Matamko ya Kristo Mwanzoni—Sura ya 103

Sauti ya ngurumo inatoka, ikiutikisa ulimwengu mzima, ikipasua masikio, na watu hawabakiwi na muda wa kuikwepa. Wengine wanapigwa, wengine wanaangamizwa, na wengine wanahukumiwa. Kwa kweli ni tukio ambalo hakuna yeyote amewahi kuliona hapo awali. Sikiliza kwa makini: Milio ya ngurumo inaambatana na sauti ya maombolezo, na sauti hii inatoka Kuzimu; inatoka jahanamu. Ni kilio cha uchungu cha wale wana wa uasi ambao wamehukumiwa na Mimi. Wale ambao hawajasikiliza kile Ninachosema na ambao hawajatia maneno Yangu katika vitendo wamehukumiwa vikali na kupokea laana ya ghadhabu Yangu. Sauti Yangu ni hukumu na ghadhabu; haimwonyeshi yeyote huruma, na haionyeshi rehema kwa yeyote, kwa maana Mimi ni Mungu Mwenyewe mwenye haki, na Nina ghadhabu, kuteketeza, utakaso, na maangamizo. Ndani Yangu, hakuna chochote kilichofichika na hakuna hisia za nyama; kinyume chake, kuna uwazi, haki, uadilifu na kutopendelea. Kwa sababu wazaliwa Wangu wa kwanza tayari wako pamoja na Mimi kwenye kiti cha enzi, wakitawala juu ya mataifa na watu wasiohesabika, mambo na watu wasio wenye haki na dhalimu wanaanza kuhukumiwa. Nitayachunguza mambo hayo moja baada ya lingine na kuwachunguza watu hao mmoja baada ya mwingine, bila kukosa chochote na kuyafunua na kuwafunua kikamilifu. Kwa maana hukumu Yangu imefunuliwa kikamilifu na kuwekwa wazi kikamilifu, na Sijabakiza chochote hata kidogo; Nitawatupa nje wote ambao hawalingani na nia Zangu, na kuwafanya waangamie kwa umilele wote katika shimo lisilo na mwisho. Huko Nitawafanya waungue milele. Hii pekee ndiyo haki Yangu, na huu pekee ndio unyofu Wangu. Hakuna anayeweza kubadilisha hili, na kila kitu lazima kinitii.

Watu wengi hupuuza maneno Yangu, wakifikiri kwamba maneno ni maneno tu na kwamba mambo ya hakika ni mambo ya hakika. Wao ni vipofu! Je, hawajui kwamba Mimi ndimi Mungu mwaminifu Mwenyewe? Maneno Yangu na mambo ya hakika hutendeka kwa wakati mmoja. Je, si huu ni ukweli kabisa? Watu hawaelewi maneno Yangu hata kidogo, na ni wale tu ambao wametiwa nuru ndio wanaoweza kuelewa kweli. Hili ni jambo la hakika. Punde tu watu wanapoona maneno Yangu, wanatishika kwa kuchanganyikiwa sana na kukimbia huku na kule ili kujificha. Hili ni kweli hata zaidi hukumu Yangu inaposhuka. Nilipoumba vitu vyote, Ninapoiharibu dunia, na Ninapowafanya wazaliwa wa kwanza kuwa kamili—mambo haya yote yanatimizwa kwa neno moja kutoka kinywani Mwangu. Hii ni kwa sababu neno Langu lenyewe ni mamlaka; ni hukumu. Inaweza kusemwa kwamba nafsi Yangu ni hukumu na uadhama, na hakuna anayeweza kubadilisha hili. Hiki ni kipengele kimoja cha amri Zangu za utawala; ni njia ambayo kwayo Ninawahukumu watu. Machoni Pangu, kila kitu—ikiwa ni pamoja na watu, matukio, na vitu vyote—kiko mikononi Mwangu na chini ya hukumu Yangu. Hakuna mtu anayethubutu wala kitu chochote kinachothubutu kufanya chochote kisichofaa, na yote lazima yatimizwe kulingana na maneno Ninayotamka. Katika dhana za binadamu, kila mtu anaamini maneno ya nafsi Yangu. Roho Wangu anapotoa matamko, kila mtu anakuwa na shaka, anakosa maarifa yoyote ya uweza Wangu, na hata anatoa tuhuma dhidi Yangu. Ninakwambia sasa, yeyote anayetilia shaka maneno Yangu, na yeyote anayeyachukulia maneno Yangu kwa kijuujuu tu, hawa ndio wale watakaoangamizwa; wao ni wana wa mateso ya milele. Kutokana na hili inaweza kuonekana kwamba kuna wachache sana ambao ni wazaliwa wa kwanza, kwa sababu hivi ndivyo Ninavyofanya kazi. Kama Nilivyosema hapo awali, Ninatimiza kila kitu bila kusogeza kidole; Ninatumia maneno Yangu tu. Hapa, basi, ndipo uweza Wangu ulipo. Katika maneno Yangu, hakuna anayeweza kupata chanzo na kusudi la kile Ninachosema. Watu hawawezi kufikia hili. Wanaweza tu kufuata mwongozo Wangu katika matendo yao, na kufuata haki Yangu katika kufanya kila kitu kinacholingana na nia Zangu, na kusababisha familia Yangu kuwa na haki na amani, kuishi milele, na kuwa thabiti na isiyoyumbayumba milele.

Hukumu Yangu inamjia kila mtu, amri Zangu za utawala zinamgusa kila mtu, na maneno Yangu na nafsi Yangu vinafunuliwa kwa kila mtu. Huu ndio wakati wa Roho Wangu kufanya kazi kuu (wakati huu, wale watakaobarikiwa, na wale watakaokumbwa na ole, wanatofautishwa). Punde tu maneno Yangu yanapotoka, Nimewatofautisha wale watakaobarikiwa na wale watakaokumbwa na ole. Haya yote yako wazi kabisa, na Ninaweza kuyaona yote kwa mtazamo mmoja. (Ninasema hili kuhusiana na ubinadamu Wangu; kwa hivyo, maneno haya hayapingani na kuamua Kwangu kabla na uteuzi Wangu.) Ninazunguka kwenye milima na mito na kati ya vitu vyote, katika anga za ulimwengu, Nikichunguza na kutakasa kila mahali ili maeneo hayo machafu na nchi hizo za uasherati vyote vikome kuwepo na kuteketezwa hadi kutokuwepo kabisa kutokana na maneno Yangu. Kwangu Mimi, kila kitu ni rahisi. Kama sasa ungekuwa wakati Niliouamua kabla kwa ajili ya uharibifu wa dunia, Ningeweza kuimeza kwa tamko la neno moja. Hata hivyo, sasa si wakati muafaka. Yote lazima yawe tayari kabla Sijafanya kazi hii ili mpango Wangu usisumbuliwe na usimamizi Wangu usivurugwe. Ninajua jinsi ya kufanya hili kwa urazini. Nina hekima Yangu, na Nina mipangilio Yangu Mwenyewe. Watu hawapaswi kusogeza kidole kimoja; kuweni waangalifu msije mkapigwa na mkono Wangu. Hili tayari limegusia amri Zangu za utawala. Kutokana na hili mtu anaweza kuona ukali wa amri Zangu za utawala, pamoja na kanuni zake, ambazo zinajumuisha vipengele viwili: Kimoja ni kwamba Ninawapiga wote ambao hawalingani na nia Zangu na wanaokiuka amri Zangu za utawala; kingine ni kwamba Ninawalaani kwa ghadhabu wote wanaokiuka amri Zangu za utawala. Vipengele hivi viwili ni vya lazima, na ndizo kanuni za utekelezaji za amri Zangu za utawala. Kila mtu anashughulikiwa kulingana na kanuni hizi mbili, bila upendeleo hata kidogo, bila kujali jinsi mtu anavyoweza kuwa mwaminifu. Hili linatosha kuonyesha haki Yangu, uadhama Wangu, na ghadhabu Yangu, ambayo itateketeza vitu vyote vya kidunia, vitu vyote vya ulimwengu, na vitu vyote ambavyo havilingani na nia Zangu. Katika maneno Yangu kuna siri ambazo zinasalia zikiwa zimefichika, na pia katika maneno Yangu, kuna siri ambazo zimefunuliwa. Hivyo, kulingana na dhana za binadamu na kufikiri kwa binadamu, maneno Yangu hayaeleweki milele, na moyo Wangu hauchunguziki milele. Yaani, lazima Niwaondolee wanadamu dhana na kufikiri kwao. Hiki ndicho kipengele muhimu kabisa cha mpango Wangu wa usimamizi. Lazima Nifanye hivi ili kuwapata wazaliwa Wangu wa kwanza na kutimiza mambo Ninayotaka kufanya.

Majanga ya dunia yanazidi kuwa makubwa siku baada ya siku, na katika nyumba Yangu, majanga makuu yanazidi kuwa na nguvu zaidi. Kwa kweli watu hawana mahali pa kujificha, hawana mahali pa kujisitiri. Kwa sababu mpito unafanyika sasa hivi, hakuna hata mtu mmoja anayejua atapiga wapi hatua yake inayofuata. Hili litafunuliwa tu baada ya hukumu Yangu. Kumbukeni! Hizi ndizo hatua za kazi Yangu, na ndiyo njia ambayo kwayo Ninafanya kazi. Nitawafariji wazaliwa Wangu wote wa kwanza mmoja baada ya mwingine, na kuwainua hatua moja kwa wakati mmoja; kuhusu watendaji huduma, Nitawaondosha na kuwaacha wote, mmoja baada ya mwingine. Hii ni sehemu moja ya mpango Wangu wa usimamizi. Baada ya watendaji huduma wote kufunuliwa, wazaliwa Wangu wa kwanza pia watafunuliwa. (Kwangu Mimi, hili ni jambo rahisi sana. Baada ya wao kusikia maneno Yangu, watendaji huduma hao wote watajiondoa hatua kwa hatua chini ya hukumu na tishio la maneno Yangu, na ni wazaliwa Wangu wa kwanza tu ndio watakaosalia. Hili ni jambo lililo nje ya udhibiti wa mwanadamu, jambo ambalo haliwezi kubadilishwa na mapenzi ya mwanadamu; ni Roho Wangu akifanya kazi binafsi.) Hili si tukio la mbali, na mnapaswa, kwa kiasi fulani, kuweza kulitambua kutokana na awamu hii ya kazi Yangu na maneno Yangu. Sababu ya Mimi kusema mengi hivi, pamoja na asili isiyotabirika ya matamko Yangu, ni mambo yasiyoweza kueleweka kwa watu. Ninazungumza na wazaliwa Wangu wa kwanza kwa sauti za faraja, rehema, na wema (kwa sababu Mimi huwatia nuru watu hawa kila mara, na Sitawaacha, na kwa sababu Niliwaamua kabla), huku Nikiwashughulikia watu wengine mbali na wazaliwa Wangu wa kwanza kwa hukumu kali, kwa vitisho, na kwa kuwatia hofu, Nikiwafanya wahisi kutishika kila wakati kiasi kwamba wanakuwa na wasiwasi mkubwa kila wakati. Punde tu hali itakapokua hadi kiwango fulani, wataiepa hali hii (Nitakapoiharibu dunia, watu hawa watakuwa katika shimo lisilo na mwisho), lakini hawatawahi kuutoroka mkono Wangu wa hukumu au kujinasua kutoka katika hali hii. Hii, basi, ni hukumu yao; huku ni kuadibu kwao. Siku ambayo wageni watawasili, Nitawafunua watu hawa, mmoja baada ya mwingine. Hizi ni hatua za kazi Yangu. Je, sasa mnaelewa nia iliyo nyuma ya matamko Yangu ya awali ya maneno hayo? Kwa maoni Yangu, jambo ambalo halijatimizwa pia ni jambo ambalo limetimizwa, lakini jambo ambalo limetimizwa si lazima liwe jambo ambalo limefanikishwa. Hii ni kwa sababu Nina hekima Yangu na njia Yangu ya kufanya kazi, mambo ambayo hayawezi kueleweka kwa wanadamu. Punde tu Nitakapopata matokeo katika hatua hii (Nitakapowafunua waovu wote wanaonipinga), Nitaanza hatua inayofuata, kwa maana mapenzi Yangu hayazuiwi na hakuna mtu anayethubutu kuzuia mpango Wangu wa usimamizi, na hakuna kitu kinachothubutu kuweka vizuizi vyovyote—lazima vyote viondoke njiani! Wazao wa joka kuu jekundu, Nisikieni! Nilikuja katika dunia hii kutoka Sayuni na kupata mwili ili kuwapata wazaliwa Wangu wa kwanza, kumfedhehesha baba yenu (maneno haya yanalenga wazao wa joka kuu jekundu), kuwategemeza wazaliwa Wangu wa kwanza, na kurekebisha makosa waliyofanyiwa wazaliwa Wangu wa kwanza. Kwa hivyo, msiwe wajeuri tena; Nitawaacha wazaliwa Wangu wa kwanza washughulike na nyinyi. Zamani, wana Wangu walidhulumiwa na kukandamizwa, na kwa kuwa Baba anatumia mamlaka kwa ajili ya wana Wake, wana Wangu watarudi kwenye kumbatio Langu la upendo, hawatadhulumiwa na kukandamizwa tena. Mimi si mdhalimu; hili linaonyesha haki Yangu, na kwa kweli ni “kuwapenda wale Ninaowapenda na kuwachukia wale Ninaowachukia.” Mkisema Mimi ni mdhalimu, basi mnapaswa kufanya haraka na kutoka nje. Msiwe wasio na aibu na wadoezi katika nyumba Yangu. Unapaswa kurudi nyumbani kwako haraka iwezekanavyo ili Nisilazimike kukuona tena. Shimo lisilo na mwisho ndilo hatima yenu, na hapo ndipo mtakaposalia. Mkiwa katika nyumba Yangu, hakutakuwa na nafasi kwa ajili yenu, kwa sababu ninyi ni wanyama wa kubeba mizigo; ninyi ndio zana Ninazotumia. Wakati Siwahitaji tena, Nitawatupa motoni ili kuwateketeza. Hii ni amri Yangu ya utawala. Lazima Nifanye namna hii—hili pekee ndilo linaloonyesha namna Ninavyofanya kazi, pamoja na haki Yangu na uadhama Wangu. La muhimu zaidi, ni kwa namna hii tu ndiyo wazaliwa Wangu wa kwanza wataruhusiwa kutawala katika mamlaka pamoja na Mimi.

Iliyotangulia:  Matamko ya Kristo Mwanzoni—Sura ya 88

Inayofuata:  Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima—Sura ya 4

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger