika njia yake mwenyewe, anaendelea kugeuka mbali na Mungu, akikwepa neema na utunzaji wa Mungu, na kuepuka ukweli Wake, akipendelea kujiuza kwa Shetani, adui wa Mungu. Na ni nani ambaye amewahi kufikiria, ikiwa mwanadamu atang’ang’ania katika ukaidi wake, jinsi Mungu atakavyowatendea wanadamu hawa ambao wanampuuza Yeye kabisa? Hakuna anayejua kwamba sababu ya vikumbusho na mahimizo ya Mungu yanayorudiwa kwa mwanadamu ni kwamba Yeye ameandaa mikononi Mwake majanga ambayo hayajawahi kuonekana hapo awali, yale ambayo hayatavumilika kwa mwili na roho ya mwanadamu, si adhabu ya mwili tu, bali yale yanayolenga roho ya mwanadamu. Unahitaji kujua hili: Mungu ataiachilia hasira ya aina gani mpango Wake utakaposhindikana, na wakati vikumbusho na mahimizo Yake hayatalipwa? Itakuwa kama kitu ambacho hakijawahi kupitiwa au kushuhudiwa na kiumbe yeyote aliyeumbwa. Na kwa hivyo Ninasema, majanga haya hayana kifani, na hayatarudiwa kamwe. Kwa maana mpango wa Mungu ni kuumba wanadamu mara hii moja tu, na kuwaokoa wanadamu mara hii moja tu. Hii ndiyo mara ya kwanza, na pia ndiyo ya mwisho. Kwa hivyo, hakuna anayeweza kuelewa nia za bidii za kazi na matarajio yenye ari ambayo kwayo Mungu anawaokoa wanadamu wakati huu.

Mungu aliuumba ulimwengu huu na kumleta mwanadamu, kiumbe hai ambaye Alimtia uzima ndani yake. Kufuatia, mwanadamu akaja kuwa na wazazi na jamaa na hakuwa mpweke tena. Tangu mwanadamu alipotazama kwa mara ya kwanza ulimwengu huu wa maada, alikusudiwa kuishi ndani ya amrisho la Mungu. Ni pumzi ya uzima inayotoka kwa Mungu ambayo inamtegemeza kila kiumbe hai katika kipindi cha ukuaji hadi kufikia utu uzima. Wakati wa mchakato huu, hakuna anayehisi kwamba mwanadamu yupo na anakua chini ya uangalizi wa Mungu; lakini badala yake, anaamini kwamba mwanadamu anakua chini ya rehema ya utunzaji wa wazazi, na kwamba ni silika yake mwenyewe ya maisha inayoendesha ukuaji. Hii ni kwa sababu mwanadamu hajui ni nani aliyemtunukia maisha yake, au ni wapi yalikotoka, sembuse hata jinsi ambavyo silika ya maisha inavyoweza kusababisha miujiza. Anajua tu kwamba chakula ndicho msingi wa kuendelea kwa maisha yake, kwamba uvumilivu ndio chanzo cha kuwepo kwa maisha yake, na kwamba imani zilizopo katika akili yake ndizo mtaji ambao kuendelea kwake kuishi kunategemea. Mwanadamu hajui kabisa kuhusu neema na riziki za Mungu, na ni kwa njia hii ndiyo yeye hufuja uzima aliopewa na Mungu…. Hakuna mtu hata mmoja, ambaye Mungu humchunga usiku na mchana, ambaye huchukua hatua ya kumwabudu. Mungu anaendelea tu kufanya kazi juu ya mwanadamu, ambaye hakuna matarajio yoyote kutoka kwake, kama jinsi ambavyo Amepanga. Anafanya hivyo kwa matumaini kwamba siku moja, mwanadamu ataamka kutoka katika ndoto yake na kwa ghafla aitambue thamani na maana ya maisha, gharama ambayo Mungu alilipa kwa yote ambayo Amemkirimu, na shauku aliyo nayo Mungu akitamani sana mwanadamu ageuke amrudie Yeye. Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuchunguza siri zinazohusiana na asili na kuendelea kwa maisha ya mwanadamu. Ni Mungu tu, ambaye Anaelewa yote haya, kwa kimya Anavumilia maumivu na mapigo yanayoletwa na mwanadamu, ambaye amepokea kila kitu kutoka kwa Mungu lakini yeye hana shukrani. Mwanadamu anafurahia yote ambayo maisha huleta kama jambo la uhakika, na, vivyo hivyo, ni “jambo la hakika,” kwamba Mungu anasalitiwa na mwanadamu, Anasahaulika na mwanadamu, na kutozwa kwa nguvu na mwanadamu. Je, inaweza kuwa kwamba mpango wa Mungu una umuhimu kama huo kweli? Je, inaweza kuwa kwamba mwanadamu, kiumbe huyu aliye hai ambaye alitoka katika mkono wa Mungu, ni wa maana namna hiyo kweli? Mpango wa Mungu kwa hakika ni muhimu kabisa; hata hivyo, kiumbe huyu aliye hai aliyeumbwa na mkono wa Mungu yupo kwa ajili ya mpango Wake. Kwa hivyo, Mungu hawezi kuuharibu mpango Wake kwa sababu Anaichukia mbari ya wanadamu. Ni kwa ajili ya mpango Wake na kwa ajili ya pumzi aliyotoa ndiyo maana Mungu anavumilia mateso yote, si kwa ajili ya mwili wa mwanadamu ila ni kwa sababu ya uzima wa mwanadamu. Anafanya hivyo si ili kurudisha mwili wa mwanadamu bali uzima Aliopuliza. Huu ndio mpango Wake.

Wale wote wanaokuja katika ulimwengu huu lazima wapitie uzima na kifo, na wengi wao wamepitia mzunguko wa kifo na kuzaliwa upya. Wale wanaoishi watakufa hivi karibuni na wafu watarejea karibuni. Yote haya ni safari ya maisha iliyopangwa na Mungu kwa ajili ya kila kiumbe hai. Lakini, mchakato huu na mzunguko huu ndio ukweli hasa ambao Mungu anataka mwanadamu autazame: kwamba uzima ambao mwanadamu amepewa na Mungu hauna mwisho, hauzuiliwi na mwili, wakati, au nafasi. Hivyo ndivyo lilivyo fumbo la maisha aliyopewa mwanadamu na Mungu, na ni thibitisho kwamba maisha yalikuja kutoka Kwake. Ingawa watu wengi huenda wasiamini kwamba uzima wa mwanadamu ulitoka kwa Mungu, mwanadamu bila kuepuka anafurahia yote yatokayo kwa Mungu, iwe anaamini au anakana uwepo Wake. Siku moja, Mungu akibadili mawazo Yake ghafla na atake kurudisha kila kitu kilichoko ardhini na kuuchukua tena uzima Alioutoa, basi vyote havitaendelea kuwepo. Mungu hutumia uzima Wake kukimu vitu vyote, vyenye uzima na visivyo na uzima, akivileta vyote katika utaratibu mzuri kwa nguvu Zake kuu na mamlaka Yake—huu ni ukweli ambao hauwezi kuwaziwa wala kufahamika na yeyote. Ukweli huu usioweza kueleweka ni udhihirisho halisi wa, na thibitisho la nguvu za uzima wa Mungu. Sasa hebu Nikuambie siri: Ukuu wa uzima wa Mungu na nguvu za uzima Wake haziwezi kueleweka na kiumbe yeyote aliyeumbwa. Hivi ndivyo ilivyo sasa, kama ilivyokuwa zamani, na ndivyo itakavyokuwa nyakati zijazo. Siri ya pili Nitakayokufunulia ni hii: Chanzo cha uzima kwa viumbe vyote kinatoka kwa Mungu; bila kujali jinsi vinavyoweza kuwa tofauti katika umbo la uzima au muundo, na haijalishi wao ni viumbe wa aina gani, hakuna kiumbe anayeweza kwenda kinyume na mkondo wa uzima uliowekwa na Mungu. Kwa vyovyote vile, kile Ninachotaka ni mwanadamu aweze kuelewa hili: Bila utunzaji, ulinzi, na ruzuku ya Mungu, mwanadamu hawezi kupokea yote aliyokusudiwa kupokea, hata ajitahidi kwa bidii vipi au kupambana kwa jitihada kubwa. Bila riziki ya uzima kutoka kwa Mungu, mwanadamu anapoteza thamani ya kuishi na maana ya maisha. Je, Mungu angewezaje kumruhusu mwanadamu, anayepoteza thamani ya maisha Yake kwa namna ya upuuzi, awe asiyejali kabisa? Kama vile Nilivyosema hapo awali: Usisahau kwamba Mungu ndiye chanzo cha uzima wako. Ikiwa mwanadamu atashindwa kuthamini yote ambayo Mungu Amemfanyia, mbali na Mungu kuchukua kile Alichotoa hapo mwanzo, pia Atamfanya mwanadamu amlipe fidia mara mbili ya gharama zote Alizotoa.

Mei 26, 2003

Iliyotangulia:  Mnapaswa Kutafakari Matendo Yenu

Inayofuata:  Kutanafusi kwa Mwenye Uweza

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger