Fumbo la Kupata Mwili (3)

Mungu anapotekeleza kazi Yake, Yeye haji kushiriki katika ujenzi au harakati zozote, bali kutekeleza huduma Yake. Kila mara Yeye anapokuwa mwili, ni ili tu kukamilisha hatua ya kazi na kuanzisha enzi mpya. Sasa Enzi ya Ufalme imewadia, na vile mafunzo ya ufalme yamewadia. Hatua hii ya kazi si kazi ya mwanadamu, na si kumfinyanga mwanadamu hadi kiwango fulani, bali ni ili tu kukamilisha sehemu ya kazi ya Mungu. Kile Anachofanya si kazi ya mwanadamu, si kufanikisha matokeo fulani katika kumfinyanga mwanadamu kabla ya kuondoka duniani; ni ili kutimiza huduma Yake na kumaliza kazi Anayopaswa kufanya, ambayo ni kupanga vizuri kazi Yake duniani, na baada ya hapo Atapata utukufu. Kazi ya Mungu mwenye mwili ni tofauti na ile ya watu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu. Mungu anapokuja kufanya kazi Yake duniani, Yeye anajali tu kuhusu kutekeleza huduma Yake. Kuhusu mambo mengine yote yasiyohusiana na huduma Yake, Yeye karibu hashiriki kabisa, hata hatilii maanani mambo kama hayo. Yeye anatekeleza tu kazi Anayopaswa kufanya, na hata zaidi hajali kuhusu kazi ambayo mwanadamu anapaswa kufanya. Kazi anayofanya ni ile tu inayohusu enzi Aliyomo na huduma Anayopaswa kutekeleza, kana kwamba mambo mengine yote yako nje ya upeo Wake. Yeye hajizatiti na maarifa ya msingi zaidi kuhusu kuishi kama mmoja miongoni mwa binadamu, wala Hajifunzi ustadi zaidi wa kijamii, wala Hajizatiti na kitu kingine chochote ambacho mwanadamu anaelewa. Yote anayopaswa kuwa nayo mwanadamu hayamhusu Yeye hata kidogo na Yeye hufanya tu kazi ambayo ni wajibu Wake. Na hivyo, jinsi mwanadamu anavyoona, Mungu mwenye mwili anapungukiwa na mengi sana—Yeye hata hatilii maanani mambo mengi ambayo mwanadamu anapaswa kuwa nayo, na hana ufahamu wa mambo kama hayo. Mambo kama vile maarifa ya kawaida kuhusu maisha, pamoja na kanuni za kujiendesha na kushughulika na ulimwengu, karibu hayahusiani kabisa na Yeye. Lakini huwezi kuhisi kutoka kwa Mungu mwenye mwili dalili yoyote ndogo ya kutokuwa wa kawaida. Yaani, ubinadamu Wake hudumisha tu maisha Yake ya kawaida ya binadamu na busara ya kawaida ya ubongo Wake, ukimpa uwezo wa kutambua kati ya mema na mabaya. Hata hivyo, Yeye hajizatiti na vitu vingine vyovyote, ambavyo vyote ni vile ambavyo mwanadamu (viumbe walioumbwa) pekee anapaswa kuwa navyo. Mungu anapata mwili tu ili kutekeleza huduma Yake Mwenyewe. Kazi Yake inaelekezwa kwa enzi nzima, si kwa mtu au mahali popote pale, bali kwa ulimwengu mzima. Huu ndio mwelekeo wa kazi Yake na kanuni ambayo kwayo Anafanya kazi. Hakuna anayeweza kubadili hili, na mwanadamu hana namna ya kuhusika ndani yake. Kila mara Mungu anapopata mwili, Analeta pamoja na Yeye kazi ya enzi hiyo, na hana nia ya kuishi pamoja na mwanadamu kwa miaka ishirini, thelathini, arobaini, au hata sabini au themanini ili mwanadamu aweze kumwelewa vizuri zaidi na kumjua kwa kina. Hakuna haja ya hilo! Kufanya hivyo hakutaongeza kina cha maarifa ambayo mwanadamu anayo kuhusu tabia asili ya Mungu kwa namna yoyote ile; badala yake, kutaongeza tu dhana zake na kusababisha dhana na mawazo yake yawe magumu kubadilika. Kwa hivyo inawapasa ninyi nyote muelewe hasa kazi ya Mungu mwenye mwili ni nini. Hakika hamwezi kuwa mmeshindwa kuelewa maneno Niliyonena kwenu: “Sikuja ili kupitia maisha ya mwanadamu wa kawaida”? Je, mmesahau maneno haya: “Mungu haji duniani kuishi maisha ya mwanadamu wa kawaida”? Hamwelewi kusudi la Mungu katika kupata mwili, wala hamjui hili: “Mungu angewezaje kuja duniani kwa nia ya kupitia maisha ya kiumbe aliyeumbwa?” Mungu huja duniani tu ili kukamilisha kazi Yake, na hivyo kazi Yake duniani ni ya muda mfupi. Yeye haji duniani kwa nia ya kusababisha Roho wa Mungu kukuza mwili Wake wa nyama kuwa mwanadamu bora ambaye ataongoza kanisa. Mungu anapokuja duniani, ni Njia kuwa mwili; mwanadamu, hata hivyo, hajui kuhusu kazi Yake na humpachikia mambo kwa lazima. Lakini ninyi nyote mnapaswa kuelewa kwamba Mungu ni Njia kuwa mwili, si mwili wa nyama ambao umekuzwa na Roho wa Mungu kuchukua jukumu la Mungu kwa muda. Mungu Mwenyewe si zao la ukuzaji, bali ni Njia, Neno, lililokuwa mwili, na leo Anatekeleza kazi Yake rasmi miongoni mwenu nyote. Ninyi nyote mnajua, na mnakiri, kwamba kupata mwili kwa Mungu ni ukweli halisi, lakini mnajifanya mnaelewa. Kuanzia kazi ya Mungu mwenye mwili hadi umuhimu na kiini cha kupata mwili Kwake, hamfahamu haya hata kidogo na mnawafuata tu wengine katika kukariri maneno kwa ufasaha kutoka akilini. Je, unaamini Mungu mwenye mwili kuwa kama unavyowazia?

Mungu anakuwa mwili ili tu kuongoza enzi na kuanzisha kazi mpya. Ni lazima mwelewe jambo hili. Hili ni tofauti sana na jukumu la mwanadamu, na haya mawili hayawezi kuwekwa katika kiwango kimoja. Mwanadamu anahitaji kukuzwa na kufanywa kuwa mtimilifu kwa kipindi kirefu kabla ya kuweza kutumiwa kutekeleza kazi, na aina ya ubinadamu unaohitajika ni wa kiwango cha juu hasa. Sio tu kwamba mwanadamu lazima aweze kudumisha busara ya ubinadamu wa kawaida, bali lazima aelewe zaidi kanuni na sheria nyingi zinazotawala jinsi anavyoshughulika na ulimwengu, na, zaidi ya hayo, lazima ajitolee kujifunza hata zaidi kuhusu hekima na maarifa ya kimaadili ya mwanadamu. Haya ndiyo ambayo mwanadamu anapaswa kujizatiti nayo. Hata hivyo, hivyo sivyo ilivyo kwa Mungu aliyekuwa mwili, kwa sababu kazi Yake haimwakilishi mwanadamu wala si kazi ya mwanadamu, na badala yake ni maonyesho ya moja kwa moja ya nafsi Yake na utendaji wa moja kwa moja wa kazi Anayopaswa kufanya. (Bila shaka, kazi Yake inatekelezwa kwa wakati unaofaa, si bila mpango au kiholela, na inaanza wakati unapofika wa kutekeleza huduma Yake.) Yeye hashiriki katika maisha ya mwanadamu au kazi ya mwanadamu, yaani, ubinadamu Wake haujazatitiwa na lolote kati ya haya (ingawa hili haliathiri kazi Yake). Yeye hutekeleza tu huduma Yake wakati unapofika wa Yeye kufanya hivyo; haijalishi hadhi Yake ni ipi, Yeye hulenga tu kufanya kazi Anayopaswa kufanya. Chochote ambacho mwanadamu anajua kumhusu Yeye na maoni yoyote ya mwanadamu kumhusu Yeye, kazi Yake haiathiriwi kabisa. Kwa mfano, Yesu alipotekeleza kazi Yake, hakuna aliyejua Yeye alikuwa nani hasa, lakini Yeye alilenga tu kufanya kazi Yake. Hakuna lolote kati ya haya lililomzuia Yeye katika kutekeleza kazi Aliyopaswa kufanya. Kwa hivyo, mwanzoni Yeye hakufunua au kutangaza utambulisho Wake Mwenyewe, na Alimfanya mwanadamu amfuate Yeye tu. Bila shaka huu haukuwa tu unyenyekevu wa Mungu, bali pia ilikuwa njia ambayo kwayo Mungu alifanya kazi katika mwili. Yeye angeweza tu kufanya kazi kwa njia hii, kwa maana mwanadamu hakuwa na njia ya kumtambua Yeye kwa macho ya kawaida. Na hata kama mwanadamu angemtambua Yeye, hili halingesaidia kazi Yake. Zaidi ya hayo, Yeye hakufanyika mwili ili kumfanya mwanadamu aje kuujua mwili Wake; ilikuwa ni kutekeleza kazi na kutekeleza huduma Yake. Kwa sababu hii, Yeye hakuweka umuhimu wowote katika kuweka utambulisho Wake wazi kwa umma. Alipokamilisha kazi yote Aliyopaswa kufanya, utambulisho Wake wote na hadhi Yake bila shaka vilikuwa wazi kwa mwanadamu. Mungu aliyekuwa mwili hunyamaza kimya na hatoi matangazo yoyote kamwe. Yeye hajali jinsi mwanadamu alivyo wala jinsi mwanadamu anavyoendelea katika kumfuata Yeye, bali hulenga tu kutekeleza huduma Yake na kutekeleza kazi Anayopaswa kufanya. Hakuna anayeweza kuzuia kazi Yake. Wakati unapofika wa Yeye kuhitimisha kazi Yake, ni lazima itahitimishwa na kutamatishwa, na hakuna anayeweza kuamuru vinginevyo. Ni baada tu ya Yeye kuondoka kwa mwanadamu Anapokamilisha kazi Yake ndipo mwanadamu ataelewa kazi Anayofanya, ingawa bado si wazi kabisa. Na itachukua muda mrefu kwa mwanadamu kuelewa kikamilifu nia ambazo kwazo Yeye alitekeleza kazi Yake mwanzoni. Yaani, kazi ya enzi ya Mungu mwenye mwili imegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu moja ya kazi ni mwili wa Mungu mwenye mwili ukifanya kazi na kuzungumza binafsi. Punde tu huduma ya mwili Wake inapotimizwa kikamilifu, sehemu nyingine ya kazi inasalia kutekelezwa na wale wanaotumiwa na Roho Mtakatifu. Ni wakati huu ndipo mwanadamu anapaswa kutimiza jukumu lake, kwa maana Mungu tayari amefungua njia, na mwanadamu mwenyewe anapaswa kuitembea. Yaani, Mungu aliyekuwa mwili anatekeleza sehemu moja ya kazi, na kisha Roho Mtakatifu na wale wanaotumiwa na Roho Mtakatifu wataiendeleza kazi hii. Kwa hivyo, mwanadamu anapaswa kujua kile ambacho kazi inayotekelezwa kimsingi na Mungu aliyekuwa mwili katika hatua hii inahusisha, na lazima aelewe hasa umuhimu wa Mungu kuwa mwili ni nini na kazi Anayopaswa kufanya ni ipi, na asitoe matakwa kwa Mungu kulingana na matakwa yanayotolewa kwa mwanadamu. Hapa ndipo palipo na kosa la mwanadamu, dhana yake, na hata zaidi, uasi wake.

Mungu anakuwa mwili si kwa nia ya kumruhusu mwanadamu kuujua mwili Wake, au kumruhusu mwanadamu kupambanua tofauti kati ya mwili wa Mungu mwenye mwili na ule wa mwanadamu; wala Mungu hawi mwili ili kutoa mafunzo kwa nguvu za utambuzi za mwanadamu, na sembuse Yeye kufanya hivyo kwa nia ya kumruhusu mwanadamu kuabudu mwili wa Mungu mwenye mwili, na hivyo kupata utukufu mkuu. Hakuna lolote kati ya mambo haya ambalo ni nia ya Mungu katika kuwa mwili. Wala Mungu hawi mwili ili kumhukumu mwanadamu, wala kumfichua mwanadamu kwa makusudi, wala kumfanyia mambo kuwa magumu. Hakuna lolote kati ya mambo haya ambalo ni nia ya Mungu. Kila mara Mungu anapokuwa mwili, ni aina ya kazi ambayo haiepukiki. Ni kwa ajili ya kazi Yake kuu zaidi na usimamizi Wake mkuu zaidi ndiyo maana Yeye hutenda Anavyotenda—si kama mwanadamu anavyoiwazia kuwa. Mungu huja duniani tu kama kazi Yake inavyohitaji, na inapobidi tu. Yeye haji duniani kwa nia ya kutazama huku na kule tu, bali kutekeleza kazi Anayopaswa kufanya. Kuna sababu nyingine gani ambayo ingemfanya Achukue mzigo mzito kama huo na kuchukua hatari kubwa kama hizo kutekeleza kazi hii? Mungu anakuwa mwili tu Anapolazimika kufanya hivyo, na daima kukiwa na umuhimu wa kipekee. Kama ingekuwa tu kwa ajili ya kuwaruhusu watu kumtazama na kupanua upeo wao, basi Yeye, kwa uhakika kabisa, Asingekuja kamwe miongoni mwa watu kirahisi hivyo. Yeye huja duniani kwa ajili ya usimamizi Wake na kazi Yake kuu zaidi, na ili awapate wanadamu zaidi. Yeye huja kuwakilisha enzi, Yeye huja kumshinda Shetani, na Yeye hujivika mwili ili kumshinda Shetani. Hata zaidi, Yeye huja ili kuongoza jamii nzima ya binadamu katika kuishi maisha yao. Yote haya yanahusu usimamizi Wake, na yanahusu kazi ya ulimwengu mzima. Kama Mungu angekuwa mwili tu ili kumruhusu mwanadamu aje kuujua mwili Wake na kufumbua macho ya watu, basi kwa nini Yeye asisafiri kwenda katika kila taifa? Je, hili lisingekuwa jambo rahisi mno? Lakini Yeye hakufanya hivyo, badala yake Akichagua mahali panapofaa pa kufanya makazi na kuanza kazi Anayopaswa kufanya. Mwili huu pekee una umuhimu mkubwa. Yeye anawakilisha enzi nzima, na pia Anatekeleza kazi ya enzi nzima; Yeye huhitimisha enzi ya awali na kuanzisha mpya. Haya yote ni mambo muhimu ambayo yanahusu usimamizi wa Mungu, na yote haya ni umuhimu wa hatua moja ya kazi ambayo Mungu huja duniani kutekeleza. Yesu alipokuja duniani, Yeye alinena tu maneno kadhaa na kutekeleza kazi fulani; Yeye hakujali uzima wa mwanadamu, na Yeye aliondoka punde tu Alipokamilisha kazi Yake. Leo, Nitakapokuwa nimemaliza kuzungumza na kuyapitishia maneno Yangu kwenu, na ninyi nyote mtakuwa mmeelewa, hatua hii katika kazi Yangu itakuwa imehitimishwa, haijalishi uzima wenu utakuwaje. Ni lazima katika siku za usoni kuwe na baadhi ya watu wa kuendeleza hatua hii katika kazi Yangu na kuendelea kufanya kazi duniani kulingana na maneno haya; wakati huo, kazi ya mwanadamu na ujenzi wa mwanadamu vitaanza. Lakini, katika wakati wa sasa, Mungu anafanya tu kazi Yake ili kutekeleza huduma Yake na kukamilisha hatua moja ya kazi Yake. Mungu anafanya kazi kwa njia tofauti na ile ya mwanadamu. Mwanadamu anapenda makusanyiko na mabaraza, na huweka umuhimu kwenye desturi, ilhali kile ambacho Mungu anachukia kabisa hasa ni makusanyiko na mikutano ya mwanadamu. Mungu huzungumza na kunena na mwanadamu kwa namna isiyo rasmi; hii ndiyo kazi ya Mungu, ambayo ni huru sana na pia inawaweka ninyi huru. Hata hivyo, Mimi ninachukia kabisa kukusanyika pamoja nanyi, na Siwezi kuzoea maisha yanayodhibitiwa sana kama yenu. Mimi ninachukia taratibu zaidi ya yote; zinamwekea mwanadamu vikwazo hadi kufikia hatua ya kumfanya aogope kufanya jambo, aogope kuzungumza, na aogope kuimba, macho yake yakikutazama wewe moja kwa moja. Mimi ninachukia kabisa namna yenu ya kukusanyika na Mimi ninachukia kabisa makusanyiko makubwa. Mimi ninakataa tu kukusanyika pamoja nanyi kwa namna hii, kwa maana namna hii ya kuishi inamfanya mtu ahisi amefungwa pingu na ninyi huzingatia desturi nyingi mno na taratibu nyingi mno. Kama mngeruhusiwa kuongoza mngewaongoza watu wote kuingia katika uwanja wa taratibu, na hawangekuwa na namna ya kutupilia mbali taratibu chini ya uongozi wenu; badala yake harufu ya dini ingezidi kuwa kali, na matendo ya mwanadamu yangeendelea tu kuongezeka kwa wingi. Watu wengine huendelea kuzungumza na kuongea wanapokusanyika na hawahisi uchovu kamwe, na wengine wanaweza kuendelea kuhubiri kwa zaidi ya siku kumi bila kukoma. Haya yote yanachukuliwa kuwa makusanyiko makubwa na mikutano ya mwanadamu; hayahusiani na maisha ya kula na kunywa, ya kufurahia, au ya roho kuwekwa huru. Hii yote ni mikutano! Mikutano yenu ya wafanyakazi wenza, pamoja na makusanyiko makubwa na madogo, yote ni ya kuchukiza Kwangu, na Sijawahi kuhisi kuvutiwa nayo. Hii ndiyo kanuni ambayo kwayo Mimi hufanya kazi: Siko tayari kuhubiri wakati wa makusanyiko, wala Sitamani kutangaza chochote katika kusanyiko kubwa la umma, na sembuse kuwaita ninyi nyote kwa siku chache za mkutano maalum. Sioni kuwa inafaa kwamba ninyi nyote mnapaswa kuketi, kwa adabu na nidhamu, katika mkusanyiko; Ninachukia kuwaona ninyi mkiishi ndani ya mipaka ya desturi yoyote ile, na hata zaidi, Mimi ninakataa kushiriki katika desturi yenu kama hiyo. Kadiri mnavyofanya hivi, ndivyo Ninavyoiona inachukiza zaidi. Sipendezwi hata kidogo na hizi desturi na taratibu zenu; haijalishi mnafanya kazi nzuri kiasi gani nazo, Mimi naziona zote kuwa za kuchukiza. Si kwamba mmepanga mambo vibaya au kwamba ninyi ni wa chini mno; ni kwamba Mimi ninachukia namna yenu ya kuishi na, hata zaidi, Mimi siwezi kuizoea. Hamwelewi hata kidogo kazi Ninayotaka kufanya. Yesu alipofanya kazi Yake wakati huo, baada ya kuhubiri mahali fulani, Yeye angewatoa wanafunzi Wake nje ya mji na kunena maneno fulani kwao ambayo iliwapasa kufahamu. Yeye mara nyingi alifanya kazi kwa namna hiyo. Kazi Yake miongoni mwa umati ilikuwa chache na ya nadra. Kulingana na kile mnachotaka kutoka Kwake, Mungu aliyekuwa mwili hapaswi kuwa na maisha ya mwanadamu wa kawaida; Yeye lazima atekeleze kazi Yake, na, iwe Yeye ameketi, amesimama, au anatembea, Yeye lazima anene. Yeye lazima afanye kazi wakati wote na hawezi kamwe kusitisha “shughuli,” vinginevyo Yeye angekuwa anapuuza wajibu Wake. Je, matakwa haya ya mwanadamu yanafaa kwa busara ya binadamu? Uadilifu wenu uko wapi? Je, haya matakwa yenu hayajapita kiasi? Je, Ninakuhitaji wewe unichunguze Ninapofanya kazi? Je, Ninakuhitaji wewe usimamie Ninapotekeleza huduma Yangu? Mimi najua vizuri kazi Ninayopaswa kufanya na wakati Ninapopaswa kuifanya; hakuna haja ya wengine kuingilia kati. Pengine inaweza kuonekana kwako kana kwamba Sijafanya mengi, lakini kufikia wakati huo kazi Yangu inakuwa imefika mwisho. Chukua kwa mfano maneno ya Yesu katika Injili Nne: Je, hayakuwa na mipaka pia? Wakati huo, Yesu alipoingia katika sinagogi na kuhubiri mahubiri, Yeye alimaliza ndani ya dakika chache ikiwa imezidi sana, na Alipomaliza kunena, Yeye aliwaongoza wanafunzi Wake kwenye mashua na kuondoka bila maelezo yoyote. Kwa kuzidi sana, wale waliokuwa ndani ya sinagogi walijadili hili miongoni mwao, lakini Yesu hakushiriki katika hilo. Mungu hufanya tu kazi Anayopaswa kufanya, na hakuna chochote zaidi ya hiki. Sasa, wengi wanataka Mimi nizungumze zaidi na kuongea zaidi, angalau saa kadhaa kwa siku. Jinsi mnavyoona, Nisiponena, Mimi si Mungu, na Mimi ni Mungu tu Ninaponena. Ninyi nyote ni vipofu! Nyote ni wanyama! Ninyi nyote ni vitu vya kijinga visivyo na busara! Ninyi mna dhana nyingi mno! Matakwa yenu yanapita kiasi! Ninyi hamna ubinadamu! Hamwelewi hata kidogo kile Mungu alicho! Ninyi mnaamini kwamba wasemaji na wahutubu wote ni miungu, na kwamba yeyote aliye tayari kuwapa ninyi maneno ni baba yenu. Niambieni, je, ninyi nyote, pamoja na sura zenu nzuri na mwonekano usio wa kawaida, bado mna hata chembe ndogo kabisa ya busara? Je, bado mnajua jua la mbingu! Kila mmoja wenu ni kama afisa mlafi na fisadi, kwa hivyo mnawezaje kuwa na busara? Mnawezaje kupambanua kati ya mema na mabaya? Nimewapa ninyi mengi, lakini ni wangapi miongoni mwenu wameyathamini? Ni nani ameyapata kwa ukamilifu wake? Ninyi hamjui ni nani aliyeleta njia ambayo kwayo mnatembea leo, kwa hivyo mnaendelea kutoa matakwa Kwangu, mkitoa matakwa haya yasiyo na urazini. Je, hamwoni aibu sana? Je, Sijanena vya kutosha? Je, Sijafanya vya kutosha? Ni nani miongoni mwenu anayeweza kuyathamini maneno Yangu kweli kama hazina? Ninyi hujipendekeza Kwangu mnapokuwa mbele Yangu, lakini ninyi hudanganya msipokuwa mbele Yangu! Matendo yenu ni ya kudharauliwa mno, na ni ya kuchukiza! Mimi najua kwamba mnaniomba Ninene na nifanye kazi si kwa sababu nyingine ila tu kufurahisha macho yenu na kupanua upeo wenu, sio kwa ajili ya kubadilisha maisha yenu. Nimenena mengi sana kwenu. Maisha yenu yalipaswa kuwa yamebadilika kitambo, hivyo basi kwa nini bado mnaendelea kurudia hali zenu za zamani hata sasa? Inawezekana kwamba maneno Yangu yameibwa kutoka kwenu na hamkuyapokea? Kusema ukweli, Sitamani kunena zaidi kwa wapotovu kama ninyi—ingekuwa bure! Sitamani kufanya kazi nyingi hivi ya bure! Ninyi mnatamani tu kupanua upeo wenu au kufurahisha macho yenu, na sio kupata uzima! Ninyi nyote mnajidanganya wenyewe! Ninawauliza ninyi, ni kiasi gani cha yale Niliyowaambia uso kwa uso ambacho mmetia katika vitendo? Mnachofanya tu ni kufanya hila ili kuwadanganya wengine! Mimi ninawachukia wale miongoni mwenu wanaofurahia kutazama kama watazamaji, na Ninaona udadisi wenu kuwa wa kuchukiza sana. Kama hamko hapa kufuatilia njia ya kweli au kuonea kiu ukweli, basi ninyi ni walengwa wa chuki Yangu! Mimi ninajua kwamba mnanisikiliza Nikizungumza tu ili kutosheleza udadisi wenu au kutimiza tamaa yenu moja au nyingine. Hamna wazo la kutafuta uwepo wa ukweli, au la kuchunguza njia sahihi ya kuingia katika uzima; matakwa haya hayapo kabisa miongoni mwenu. Mnachofanya tu ni kumchukulia Mungu kama kitu cha kuchezea ambacho mnakichunguza na kukitazama kwa kupendezwa nacho. Mna shauku kiasi kidogo mno ya kufuatilia uzima, lakini tamaa nyingi ya kuwa wadadisi! Kuwaeleza watu kama hao njia ya uzima ni sawa na kupoteza mate; ni afadhali Nisinene kabisa! Acheni Niwaambie: Kama mnatafuta tu kujaza pengo ndani ya mioyo yenu, basi ni afadhali msije Kwangu! Inawapasa kuweka umuhimu katika kupata uzima! Msijidanganye! Ni afadhali msichukue udadisi wenu kama msingi wa ufuatiliaji wenu wa uzima au kuutumia kama kisingizio cha kunitaka Ninene nanyi. Hizi zote ni hila ambazo ninyi ni stadi sana kwazo! Ninakuuliza tena: Ni kiasi gani cha yale Ninayokutaka uingie ambayo umeyaingia kweli? Je, umeelewa yote ambayo Nimekwambia? Je, umetia katika vitendo yote ambayo Nimekwambia?

Kazi ya kila enzi huanzishwa na Mungu Mwenyewe, lakini unapaswa kujua kwamba, haijalishi ni namna gani ambayo kwayo Mungu hufanya kazi, Yeye haji kuanzisha harakati, au kufanya mikutano maalum, au kuanzisha shirika la aina yoyote kwa ajili yenu. Yeye huja tu kutekeleza kazi Anayopaswa kufanya. Kazi Yake haizuiliwi na mwanadamu yeyote. Yeye hufanya kazi Yake vyovyote Anavyotaka; haijalishi mwanadamu anafikiri nini au anaielewa vipi, Yeye anajali tu kuhusu kutekeleza kazi Yake. Kuanzia uumbaji wa ulimwengu hadi sasa, tayari kumekuwa na hatua tatu za kazi; kutoka kwa Yehova hadi kwa Yesu, na kutoka Enzi ya Sheria hadi Enzi ya Neema, Mungu hajawahi kuitisha mkutano maalum kwa ajili ya mwanadamu, wala Yeye hajawahi kuwakusanya wanadamu wote pamoja ili kuitisha mkutano maalum wa kazi wa kimataifa na hivyo kueneza kazi Yake. Kile anachofanya tu ni kutekeleza kazi ya awali ya enzi nzima kwa wakati unaofaa na mahali panapofaa, na hivyo kuanzisha enzi na kuongoza jamii ya binadamu katika jinsi ya kuishi maisha yao. Mikutano maalum ni makusanyiko ya mwanadamu; kuwakusanya watu pamoja kusherehekea sikukuu ni kazi ya mwanadamu. Mungu haadhimishi sikukuu na, hata zaidi, Yeye anaziona kuwa za kuchukiza; Yeye haitishi mikutano maalum na, zaidi ya hayo, Yeye anaiona kuwa ya kuchukiza. Sasa unapaswa kuelewa hasa kazi inayofanywa na Mungu mwenye mwili ni nini!

Iliyotangulia:  Fumbo la Kupata Mwili (2)

Inayofuata:  Fumbo la Kupata Mwili (4)

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger