Yote Yanakamilishwa kwa Neno la Mungu

Mungu hunena maneno Yake na kufanya kazi Yake kulingana na enzi tofauti, na katika enzi tofauti, Yeye hunena maneno tofauti. Mungu hafuati taratibu, wala harudii kazi ileile, wala hashikilii mambo ya zamani; Yeye ni Mungu ambaye daima ni mpya na si wa zamani kamwe, na Yeye hunena maneno mapya kila siku. Unapaswa kuyafuata yale yanayopaswa kufuatwa katika wakati wa sasa; hili ni jukumu na wajibu wa mwanadamu. Ni muhimu kwamba utendaji ujikite katika nuru na maneno ya Mungu katika wakati wa sasa. Mungu hafuati taratibu, na anaweza kunena kutoka katika mitazamo mingi tofauti ili kufichua hekima na uweza Wake. Haijalishi kama Ananena kutoka katika mtazamo wa Roho, au wa mwanadamu, au wa mtu mwingine—Mungu daima ndiye Mungu, na huwezi kusema kwamba Yeye si Mungu kwa sababu Ananena kutoka katika mtazamo wa mwanadamu. Watu wengine wamepata dhana kutokana na mitazamo tofauti ambayo Mungu hunena kutoka kwayo. Watu kama hao hawana maarifa ya Mungu, na hawana maarifa ya kazi Yake. Ikiwa Mungu daima angenena kutoka katika mtazamo mmoja, je, mwanadamu hangemwekea Mungu mipaka? Je, Mungu angeruhusu mwanadamu kutenda kwa namna hiyo? Bila kujali Mungu ananena kutoka katika mtazamo upi, Yeye ana makusudi ya kufanya hivyo. Ikiwa Mungu daima angenena kutoka katika mtazamo wa Roho, je, ungeweza kuwasiliana na Yeye? Hivyo, wakati mwingine Yeye hunena kutoka katika mtazamo wa mtu mwingine ili kukukimu na kukuongoza kuingia katika uhalisi. Kila jambo analofanya Mungu linafaa. Kwa ufupi, yote yanafanywa na Mungu, na hupaswi kutilia shaka jambo hili. Yeye ndiye Mungu, na hivyo haijalishi Ananena kutoka katika mtazamo upi, Yeye daima atakuwa Mungu. Huu ni ukweli usiobadilika kamwe. Vyovyote Anavyofanya kazi, Yeye bado ndiye Mungu, na kiini Chake hakitabadilika! Petro alimpenda Mungu sana na alikuwa mtu aliyekuwa akipatana na nia za Mungu, lakini Mungu hakumshuhudia kama Bwana wala Kristo, kwa maana kiini cha kiumbe ni jinsi kilivyo, na hakiwezi kubadilika kamwe. Katika kazi Yake, Mungu hafuati taratibu, bali anatumia mbinu tofauti ili kuifanya kazi Yake iwe yenye ufanisi na kumfanya mwanadamu kumjua Yeye kwa kina. Kusudi la kila mbinu Yake ya kufanya kazi ni kumsaidia mwanadamu kumjua Yeye na ni kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Haijalishi ni mbinu ipi ya kufanya kazi Anayotumia, kila moja ni ili kumjenga mwanadamu na kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Ingawa mojawapo ya mbinu Zake za kufanya kazi inaweza kuwa imedumu kwa muda mrefu sana, hii ni ili kuimarisha imani ya mwanadamu Kwake. Hivyo, hampaswi kuwa na shaka katika mioyo yenu. Hizi zote ni hatua za kazi ya Mungu, na ninyi lazima mzitii.

Kile kinachozungumziwa katika wakati wa sasa ni kuingia katika uhalisi—si kupaa mbinguni, wala kutawala kama wafalme; yote yanayozungumziwa ni ufuatiliaji wa kuingia katika uhalisi. Hakuna ufuatiliaji wa vitendo zaidi kuliko huu, na kuzungumzia kutawala kama wafalme si jambo la uhalisi. Mwanadamu ana udadisi mkubwa, na anapima kazi ya Mungu katika wakati wa sasa kwa dhana zake za kidini. Baada ya kupitia mbinu nyingi sana za Mungu za kufanya kazi, mwanadamu bado haijui kazi ya Mungu, bado anatafuta ishara na maajabu, na bado anatazama kuona kama maneno ya Mungu yametimia. Je, huu si upofu uliopitiliza? Ikiwa maneno ya Mungu hayajatimia, je, bado ungeamini kwamba Yeye ndiye Mungu? Katika wakati wa sasa, watu wengi kama hao kanisani wanangoja kuona ishara na maajabu. Wanasema kwamba maneno ya Mungu yakitimia, basi Yeye ndiye Mungu; maneno ya Mungu yasipotimia, basi Yeye si Mungu. Je, basi, unamwamini Mungu kwa sababu maneno Yake yametimia, au kwa sababu Yeye ndiye Mungu Mwenyewe? Mtazamo wa mwanadamu wa imani katika Mungu lazima urekebishwe! Unapoona kwamba maneno ya Mungu hayajatimia, unakimbia—huyu ni mwumini wa aina gani? Unapomwamini Mungu, lazima utii mipango ya Mungu katika mambo yote na utii kazi yote ya Mungu. Mungu alinena maneno mengi sana katika Agano la Kale—ni yapi kati ya hayo uliyoyaona yakitimia kwa macho yako mwenyewe? Je, unaweza kusema kwamba Yehova si Mungu wa kweli kwa sababu hukuyaona hayo? Ingawa maneno mengi yanaweza kuwa yametimia, mwanadamu hawezi kuyaona hayo waziwazi kwa sababu mwanadamu hana ukweli na haelewi chochote. Wengine hutaka kukimbia wanapohisi kwamba maneno ya Mungu hayajatimia. Jaribu. Uone kama utaweza kukimbia. Baada ya kukimbia, bado utarudi. Mungu anakudhibiti kwa neno Lake, na ukiondoka kanisani na kuliacha neno la Mungu, hutakuwa na namna ya kuendelea kuishi. Usipoamini hili, lijaribu mwenyewe—unafikiri unaweza kuondoka tu? Roho wa Mungu anakudhibiti. Huwezi kuondoka. Hii ni amri ya utawala wa Mungu! Watu wengine wakitaka kujaribu, wanaweza! Unasema mtu huyu si Mungu, basi mkosee Yeye na uone kile Atakachofanya. Inawezekana kwamba mwili wako hautakufa na bado utaweza kula na kuvaa, lakini kiakili hutaweza kuvumilia; utahisi msongo na maumivu; hakuna kitakachokuwa cha kuumiza zaidi kuliko hayo. Mwanadamu hawezi kuvumilia mateso na maumivu ya kiakili—labda unaweza kuvumilia mateso ya mwili, lakini huwezi kabisa kuvumilia msongo wa kiakili na mateso ya muda mrefu. Katika wakati wa sasa, watu wengine huwa hasi kwa sababu hawajaweza kuona ishara na maajabu yoyote, lakini hakuna anayethubutu kukimbia haijalishi wanakuwa hasi kiasi gani, kwa maana Mungu humdhibiti mwanadamu kwa neno Lake. Licha ya kwamba ukweli haujatokea, bado hakuna anayeweza kutoroka. Je, haya si matendo ya Mungu? Katika wakati wa sasa, Mungu amekuja duniani ili kumpa mwanadamu uzima. Yeye hakubembelezi daima, kama watu wanavyowazia, kwa kuonyesha ishara na maajabu ili kudumisha uhusiano wa amani kati ya Mungu na mwanadamu. Wale wote ambao mkazo wao hauko kwenye uzima, na ambao badala yake wanazingatia kumfanya Mungu aonyeshe ishara na maajabu, ni Mafarisayo! Na ni Mafarisayo ndio waliomsulubisha Yesu msalabani. Ukimpima Mungu kulingana na mtazamo wako mwenyewe wa imani katika Mungu, ukimwamini Mungu ikiwa maneno Yake yametimia, na kuwa na shaka na hata kumkufuru Mungu ikiwa hayajatimia, basi je, humsulubishi Yeye msalabani? Watu kama hawa hawashughulikii wajibu wao ipasavyo, na hutamani starehe!

Kipengele kimoja cha tatizo kubwa zaidi linalomkabili mwanadamu ni kwamba hajui kazi ya Mungu. Ingawa mtazamo wa mwanadamu si wa kukana, ni wa shaka. Mwanadamu hakani, lakini pia hakubali kikamilifu. Ikiwa watu wana ufahamu kamili wa kazi ya Mungu, hawatakimbia. Kipengele kingine ni kwamba mwanadamu hajui uhakika. Katika wakati wa sasa, ni neno la Mungu ndilo ambalo kila mtu amekutana nalo; kusema ukweli, usifikiri kwamba utaweza kuona ishara na maajabu katika siku zijazo. Ninakuambia waziwazi: Wakati wa hatua ya sasa, yote unayoweza kuona ni maneno ya Mungu, na ingawa hakuna ukweli uliotokea, uzima wa Mungu bado unaweza kutendeka ndani ya mwanadamu. Ni kazi hii ndiyo kazi kuu ya Ufalme wa Milenia, na ikiwa huwezi kutambua kazi hii, basi utakuwa dhaifu na kuanguka; utaingia katikati ya majaribu na, katika hali mbaya zaidi, utatiwa utumwani na Shetani. Mungu amekuja duniani hasa kunena maneno Yake; kile unachokutana nacho ni neno la Mungu, kile unachosoma ni neno la Mungu, kile unachosikia ni neno la Mungu, kile unachofuata ni neno la Mungu, kile unachopitia ni neno la Mungu, na katika kupata mwili wakati huu, Mungu hasa anatumia neno kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Yeye haonyeshi ishara na maajabu, na hasa hafanyi kazi Aliyofanya Yesu zamani. Ingawa Wao ni Mungu, na wote wawili ni mwili, huduma Zao si sawa. Yesu alipokuja, Yeye pia alifanya sehemu ya kazi ya Mungu na kunena baaadhi ya maneno —lakini ni kazi gani kuu Aliyoikamilisha? Kile Alichokamilisha hasa kilikuwa kazi ya kusulubiwa. Alikuwa mfano wa mwili wenye dhambi ili kukamilisha kazi ya kusulubiwa na kuwakomboa binadamu wote, na Alihudumu kama sadaka ya dhambi kwa ajili ya dhambi za binadamu wote. Hii ndiyo kazi kuu Aliyoikamilisha. Hatimaye, Aliwaonyesha njia ya msalaba wale waliokuja baadaye. Yesu alipokuja, ilikuwa hasa ili kukamilisha kazi ya ukombozi. Aliwakomboa binadamu wote, na kumletea mwanadamu injili ya ufalme wa mbinguni, na, zaidi ya hayo, Alionyesha njia ya kuingia katika ufalme wa mbinguni. Matokeo yake, wale wote waliokuja baadaye walisema, "Tunapaswa kutembea katika njia ya msalaba, na kujitoa mhanga kwa ajili ya msalaba." Bila shaka, mwanzoni, Yesu pia alifanya kazi nyingine na kunena baadhi ya maneno ili kumfanya mwanadamu atubu na kuungama dhambi zake. Lakini huduma Yake bado ilikuwa kusulubiwa, na miaka mitatu na nusu Aliyotumia kuhubiri njia ilikuwa matayarisho kwa ajili ya kusulubiwa kulikokuja baadaye. Nyakati kadhaa ambazo Yesu aliomba pia zilikuwa kwa ajili ya kusulubiwa. Maisha ya kawaida ya kibinadamu Aliyoyaishi na miaka thelathini na mitatu na nusu Aliyoishi duniani yalikuwa hasa kwa ajili ya kukamilisha kazi ya kusulubiwa; yalikuwa ya Kumpa Yeye nguvu ya kubeba kazi hii. Ndiyo maana inasemwa kwamba Mungu alimwaminia Yeye kazi ya kusulubiwa. Mungu mwenye mwili atakamilisha kazi gani katika wakati wa sasa? Katika wakati wa sasa, Mungu amekuwa mwili hasa ili kukamilisha kazi ya "Neno kuonekana katika mwili." Yeye anatumia neno kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na kumfanya mwanadamu akubali kupogolewa na neno na kusafishwa na neno. Katika maneno Yake Anakufanya upate riziki na upate uzima, na anakufanya uone kazi na matendo Yake. Mungu anatumia neno kukuadibu na kukusafisha, na hivyo, hata ukipata maumivu, ni kwa sababu ya neno la Mungu pia. Katika wakati wa sasa, Mungu hafanyi kazi kwa ukweli, bali kwa maneno. Ni baada tu ya neno Lake kukujia ndiyo Roho Mtakatifu anaweza kufanya kazi ndani yako na kukufanya uhisi maumivu au uonje utamu. Ni neno la Mungu pekee linaloweza kukuingiza katika uhalisi, na ni neno la Mungu pekee linaloweza kukufanya kuwa mtimilifu. Kwa hivyo, angalau lazima uelewe hili: Kazi inayofanywa na Mungu katika siku za mwisho hasa ni ile ya kutumia neno Lake kumfanya kila mtu kuwa mtimilifu na kumwelekeza mwanadamu. Kazi yote Anayofanya ni kupitia neno; Yeye hatumii ukweli kukuadibu. Kuna nyakati ambapo watu wengine humpinga Mungu. Mungu hakusababishii mateso mkubwa, mwili wako hauadibiwi, wala hauhisi maumivu yoyote—lakini mara tu neno Lake linapokujia, na kukusafisha, inakuwa isiyovumilika kwako. Je, si hivyo ndivyo ilivyo? Wakati wa watendaji huduma, Mungu alisema amtumbukize mwanadamu katika shimo lisilo na mwisho. Je, mwanadamu kweli aliishia katika shimo lisilo na mwisho? Kwa kutumia tu maneno kumsafisha mwanadamu, mwanadamu aliingia katika shimo lisilo na mwisho. Kwa hivyo, katika siku za mwisho, Mungu anapokuwa mwili, Anatumia hasa neno kukamilisha yote na kufichua yote. Ni katika maneno Yake pekee ndiyo unaweza kuona kile Alicho; ni katika maneno Yake pekee ndiyo unaweza kuona kwamba Yeye ndiye Mungu Mwenyewe. Mungu mwenye mwili anapokuja duniani, Yeye hafanyi kazi nyingine isipokuwa kunena maneno—hivyo hakuna haja ya ukweli; maneno pekee yanatosha. Hiyo ni kwa sababu Amekuja hasa kufanya kazi hii, kumwezesha mwanadamu kuuona uweza Wake mkuu na ukuu Wake katika maneno Yake, kumwezesha mwanadamu kuona unyenyekevu na kufichika Kwake katika maneno Yake, na kumwezesha mwanadamu kumjua kikamilifu kupitia maneno Yake. Kile Anacho na Alicho kiko katika maneno Yake. Hekima na maajabu Yake viko katika maneno Yake. Katika hili unaweza kuona mbinu nyingi ambazo Mungu anatumia kunena maneno Yake. Mungu amekuwa akifanya kazi kwa muda mrefu sana, na mara nyingi Amekuwa akimkimu mwanadamu, akimfichua, au akimpogoa. Mungu hamlaani mtu kiurahisi, na hata Anapofanya hivyo, ni kupitia neno ndiyo Yeye humlaani. Kwa hivyo, katika enzi hii ya Mungu kuwa mwili, usitarajie kumwona Mungu akiwaponya wagonjwa na kuondosha mapepo tena, na uache kuendelea kutafuta ishara —hazina manufaa yoyote! Ishara hizo haziwezi kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu! Kusema waziwazi: Katika wakati wa sasa, Mungu wa vitendo Mwenyewe wa mwili hatendi; Ananena tu. Huu ndio ukweli! Yeye anatumia maneno kukufanya kuwa mtimilifu, na anatumia maneno kukulisha na kukunyunyizia. Anatumia pia maneno kufanya kazi, na Anatumia maneno kuchukua nafasi ya ukweli na kukufanya ujue uhakika Wake. Ukiona namna hii ya kazi ya Mungu waziwazi, basi haitakuwa rahisi kwako kuwa hasi. Badala ya kuzingatia mambo yaliyo hasi, ninyi mnapaswa kuzingatia tu yale yaliyo chanya—yaani, bila kujali kama maneno ya Mungu yametimia au la, au kama ukweli umetokea au la, Mungu humsababisha mwanadamu kupata uzima kutoka katika maneno Yake, na hii ndiyo ishara kuu zaidi ya zote; na hata zaidi, ni ukweli usiopingika. Huu ndio ushahidi bora zaidi ambao kupitia kwa ushahidi huo mnaweza kumjua Mungu, na ni ishara kuu hata zaidi kuliko ishara. Ni maneno haya pekee yanayoweza kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu.

Mara tu Enzi ya Ufalme ilipoanza, Mungu alianza kutoa maneno Yake. Katika siku zijazo, maneno haya yatatimia hatua kwa hatua, na wakati huo, uzima wa mwanadamu utakuwa tayari umekomaa. Mungu anatumia neno kufichua tabia potovu za mwanadamu; jambo hili ni la vitendo zaidi, na la lazima zaidi. Yeye hatumii chochote isipokuwa neno kufanya kazi Yake ili kuifanya imani ya mwanadamu kuwa timilifu, kwa maana wakati wa sasa ni Enzi ya Neno, na inahitaji imani, azimio, na ushirikiano wa mwanadamu. Kazi ya Mungu mwenye mwili katika siku za mwisho ni kutumia neno Lake kumhudumia na kumkimu mwanadamu. Ni baada tu ya Mungu mwenye mwili kumaliza kunena maneno Yake ndiyo yataanza kutimia. Wakati Anaponena, maneno Yake hayatimii, kwa sababu Anapokuwa katika hatua ya mwili, maneno Yake hayawezi yakatimia. Hii ni ili kwamba mwanadamu aweze kuona kwamba Mungu ni mwili wala si Roho; ili kwamba mwanadamu aweze kuuona uhakika wa Mungu kwa macho yake mwenyewe. Siku ambayo kazi Yake itakamilika, wakati maneno yote yanayopaswa kunenwa na Yeye duniani yatakuwa yamenenwa, maneno Yake yataanza kutimia. Sasa si enzi ya kutimia kwa maneno ya Mungu, kwa sababu hajamaliza kunena maneno Yake. Hivyo, unapoona kwamba Mungu bado ananena maneno Yake duniani, usingoje kutimia kwa maneno Yake; Mungu anapoacha kunena maneno Yake, na wakati kazi Yake duniani itakapokuwa imekamilika, huo ndio utakuwa wakati ambapo maneno Yake yataanza kutimia. Katika maneno Anayonena duniani, kwa upande mmoja, kuna utoaji wa uzima, na kwa upande mwingine, kuna unabii—unabii wa mambo yatakayokuja, mambo yatakayofanywa, na mambo ambayo hayajatimizwa. Kulikuwa pia na unabii katika maneno ya Yesu. Kwa upande mmoja, Alitoa uzima, na kwa upande mwingine, Alinena unabii. Katika wakati wa sasa, hakuna mazungumzo ya maneno na ukweli kwenda sambamba kwa sababu kuna tofauti kubwa mno kati ya kile kinachoweza kuonekana kwa macho ya mwanadamu mwenyewe na ukweli unaotekelezwa na Mungu. Inaweza tu kusemwa kwamba mara tu kazi ya Mungu itakapokamilika, maneno Yake yatatimia, na ukweli utakuja baada ya maneno. Katika siku za mwisho, Mungu mwenye mwili anakuja duniani kutekeleza huduma ya neno, na katika kutekeleza huduma ya neno, Ananena maneno tu, na hajali mambo mengine. Mara tu kazi ya Mungu inapobadilika, maneno Yake yataanza kutimia. Katika wakati wa sasa, maneno yanatumiwa kwanza kukufanya kuwa mtimilifu; Anapopata utukufu katika ulimwengu mzima, kazi Yake itakuwa imekamilika—maneno yote yanayopaswa kunenwa yatakuwa yamenenwa, na maneno yote yatakuwa yamekuwa ukweli. Mungu amekuja duniani katika siku za mwisho kutekeleza huduma ya neno ili kwamba binadamu waweze kumjua Yeye, na ili kwamba binadamu waweze kuona kile Alicho, pamoja na hekima Yake na matendo Yake yote ya ajabu, kutoka katika neno Lake. Katika Enzi ya Ufalme, Mungu hasa anatumia neno kuwashinda binadamu wote. Katika siku zijazo, neno Lake pia litakuja juu ya kila dini, sekta, taifa na dhehebu. Mungu anatumia neno kushinda, ili kuwafanya watu wote waone kwamba neno Lake lina mamlaka na uweza—na hivyo katika wakati wa sasa, ninyi mnakabiliana tu na neno la Mungu.

Maneno yanayonenwa na Mungu katika enzi hii ni tofauti na yale yaliyonenwa katika Enzi ya Sheria, na hivyo, pia, yanatofautiana na maneno yaliyonenwa katika Enzi ya Neema. Kazi ya neno haikufanywa katika Enzi ya Neema; kulikuwa tu na kutajwa kwa Mungu kusulubiwa ili kuwakomboa binadamu wote. Biblia inarejelea tu kwa nini Yesu alipaswa kusulubiwa, mateso Aliyoyapitia wakati wote wa kusulubiwa, na jinsi mwanadamu alivyopaswa kusulubiwa kwa ajili ya Mungu. Katika enzi hiyo, kazi yote iliyofanywa na Mungu ilijikita katika kusulubiwa. Katika Enzi ya Ufalme, Mungu mwenye mwili ananena maneno ili kuwashinda wale wote wanaomwamini Yeye. Hili ndiyo "Neno kuonekana katika mwili"; Mungu amekuja katika siku za mwisho kufanya kazi hii, na kutimiza maana halisi ya Neno kuonekana katika mwili. Ananena maneno tu, na ni nadra ukweli kutokea. Hiki ndicho kiini hasa cha Neno kuonekana katika mwili, na Mungu mwenye mwili anaponena maneno Yake, hili ndilo kuonekana kwa Neno katika mwili, na ndilo Neno kuja katika mwili. "Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu, naye Neno akawa mwili." Hii (kazi ya kuonekana kwa Neno katika mwili) ndiyo kazi ambayo Mungu ataikamilisha katika siku za mwisho, na ndiyo sura ya mwisho ya mpango Wake wote wa usimamizi, na hivyo Mungu lazima aje duniani na kudhihirisha maneno Yake katika mwili. Kile kinachofanywa katika wakati wa sasa, kile kitakachofanywa katika siku sijazo, kile kitakachotimizwa na Mungu, hatima ya mwisho ya mwanadamu, ni nani atakayeokolewa, ni nani atakayeangamizwa, na kadhalika—kazi hii yote inayopaswa kufikiwa mwishoni imeelezwa waziwazi, na haya yote ni ili kutimiza maana halisi ya Neno kuonekana katika mwili. Amri za utawala na katiba zilizotolewa hapo awali, ni nani atakayeangamizwa, ni nani atakayeingia katika pumziko—maneno haya yote lazima yatimie. Hii ndiyo kazi hasa inayotimizwa na Mungu mwenye mwili katika siku za mwisho, ili kwamba watu waweze kuelewa mahali wale walioamuliwa kabla na Mungu wataishia na mahali wale ambao hawajaamuliwa kabla na Mungu wataishia, jinsi watu Wake na wana Wake watakavyoainishwa, kile kitakachotokea kwa Israeli, kile kitakachotokea kwa Misri—katika siku zijazo, kila moja ya maneno haya litatimia. Kasi ya kazi ya Mungu inaongezeka. Mungu anatumia neno kama namna ya kumfichulia mwanadamu kile kinachopaswa kufanywa katika kila enzi, kile kinachopaswa kufanywa na Mungu mwenye mwili wa siku za mwisho, na huduma Yake inayopaswa kutekelezwa, na maneno haya yote ni ili kutimiza maana halisi ya Neno kuonekana katika mwili.

Nimesema hapo awali kwamba "Wale wote wanaozingatia kuona ishara na maajabu watatelekezwa; wao si wale watakaofanywa kuwa watimilifu." Nimenena maneno mengi sana, lakini mwanadamu bado hana ufahamu hata kidogo wa kazi hii, na, baada ya kufika katika hatua hii, bado watu wanaomba ishara na maajabu. Je, imani yako katika Mungu si chochote zaidi ya ufuatiliaji wa ishara na maajabu, au ni ili kupata uzima? Yesu pia alinena maneno mengi, na baadhi ya hayo bado hayajatimia. Je, unaweza kusema kwamba Yesu si Mungu? Mungu alishuhudia kwamba Yeye alikuwa Kristo na Mwana mpendwa wa Mungu. Je, unaweza kukana jambo hili? Katika wakati wa sasa, Mungu ananena maneno tu, na ikiwa hulijui hili kikamilifu, basi huwezi kusimama imara. Je, unamwamini Yeye kwa sababu Yeye ni Mungu, au unamwamini Yeye kwa kutegemea iwapo maneno Yake yanatimia au la? Je, unaamini katika ishara na maajabu, au unamwamini Mungu? Katika wakati wa sasa, Yeye haonyeshi ishara na maajabu—je, Yeye ndiye Mungu kweli? Ikiwa maneno Anayonena hayatimii, je, Yeye ndiye Mungu kweli? Je, kiini cha Mungu huamuliwa na iwapo maneno Anayonena yanatimia au la? Kwa nini watu wengine daima hungoja kutimia kwa maneno ya Mungu kabla ya kumwamini Yeye? Je, hili halimaanishi kwamba hawamjui Yeye? Wale wote walio na dhana kama hizo ndio wale wanaomkana Mungu. Wanatumia dhana kumpima Mungu; ikiwa maneno ya Mungu yanatimia, wanamwamini Yeye, na ikiwa hayatimii, basi hawamwamini Yeye; na daima wanafuatilia kuona ishara na maajabu. Je, watu hawa si Mafarisayo wa nyakati za sasa? Iwapo unaweza kusimama imara au la kunategemea iwapo unamjua Mungu wa vitendo au la—hili ni jambo muhimu sana! Kadiri uhalisi wa neno la Mungu unavyokuwa mkubwa ndani yako, ndivyo maarifa yako ya uhakika wa Mungu yanavyokuwa makubwa zaidi, na ndivyo unavyoweza zaidi kusimama imara wakati wa majaribu. Kadiri unavyozingatia zaidi kuona ishara na maajabu, ndivyo unavyoshindwa zaidi kusimama imara, na utaanguka katikati ya majaribu. Ishara na maajabu si msingi; uhakika wa Mungu pekee ndio uzima. Watu wengine hawajui matokeo yanayopaswa kufikiwa na kazi ya Mungu. Wanatumia siku zao wakiwa katika mkanganyiko, bila kufuatilia maarifa ya kazi ya Mungu. Lengo la ufuatiliaji wao daima ni kumfanya Mungu atimize matamanio yao tu, na ni hapo tu ndipo watakapokuwa makini katika imani yao. Wanasema kwamba watafuatilia uzima ikiwa maneno ya Mungu yatatimia, lakini kwamba ikiwa maneno Yake hayatatimia, basi hakuna uwezekano wa wao kufuatilia uzima. Watu wanafikiri kwamba imani katika Mungu ni ufuatiliaji wa kuona ishara na maajabu na ufuatiliaji wa kupaa mbinguni na mbingu ya tatu. Hakuna hata mmoja wao anayesema kwamba imani yake katika Mungu ni ufuatiliaji wa kuingia katika uhalisi, ufuatiliaji wa uzima, na ufuatiliaji wa kupatwa na Mungu. Kuna thamani gani katika ufuatiliaji kama huu? Wale wasiofuatilia maarifa ya Mungu na kumridhisha Mungu si wale wanaomwamini Mungu; wao ndio wanaomkufuru Mungu!

Sasa ninyi mnaelewa imani katika Mungu ni nini? Je, imani katika Mungu inamaanisha kuona ishara na maajabu? Je, inamaanisha kupaa mbinguni? Kumwamini Mungu si jambo rahisi hata kidogo. Njia za kidini za imani zinapaswa kuondolewa; kufuatilia kuponya wagonjwa na kuondosha mapepo, kuzingatia ishara na maajabu, kutamani zaidi neema, amani na furaha ya Mungu, kufuatilia matarajio na starehe za mwili—hizi ni njia za kidini za imani, na njia kama hizo za imani ni aina ya imani isiyo yakini. Imani ya vitendo katika Mungu katika wakati wa sasa ni nini? Ni kulikubali neno la Mungu kama uhalisi wa maisha yako, kumjua Mungu kutoka katika neno Lake, na hivyo kufikia upendo wa kweli Kwake. Kusema wazi: Imani katika Mungu ni ili kwamba uweze kumtii Mungu, kumpenda Mungu, na kutimiza wajibu unaopaswa kutimizwa na kiumbe aliyeumbwa. Hili ndilo lengo la kumwamini Mungu. Lazima uje kujua kupendeza kwa Mungu, jinsi Mungu anavyostahili kuheshimiwa, na jinsi kazi anayofanya Mungu juu ya viumbe Wake walioumbwa ilivyo wokovu wao na kufanywa kwao kuwa watimilifu—haya ndiyo mambo ya msingi kabisa ya imani yako katika Mungu. Imani katika Mungu hasa ni kuhama kutoka katika maisha ya mwili kwenda maisha ya kumpenda Mungu, na kutoka katika kuishi katika upotovu kwenda kuishi katika uzima wa maneno ya Mungu; ni kutoka chini ya nguvu za Shetani na kuishi chini ya utunzaji na ulinzi wa Mungu; ni ili kwamba uweze kumtii Mungu badala ya mwili, ili kwamba Mungu aweze kuupata moyo wako wote na kukufanya kuwa mtimilifu, na ili kwamba uweze kuwekwa huru kutoka katika tabia potovu za kishetani. Imani katika Mungu hasa ni ili kwamba uweza mkuu na utukufu wa Mungu uweze kudhihirishwa ndani yako, ili kwamba uweze kufuata mapenzi ya Mungu, ili kwamba mpango wa Mungu uweze kutimizwa, na ili kwamba uweze kumshuhudia Mungu mbele ya Shetani. Imani katika Mungu haipaswi kujikita katika tamaa ya kuona ishara na maajabu, wala haipaswi kuwa kwa ajili ya mwili wako mwenyewe. Inapaswa kuwa kuhusu ufuatiliaji wa kumjua Mungu, kuweza kumtii Mungu, na, kama Petro, kumtii Yeye hadi kufa. Kusudi kuu ni kufikia jambo hili. Mtu hula na kunywa neno la Mungu pia ili kumjua Mungu na kumridhisha Yeye. Kula na kunywa neno la Mungu hukupa maarifa makubwa zaidi ya Mungu, ambapo ni baada ya hapo tu ndipo unaweza kumtii Yeye. Ni kwa kuwa na maarifa ya Mungu pekee ndiyo unaweza kumpenda Yeye, na hili pekee ndilo lengo ambalo mwanadamu anapaswa kuwa nalo katika imani yake katika Mungu. Ikiwa, katika imani yako katika Mungu, daima unatamani kuona ishara na maajabu, basi mtazamo huu juu ya imani katika Mungu si sahihi. Imani katika Mungu hasa ni kuyakubali maneno ya Mungu kama uhalisi wa maisha ya mtu. Wakati maneno yanayotoka kinywani mwa Mungu yanapowekwa katika vitendo na watu na kutimizwa ndani yao, lengo la Mungu linafikiwa. Katika kumwamini Mungu, mwanadamu anapaswa kufuatilia kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu, kuweza kumtii Mungu, na kufikia utii kamili kwa Mungu. Ikiwa unaweza kumtii Mungu bila malalamiko, unaweza kujali nia za Mungu, na kufikia kimo cha Petro, ukiwa na mtindo wa Petro uliozungumziwa na Mungu, basi huo ndio utakuwa wakati ambapo umefanikiwa katika imani katika Mungu, na utamaanisha kwamba umepatwa na Mungu.

Mungu anafanya kazi Yake katika ulimwengu mzima. Wale wote wanaomwamini Yeye lazima walikubali neno Lake, na kula na kunywa neno Lake; hakuna anayeweza kupatwa na Mungu kwa kuona ishara na maajabu yanayoonyeshwa na Mungu. Katika enzi zote na vizazi vyote, Mungu daima ametumia neno kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Hivyo hampaswi kuweka umakini wenu wote kwenye ishara na maajabu, bali mnapaswa kufuatilia kufanywa kuwa watimilifu na Mungu. Katika Enzi ya Sheria ya Agano la Kale, Mungu alinena baadhi ya maneno, na katika Enzi ya Neema, Yesu, pia, alinena maneno mengi. Baada ya Yesu kusema maneno mengi, mitume na wanafunzi wa baadaye waliwaongoza watu kutenda kulingana na amri zilizotolewa na Yesu, na wakapitia mambo kulingana na maneno yaliyonenwa na Yesu na kanuni Alizowasilisha. Katika siku za mwisho, Mungu hasa anatumia neno kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Yeye hatumii ishara na maajabu kumlazimisha mwanadamu asadiki; jambo hili haliwezi kufichua uweza mkuu wa Mungu. Ikiwa Mungu angeonyesha tu ishara na maajabu, hili halingeweza kufichua uhakika wa Mungu, na hili halingeweza kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Mungu hamfanyi mwanadamu kuwa mtimilifu kwa ishara na maajabu, bali anatumia neno ili kumnyunyizia na kumchunga mwanadamu, ambapo baada ya hapo mwanadamu anaweza kumtii Mungu kikamilifu na kupata maarifa ya Mungu. Hili ndilo lengo la kazi Anayofanya na maneno Anayonena. Mungu hatumii mbinu ya kuonyesha ishara na maajabu ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu—Yeye anatumia maneno, na anatumia mbinu nyingi za kazi ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu. Iwe ni usafishaji, upogoaji, au utoaji wa maneno, Mungu ananena kutoka katika mitazamo mingi tofauti ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na kumwezesha mwanadamu kupata maarifa zaidi ya kazi, hekima na maajabu ya Mungu. Mwanadamu anapofanywa kuwa kamili wakati ambapo Mungu anahitimisha enzi katika siku za mwisho, basi atastahili kuona ishara na maajabu. Unapokuja kumjua Mungu na kuweza kumtii Mungu haijalishi kile Anachofanya, hutakuwa tena na dhana zozote kumhusu Yeye unapoona ishara na maajabu. Kwa sasa, wewe ni mpotovu na huwezi kuwa na utii kamili kwa Mungu—je, unafikiri kwamba una sifa ya kuona ishara na maajabu? Mungu anapoonyesha ishara na maajabu, huo ndio wakati ambapo Mungu anamuadhibu mwanadamu, na pia ndio wakati ambapo enzi inabadilika, na, hata zaidi, ndio wakati ambapo enzi inahitimishwa. Wakati kazi ya Mungu inatekelezwa kwa kawaida, Yeye haonyeshi ishara na maajabu. Kuonyesha ishara na maajabu ni rahisi sana Kwake, lakini hiyo si kanuni ya kazi ya Mungu, wala si lengo la usimamizi wa Mungu kwa mwanadamu. Ikiwa mwanadamu angeona ishara na maajabu, na mwili wa kiroho wa Mungu pia ungeonekana kwa mwanadamu, je, watu wote hawange"mwamini" Mungu? Nilisema hapo awali kwamba kundi la washindi lingepatikana kutoka katika Mashariki, washindi ambao wangetoka katika dhiki kuu. Maneno haya yanamaanisha nini? Yanamaanisha kwamba watu hawa wanaopatikana wanakuwa watiifu kweli tu baada ya kupitia hukumu, kuadibu, upogoaji, na kila aina ya usafishaji. Imani ya watu hawa si isiyo yakini, bali ni ya vitendo. Hawajaona ishara na maajabu yoyote, wala miujiza yoyote; hawawezi kunena maneno na mafundisho makuu, au kutoa umaizi wa kina; badala yake, wana uhalisi, na maneno ya Mungu, na maarifa ya vitendo na ya kweli ya Mungu. Je, kundi kama hilo haliwezi kufichua uweza mkuu wa Mungu vyema zaidi? Kazi ya Mungu katika siku za mwisho ni kazi ya vitendo. Katika enzi ya Yesu, Yeye hakuja kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, bali kumkomboa mwanadamu, na hivyo Alionyesha miujiza kadhaa ili kuwafanya watu wamfuate Yeye. Kwa maana Alikuja hasa kukamilisha kazi ya kusulubiwa, na kuonyesha ishara hakukuwa sehemu ya kazi ya huduma Yake. Ishara na maajabu kama hayo yalikuwa kazi iliyofanywa ili kuifanya kazi Yake iwe na ufanisi; yalikuwa kazi ya ziada, na hayakuwakilisha kazi ya enzi nzima. Katika Enzi ya Sheria ya Agano la Kale, Mungu pia alionyesha ishara na maajabu kadhaa—lakini kazi anayofanya Mungu katika wakati wa sasa ni kazi ya vitendo, na Yeye hakika hangeonyesha ishara na maajabu sasa. Ikiwa Angeonyesha ishara na maajabu, kazi Yake ya vitendo ingevurugwa, na Asingeweza kufanya kazi yoyote zaidi. Ikiwa Mungu angesema atumie neno ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, lakini pia aonyeshe ishara na maajabu, je, hilo lingeweza kufichua iwapo mwanadamu anamwamini Yeye kweli au la? Hivyo, Mungu hafanyi mambo kama hayo. Kuna mambo mengi sana ya kidini ndani ya mwanadamu; Mungu amekuja katika siku za mwisho ili kuondoa dhana zote za kidini na mambo ya kimiujiza ndani ya mwanadamu, ili kumfanya mwanadamu ajue uhakika wa Mungu, na kuondoa mfano wa Mungu ambao si yakini na usio na uhalisi, na ambao unaweza kusemwa kuwa haupo kabisa. Na hivyo, sasa jambo lililo la thamani pekee ni wewe kuwa na maarifa ya uhakika! Ukweli unashinda kila kitu. Una ukweli kiasi gani leo? Je, kila anayeonyesha ishara na maajabu ni Mungu? Roho waovu pia wanaweza kuonyesha ishara na maajabu; je, wote ni Mungu? Katika imani yake katika Mungu, kile ambacho mwanadamu anatafuta ni ukweli, na kile anachofuatilia ni uzima, badala ya ishara na maajabu. Hili linapaswa kuwa lengo la wale wote wanaomwamini Mungu.

Iliyotangulia:  Enzi ya Ufalme Ni Enzi ya Neno

Inayofuata:  Wale Wanaopaswa Kukamilishwa Lazima Wapitie Usafishaji

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger