Enzi ya Ufalme Ni Enzi ya Neno
Katika Enzi ya Ufalme, Mungu anatumia maneno kuileta enzi mpya, kubadilisha namna ambazo kwazo Anafanya kazi, na kufanya kazi ya enzi nzima. Hii ndiyo kanuni ambayo kwayo Mungu anafanya kazi katika Enzi ya Neno. Yeye alipata mwili na ananena kutoka katika mitazamo tofauti, akimwezesha mwanadamu amwone Mungu kweli, ambaye ndiye Neno linaoonekana katika mwili, na kuiona hekima Yake na kustaajabisha Kwake. Mungu anafanya kazi kwa namna hii ili kufikia vyema zaidi malengo ya kuwashinda watu, kuwafanya watu kuwa watimilifu, na kuwaondosha watu. Hii ndiyo maana halisi ya matumizi ya maneno kufanya kazi katika Enzi ya Neno. Kwa njia ya maneno, watu wanapata kuijua kazi ya Mungu, tabia ya Mungu, kiini cha mwanadamu, na kile ambacho mwanadamu anapaswa kukiingia. Kwa njia ya maneno, kazi yote ambayo Mungu anataka kufanya katika Enzi ya Neno inatimizwa. Kwa njia ya maneno, watu wanafunuliwa na wanaondoshwa, na wanajaribiwa. Watu wameyaona maneno haya, wameyasikia maneno haya, na wametambua uwepo wa maneno haya. Matokeo yake, wamekuja kuamini katika uwepo wa Mungu, uweza na hekima ya Mungu, na moyo wa Mungu wa kumpenda na kumwokoa mwanadamu. Neno “maneno” linaweza kuwa la kawaida na rahisi, lakini maneno yanayonenwa kutoka kinywani mwa Mungu mwenye mwili yanautikisa ulimwengu; yanaibadilisha mioyo ya watu, yanazibadilisha fikira zao na tabia za zamani, na yanabadilisha jinsi dunia nzima ilivyokuwa ikionekana. Katika enzi zote, ni Mungu wa leo pekee anayefanya kazi kwa namna hii, na ni Yeye pekee anayezungumza namna hii na anayemwokoa mwanadamu namna hii. Kuanzia wakati huu kuendelea, mwanadamu anaishi chini ya mwongozo wa maneno ya Mungu, katikati ya uchungaji na ruzuku ya maneno Yake; watu wote wanaishi katika ulimwengu wa maneno ya Mungu, katikati ya laana na baraka za maneno ya Mungu, na idadi kubwa ya watu wanaishi chini ya hukumu na kuadibu kwa maneno Yake. Maneno haya na kazi hii vyote ni kwa ajili ya wokovu wa mwanadamu, kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu, na kwa ajili ya kubadilisha mwonekano wa asili wa dunia ya uumbaji wa zamani. Mungu aliiumba dunia kutumia maneno, Anawaongoza watu wote ulimwenguni kutumia maneno, Anawashinda na kuwaokoa kutumia maneno, na hatimaye Atatumia maneno kuhitimisha dunia ya zamani nzima, na hivyo kukamilisha mpango Wake mzima wa usimamizi. Katika Enzi nzima ya Ufalme, Mungu anatumia maneno kufanya kazi Yake, na kufanikisha matokeo ya kazi Yake. Hafanyi maajabu au kutenda miujiza, bali anafanya tu kazi Yake kupitia maneno. Kwa sababu ya maneno haya, watu wote wanalishwa na wanaruzukiwa, na wanapata maarifa na uzoefu wa kweli. Katika Enzi ya Neno, mwanadamu amebarikiwa kwa namna ya kipekee. Hateseki kwa maumivu ya mwili na anafurahia tu ruzuku tele ya maneno ya Mungu; bila kuhitaji kwenda kutafuta kwa upofu au kukimbia huku na kule, kutoka katikati ya utulivu wake, anaona kuonekana kwa Mungu, anamsikia Akizungumza kwa kinywa Chake mwenyewe, anapokea kile Anachoruzuku, na anamwona Yeye binafsi akifanya kazi Yake. Haya ni mambo ambayo watu wa enzi zilizopita hawakuweza kufurahia, na ni baraka ambazo hawangeweza kamwe kupokea.
Mungu ameazimia kumfanya mwanadamu kuwa kamili, na bila kujali Anazungumza kutoka katika mtazamo upi, yote ni kwa ajili ya kuwakamilisha watu. Maneno yanayozungumzwa kutoka katika mtazamo wa Roho ni magumu kwa watu kuelewa; hawana namna ya kupata njia ya utendaji, kwa kuwa uwezo wao wa kufahamu una mipaka. Kazi ya Mungu hutimiza matokeo tofauti, na katika kuchukua kila hatua ya kazi Yeye ana kusudi Lake. Zaidi ya hayo, ni lazima Azungumze kutoka katika mitazamo tofauti, kwa kuwa ni kwa kufanya hivyo tu ndiyo Anaweza kumkamilisha mwanadamu. Kama Angenena tu kutoka katika mtazamo wa Roho, hakungekuwa na njia ya kukamilisha hatua hii ya kazi ya Mungu. Kutokana na namna ya tabia ya sauti ambayo kwayo Anazungumza, unaweza kuona kwamba Ameazimia kulifanya kundi hili la watu kuwa kamili. Basi, hatua ya kwanza inapaswa kuwa ipi kwa kila mmoja wa wale wanaotaka kufanywa wakamilifu? Zaidi ya yote, ni lazima uijue kazi ya Mungu. Leo, mbinu mpya imeanza katika kazi ya Mungu; enzi imebadilika, namna ambavyo Mungu anafanya kazi pia imebadilika, na njia ambayo kwayo Mungu anazungumza ni tofauti. Leo, si tu kwamba mbinu ya kazi Yake imebadilika, bali pia enzi imebadilika. Sasa ni Enzi ya Ufalme. Pia ni enzi ya kumpenda Mungu. Ni limbuko la Enzi ya Ufalme wa Milenia; Enzi ya Ufalme wa Milenia pia ndiyo Enzi ya Neno, ambayo ndani yake Mungu anatumia namna nyingi za kunena ili kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na Anazungumza kutoka katika mitazamo tofauti ili kumruzuku mwanadamu. Baada ya kuingia katika Enzi ya Ufalme wa Milenia, Mungu anaanza kutumia maneno kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, akimruhusu mwanadamu aingie katika uhalisi wa maisha na kumwongoza kwenye njia sahihi. Akiwa amepitia hatua nyingi sana za kazi ya Mungu, mwanadamu ameona kwamba kazi ya Mungu haibaki bila kubadilika, bali inabadilika na kuzidi kuwa ya kina bila kukoma. Watu wameipitia kwa muda mrefu sana, wakati ambao kazi hiyo imebadilika tena na tena, imesonga tena na tena. Hata ibadilike kiasi gani, haikengeuki kamwe kutoka kwa kusudi la Mungu la kuwaletea wanadamu wokovu. Hata kupitia mabadiliko elfu kumi, kamwe haiendi kando na kusudi lake la asili. Bila kujali jinsi mbinu ya kazi ya Mungu inavyoweza kubadilika, kazi hii haiondoki kamwe kutoka kwa ukweli au na uzima. Mabadiliko katika mbinu ambayo kwayo kazi inafanywa yanahusisha tu mabadiliko katika muundo wa kazi, na mtazamo ambao Mungu anazungumza kutoka; hakuna mabadiliko katika lengo kuu la kazi ya Mungu. Mabadiliko katika namna ya tabia ya sauti ya Mungu na mbinu ya kazi Yake yanafanywa ili kufikia matokeo. Mabadiliko katika namna ya tabia ya sauti hayamaanishi mabadiliko katika kusudi au kanuni ya kazi hiyo. Kumwamini Mungu kwa kiasi kikukubwa kunamaanisha kufuatilia uzima; ikiwa unamwamini Mungu lakini hufuatilii uzima, ukweli, au maarifa ya Mungu, basi hii si imani katika Mungu! Na, je, ni jambo halisi bado kufuatilia kuingia katika ufalme ili kuwa mfalme? Kufikia upendo wa kweli kwa Mungu kupitia kufuatilia uzima—huu pekee ndio uhalisi; ufuatiliaji na utendaji wa ukweli—yote haya ni uhalisi. Kwa kusoma maneno ya Mungu, na wakati huo huo kupitia maneno haya, utakuja kushika maarifa ya Mungu katikati ya upitiaji halisi, na huu ni ufuatiliaji wa kweli.
Sasa ni Enzi ya Ufalme. Kuingia katika enzi hii mpya kunategemea iwapo umeingia katika uhalisi wa maneno ya Mungu, na iwapo maneno Yake yamekuwa uhalisi wa maisha yako. Maneno ya Mungu yanamwonekania kila mtu ili kwamba, mwishowe, watu wote wataishi katika ulimwengu wa maneno ya Mungu, na maneno Yake yamtie nuru na kumwangaza kila mtu kutoka ndani. Ikiwa, katika wakati huu, unakuwa asiye mwangalifu katika kusoma maneno ya Mungu, na huna hamu na maneno Yake, basi hili linaonyesha kwamba hali yako si sahihi. Ikiwa huwezi kuingia katika Enzi ya Neno, basi Roho Mtakatifu hatafanya kazi ndani yako; ikiwa umeingia katika enzi hii, Atafanya kazi Yake. Unaweza kufanya nini mwanzoni mwa Enzi ya Neno ili upate kazi ya Roho Mtakatifu? Katika enzi hii, na kati yenu, Mungu atatimiza ukweli ufuatao: kwamba kila mtu ataishi kwa kudhihirisha maneno ya Mungu, ataweza kuutia ukweli katika vitendo, na atampenda Mungu kwa moyo wake; kwamba watu wote watayatumia maneno ya Mungu kama msingi wao na kama uhalisi wao, na watakuwa na mioyo inayomcha Mungu; na kwamba, kupitia kutenda maneno ya Mungu, mwanadamu atatawala pamoja na Mungu. Hii ndiyo kazi itakayotimizwa na Mungu. Je, unaweza kushinda bila kusoma maneno ya Mungu? Leo, kuna wengi wanaohisi kwamba hawawezi kushinda hata siku moja au mbili bila kusoma maneno Yake. Lazima wasome maneno Yake kila siku, na ikiwa muda hauruhusu, kuyasikiliza kunatosha. Hii ndiyo hisia ambayo Roho Mtakatifu huwapa watu, na ndivyo Anavyoanza kuwagusa. Yaani, Anawadhibiti watu kupitia maneno, ili waweze kuingia katika uhalisi wa maneno ya Mungu. Ikiwa, baada ya siku moja tu bila kula na kunywa maneno ya Mungu, unahisi giza na kiu, na unashindwa kuvumilia, hili linaonyesha kwamba umeguswa na Roho Mtakatifu, na kwamba Yeye hajakuacha. Basi, wewe ni mtu aliye katika mkondo huu. Hata hivyo, ikiwa baada ya siku moja au mbili bila kula na kunywa maneno ya Mungu, wewe huhisi chochote, ikiwa huna kiu, na huguswi hata kidogo, hili linaonyesha kwamba Roho Mtakatifu amekupa kisogo. Hili linamaanisha, basi, kwamba kuna kitu kisicho sahihi na hali iliyo ndani yako; hujaingia katika Enzi ya Neno, na wewe ni mmoja wa wale waliobaki nyuma. Mungu hutumia maneno kuwadhibiti watu; unahisi vizuri ikiwa unakula na kunywa maneno ya Mungu, na ikiwa hufanyi hivyo, huna njia ya kufuata. Maneno ya Mungu yanakuwa chakula cha watu, na nguvu inayowasukuma. Biblia inasema kwamba “Mwanadamu hataishi kwa mkate pekee, lakini kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Mungu” (Mathayo 4:4). Leo, Mungu ataikamilisha kazi hii, na Atatimiza ukweli huu ndani yenu. Inakuwaje kwamba zamani, watu waliweza kushinda siku nyingi bila kusoma maneno ya Mungu na bado waliweza kula na kufanya kazi kama kawaida, lakini hivyo sivyo ilivyo leo? Katika enzi hii, Mungu hasa hutumia maneno kudhibiti vyote. Mwanadamu anahukumiwa na kukamilishwa kupitia katika maneno ya Mungu, na kisha hatimaye kupelekwa katika ufalme kwa maneno haya. Maneno ya Mungu tu ndiyo yanayoweza kuukimu uzima wa mwanadamu, na ni maneno ya Mungu tu yanayoweza kumpa mwanadamu mwangaza na njia ya kutenda, hasa katika Enzi ya Ufalme. Alimradi hupotoki kutoka katika uhalisi wa maneno ya Mungu, ukila na kunywa maneno Yake kila siku, Mungu atakukamilisha.
Kufuatilia uzima si jambo linaloweza kuharakishwa; ukuaji wa uzima haufanyiki kwa siku moja au mbili tu. Kazi ya Mungu ni ya kawaida na ya vitendo, na kuna mchakato ambao lazima ipitie. Ilimchukua Yesu mwenye mwili miaka thelathini na tatu na nusu kukamilisha kazi Yake ya kusulubiwa—basi vipi kuhusu kumtakasa mwanadamu na kubadilisha maisha yake, kazi iliyo ngumu kabisa? Si kazi rahisi kumfanya mtu wa kawaida anayemdhihirisha Mungu. Hili ni kweli hasa kwa watu waliozaliwa katika nchi ya joka kuu jekundu, ambao wana ubora duni wa tabia na wanahitaji kipindi kirefu cha maneno na kazi ya Mungu. Kwa hivyo usiwe na haraka ya kuona matokeo. Ni lazima uchukue hatua katika kula na kunywa maneno ya Mungu, na utie bidii zaidi katika maneno ya Mungu. Unapomaliza kusoma maneno Yake, lazima uweze kuyatia katika vitendo halisi, ukue katika maarifa, umaizi, utambuzi, na hekima katika maneno ya Mungu. Kupitia hili, utabadilika bila kutambua. Ikiwa unaweza kufanya kula na kunywa maneno ya Mungu, kuyasoma, kuyajua, kuyapitia, na kuyatenda kuwa kanuni yako, utafikia ukomavu bila kutambua. Kuna wale wanaosema kwamba hawawezi kutia maneno ya Mungu katika vitendo hata baada ya kuyasoma. Haraka yako ni ya nini? Unapofikia kimo fulani, utaweza kutia maneno Yake katika vitendo. Je, mtoto wa miaka minne au mitano anaweza kusema kwamba hawezi kuwategemeza au kuwaheshimu wazazi wake? Unapaswa kujua kimo chako cha sasa ni kikubwa kiasi gani. Tia katika vitendo kile unachoweza kutia katika vitendo, na uepuke kuwa mtu anayevuruga usimamizi wa Mungu. Kula na kunywa tu maneno ya Mungu, na ufanye hilo kuwa kanuni yako kuanzia sasa. Usiwe na wasiwasi, kwa wakati huu, kuhusu iwapo Mungu anaweza kukufanya uwe kamili. Usichunguze hilo kwa kina bado. Chukua tu maneno ya Mungu na uyale na uyanywe, na hakika Mungu atakufanya uwe kamili. Hata hivyo, kuna kanuni ambayo kwayo lazima ule na unywe maneno Yake. Usifanye hivyo kwa upofu. Katika kula na kunywa maneno ya Mungu, kwa upande mmoja, tafuta maneno unayopaswa kuyajua—yale yanayohusiana na maono—na kwa upande mwingine, tafuta kile unachopaswa kutia katika vitendo halisi—kile unachopaswa kukiingia. Kipengele kimoja kinahusiana na maarifa, na kingine na kuingia. Punde tu unapovielewa vyote viwili—unapoelewa kile unachopaswa kujua na kile unachopaswa kutenda—utajua jinsi ya kula na kunywa maneno ya Mungu.
Kuanzia sasa, kuzungumzia maneno ya Mungu kunapaswa kuwa kanuni ambayo kwayo unazungumza. Kwa kawaida, mnapokutana pamoja, mnapaswa kuingia katika ushirika kuhusu maneno ya Mungu, mkiyafanya maneno ya Mungu kuwa maudhui ya ushirika wenu, mkizungumzia kile mnachojua kuhusu maneno haya, jinsi mnavyoyaweka katika vitendo, na jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi. Mradi tu unafanya ushirika kuhusu maneno ya Mungu, Roho Mtakatifu atakuangaza. Kufikia ulimwengu wa maneno ya Mungu kunahitaji ushirikiano wa mwanadamu. Usipoingia katika hili, Mungu hatakuwa na njia ya kufanya kazi; ukifunga mdomo wako na usizungumzie maneno Yake, Yeye hatakuwa na njia ya kukuangaza. Wakati wowote ambapo huna shughuli nyingine, zungumzia maneno ya Mungu, na usijihusishe katika kupiga porojo! Acha maisha yako yajazwe na maneno ya Mungu—hapo tu ndipo utakuwa muumini mwenye kumcha Mungu. Haijalishi ikiwa ushirika wako ni wa juu juu. Bila ujuujuu hakuwezi kuwa na kina. Lazima kuwe na mchakato. Kupitia mafunzo yako, utaelewa mwangaza wa Roho Mtakatifu juu yako, na jinsi ya kula na kunywa maneno ya Mungu kwa ufanisi. Baada ya muda wa kuchunguza, utaingia katika uhalisi wa maneno ya Mungu. Ni pindi tu ukiwa na dhamira ya kushirikiana ndipo utaweza kupokea kazi ya Roho Mtakatifu.
Kanuni ya kula na kunywa maneno ya Mungu ina vipengele viwili: kimoja kinahusiana na maarifa, na kingine kinahusiana na kuingia. Ni maneno yapi unayopaswa kuja kuyajua? Unapaswa kuja kuyajua maneno yanayohusiana na maono (kama vile, yale yanayohusiana na ni enzi ipi ambayo kazi ya Mungu imeingia katika sasa, kile ambacho Mungu anataka kutimiza sasa, kupata mwili ni nini, na kadhalika; haya yote yanahusiana na maono). Maana ya njia ambayo mwanadamu anapaswa kuingia katika ni ipi? Hili linarejelea maneno ya Mungu ambayo mwanadamu anapaswa kuyatenda na kuingia ndani. Yaliyo hapo juu ni vipengele viwili vya kula na kunywa maneno ya Mungu. Kuanzia sasa, ule na unywe maneno ya Mungu kwa namna hii. Ikiwa una ufahamu wazi wa maneno Yake kuhusu maono, basi hakuna haja ya kuendelea kusoma wakati wote. Jambo lenye umuhimu wa msingi ni kula na kunywa maneno zaidi yanayohusu kuingia, kama vile jinsi ya kuugeuza moyo wako kumwelekea Mungu, jinsi ya kutuliza moyo wako mbele za Mungu, na jinsi ya kuasi dhidi ya mwili. Haya ndiyo mambo unayopaswa kutia katika vitendo. Bila kujua jinsi ya kula na kunywa maneno ya Mungu, ushirika wa kweli hauwezekani. Punde tu unapojua jinsi ya kula na kunywa maneno Yake, wakati ambapo umefahamu kile ambacho ni muhimu, ushirika utakuwa huru, na haijalishi suala linaloibuliwa, utaweza kushiriki na kufahamu uhalisi. Ikiwa, unapokuwa unashiriki kuhusu maneno ya Mungu, huna uhalisi, basi hujafahamu kile ambacho ni muhimu, jambo ambalo linaonyesha kwamba hujui jinsi ya kula na kunywa maneno ya Mungu. Watu wengine wanaweza kuona kusoma maneno ya Mungu kuwa jambo la kuchosha, jambo ambalo si hali ya kawaida. Kilicho cha kawaida ni kutochoka kamwe kusoma maneno ya Mungu, kuwa na kiu nayo daima, na kuona maneno ya Mungu kuwa mazuri daima. Hivi ndivyo mtu aliye na kuingia halisi anavyokula na kunywa maneno ya Mungu. Unapohisi kwamba maneno ya Mungu ni ya vitendo mno na ndiyo hasa ambayo mwanadamu anapaswa kuyaingia; unapohisi kwamba maneno Yake ni ya msaada na ya manufaa makubwa kwa mwanadamu, na kwamba ni ruzuku ya uzima wa mwanadamu—ni Roho Mtakatifu anayekupa hisia hii, na ni Roho Mtakatifu anayekugusa. Hili linathibitisha kwamba Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yako na kwamba Mungu hajakupa kisogo. Watu wengine, wanapoona kwamba Mungu ananena daima, wanachoshwa na maneno Yake, na kufikiri si muhimu iwapo wanayasoma au la—jambo ambalo si hali ya kawaida. Wanakosa moyo ulio na kiu ya kuingia katika uhalisi, na watu kama hao hawana shauku wala hawatilii maanani kufanywa kuwa watimilifu. Wakati wowote unapogundua kwamba huna kiu ya maneno ya Mungu, hili linaonyesha kwamba hauko katika hali ya kawaida. Zamani, iwapo Mungu alikuwa amekupa kisogo kungeweza kupimwa na iwapo ulikuwa na amani ndani yako, na iwapo ulipata furaha. Sasa jambo muhimu ni iwapo una kiu ya maneno ya Mungu, iwapo maneno Yake ni uhalisi wako, iwapo wewe ni mwaminifu, na iwapo unaweza kufanya yote uwezayo kwa ajili ya Mungu. Yaani, mwanadamu hupimwa kulingana na uhalisi wa maneno ya Mungu. Mungu anayaelekeza maneno Yake kwa binadamu wote. Ikiwa uko tayari kuyasoma, Yeye atakutia nuru, lakini ikiwa hauko tayari, Hatakutia nuru. Mungu huwatia nuru wale wenye njaa na kiu ya haki, na Yeye huwatia nuru wale wanaomtafuta. Wengine wanasema kwamba Mungu hakuwatia nuru hata baada ya wao kusoma maneno Yake. Lakini uliyasoma maneno haya kwa namna gani? Ikiwa ulisoma maneno Yake kwa namna ja kiijuujuu tu, na hukutilia maanani uhalisi, Mungu angewezaje kukutia nuru? Mtu asiyethamini maneno ya Mungu anawezaje kufanywa kuwa mtimilifu na Yeye? Ikiwa huthamini maneno ya Mungu, basi hutakuwa na ukweli wala uhalisi. Ikiwa unathamini maneno Yake, basi utaweza kutia ukweli katika vitendo, na hapo tu ndipo utakuwa na uhalisi. Hii ndiyo sababu lazima ule na unywe maneno ya Mungu nyakati zote, uwe una shughuli nyingi au la, mazingira yawe mabaya au la, na uwe unajaribiwa au la. Kwa ujumla, maneno ya Mungu ni msingi wa uwepo wa mwanadamu. Hakuna mtu anayepaswa kuyaacha maneno Yake, bali lazima ale maneno Yake kama anavyokula milo mitatu kwa siku. Je, kufanywa kuwa mtimilifu na kupatwa na Mungu kunaweza kuwa rahisi hivyo? Uwe unaelewa kwa sasa au la, na uwe una umaizi katika kazi ya Mungu au la, lazima ule na unywe zaidi maneno ya Mungu. Huku ni kuingia kwa namna ya kuchukua hatua. Baada ya kusoma maneno ya Mungu, ufanye haraka kutia katika vitendo kile unachoweza kukiingia, na uweke kando kwa sasa kile usichoweza. Kunaweza kuwa na maneno mengi ya Mungu ambayo huwezi kuyaelewa mwanzoni, lakini baada ya miezi miwili au mitatu, pengine hata mwaka mmoja, utayaelewa. Hili linawezekanaje? Ni kwa sababu Mungu hawezi kuwafanya watu kuwa watimilifu kwa siku moja au mbili. Wakati mwingi, unaposoma maneno Yake, hutaelewa mara moja. Wakati huo, haijalishi unayasoma namna gani, yataonekana kama maandishi matupu tu; lazima uyapitie kwa muda kabla ya kuweza kuyaelewa. Kwa kuwa Mungu amenena mengi sana, unapaswa kufanya kila uwezalo kula na kunywa maneno Yake, na kisha, bila wewe kutambua, utakuja kuelewa, na bila wewe kutambua, Roho Mtakatifu atakutia nuru. Roho Mtakatifu anapomtia nuru mwanadamu, mara nyingi ni bila mwanadamu kutambua. Yeye hukutia nuru na kukuongoza unapokuwa na kiu na kutafuta. Kanuni ya kazi ya Roho Mtakatifu ni kwamba ina kitovu katika maneno ya Mungu unayokula na kunywa. Wale wote wasiotilia maanani maneno ya Mungu na daima wana mtazamo tofauti kuelekea maneno Yake—wakiamini, katika fikira zao zilizovurugika, kwamba si muhimu iwapo wanayasoma maneno Yake au la—ni wale ambao hawana uhalisi. Kazi ya Roho Mtakatifu wala nuru Yake haiwezi kuonekana ndani ya mtu kama huyo. Watu kama hawa ni wadoezi, na ni watu wanaojifanya wasio na sifa za kweli, kama Bwana Nanguo wa mfano ule.
Bila maneno ya Mungu kama uhalisi wako, huna kimo halisi. Wakati wa kujaribiwa utakapofika, hakika utaanguka, na kisha kimo chako cha kweli kitafunuliwa. Lakini wale ambao hutafuta mara kwa mara kuingia katika uhalisi, wanapokabiliwa na majaribu, wanakuja kuelewa kusudi la kazi ya Mungu, na kwamba mtu yeyote aliye na dhamiri na aliye na kiu ya Mungu anapaswa kuchukua hatua ya vitendo kumlipa Mungu kwa upendo Wake. Wale ambao hawana uhalisi hawawezi kusimama imara hata wanapokabiliwa na mambo madogo. Hiyo ndiyo tofauti kati ya wale walio na kimo halisi na wale wasio nacho. Kwa nini inakuwa kwamba, ingawa wote wanakula na kunywa maneno ya Mungu, wengine wanaweza kusimama imara katikati ya majaribu, huku wengine wakikimbia? Tofauti dhahiri ni kwamba wengine wanakosa kimo halisi; hawana maneno ya Mungu ya kutumika kama uhalisi wao, na maneno Yake hayajakita mizizi ndani yao. Punde tu wanapojaribiwa, wanakosa njia. Basi, kwa nini wengine wanaweza kusimama imara katikati ya majaribu? Ni kwa sababu wanaelewa ukweli na wana maono, na wanaelewa nia za Mungu na matakwa Yake, na hivyo wanaweza kusimama imara katika majaribu. Hiki ni kimo halisi, na huu, pia, ni uzima. Wengine wanaweza pia kusoma maneno ya Mungu, lakini hawayatii katika vitendo, hawayachukulii kwa uzito; wale ambao hawayachukulii kwa uzito hawatilii maanani utendaji. Wale ambao hawana maneno ya Mungu ya kutumika kama uhalisi wao hawana kimo halisi, na watu kama hao hawawezi kusimama imara katika majaribu.
Maneno ya Mungu yanaponenwa, unapaswa kuyapokea mara moja, na kuyala na kuyanywa. Haijalishi unaelewa kiasi gani, mtazamo mmoja ambao lazima ushikilie sana ni kula na kunywa, kuyajua, na kuyatenda maneno Yake. Hili ni jambo ambalo unapaswa kuweza kufanya. Usijali kamwe kuhusu jinsi kimo chako kinaweza kuwa kikubwa; zingatia tu kula na kunywa maneno Yake. Hili ndilo jambo ambalo mwanadamu anapaswa kuwa na ushirikiano kulihusu. Katika maisha yako ya kiroho, unapaswa hasa kujaribu kuingia katika uhalisi wa kula na kunywa maneno ya Mungu na kuyatia katika vitendo. Si kazi yako kuzingatia kitu kingine chochote. Wale wanaoongoza kanisa wanapaswa kuweza kuwaongoza akina ndugu wao wote ili wajue jinsi ya kula na kunywa maneno ya Mungu. Hili ni jukumu la kila mtu anayeongoza kanisa. Wawe vijana au wazee, wote wanapaswa kuchukulia kula na kunywa maneno ya Mungu kuwa jambo lenye umuhimu mkubwa na wanapaswa kuwa na maneno Yake mioyoni mwao. Kuingia katika uhalisi huu kunamaanisha kuingia katika Enzi ya Ufalme. Leo, watu wengi wanahisi kwamba hawawezi kuishi bila kula na kunywa maneno ya Mungu, na wanahisi kwamba maneno Yake ni mapya bila kujali wakati. Hili linamaanisha kwamba wanaanza kuitembea njia sahihi. Mungu hutumia maneno kufanya kazi Yake na kumruzuku mwanadamu. Kila mtu anapoyatamani na kuwa na kiu ya maneno ya Mungu, watu wataingia katika dunia wa maneno Yake.
Mungu amenena maneno mengi sana. Umekuja kujua kiasi gani? Umeingia kiasi gani? Ikiwa wale wanaoongoza kanisa hawajawaongoza akina ndugu wao katika uhalisi wa maneno ya Mungu, basi watakuwa wamezembea katika jukumu lao, na watakuwa wameshindwa kutimiza majukumu yao! Iwe ufahamu wako ni wa kina au wa kijuujuu, bila kujali kiwango cha ufahamu wako, lazima ujue jinsi ya kula na kunywa maneno Yake, lazima utilie maanani sana maneno Yake, na uelewe umuhimu na lazima ya kuyala na kuyanywa. Kwa kuwa Mungu amenena mengi sana, ikiwa huli wala hunywi maneno Yake, au kuyafuatilia, au kuyatia katika vitendo, huku hakuwezi kuitwa kumwamini Mungu. Kwa kuwa unamwamini Mungu, basi lazima ule na unywe maneno Yake, upitie maneno Yake, na uishi kwa kudhihirisha maneno Yake. Huku pekee ndiko kunaweza kuitwa imani katika Mungu! Ukisema unamwamini Mungu kwa kinywa chako na bado huwezi kutia neno Lake lolote katika vitendo au kuleta uhalisi wowote, huku hakuitwi kumwamini Mungu. Badala yake, ni "kutafuta kula mikate mpaka ushibe." Kuzungumza tu kuhusu shuhuda ndogondogo, mambo yasiyo na maana, na mambo ya kijuujuu, bila kuwa na hata chembe ndogo ya uhalisi: haya hayahesabiwi kama imani katika Mungu, na hujafahamu kabisa njia sahihi ya kumwamini Mungu. Kwa nini lazima ule na unywe maneno ya Mungu zaidi? Ikiwa huli wala hunywi maneno Yake bali unatafuta tu kwenda mbinguni, je, huko ni kumwamini Mungu? Hatua ya kwanza ambayo mtu anayemwamini Mungu anapaswa kuchukua ni ipi? Ni kwa njia ipi ndiyo Mungu humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu? Je, unaweza kufanywa kuwa mtimilifu bila kula na kunywa maneno ya Mungu? Je, unaweza kuchukuliwa kuwa mtu wa ufalme bila maneno ya Mungu kutumika kama uhalisi wako? Je, imani katika Mungu inahusu nini hasa? Waumini katika Mungu wanapaswa, angalau, kuwa na tabia nzuri kwa nje; jambo la muhimu kabisa zaidi ya yote ni kuwa na maneno ya Mungu. Haijalishi chochote, huwezi kamwe kuyaacha maneno Yake. Kumjua Mungu na kuridhisha nia Zake yote yanafanikishwa kupitia maneno Yake. Katika siku za usoni, kila taifa, dhehebu, dini, na sekta itashindwa kupitia maneno ya Mungu. Mungu atanena moja kwa moja, na watu wote watashika maneno ya Mungu mikononi mwao, na kwa njia hii watafanywa kuwa watimilifu. Ndani na nje, maneno ya Mungu yanaenea kote: Kila mtu atazungumza maneno ya Mungu kwa kinywa chake, atatenda kulingana na maneno ya Mungu, na ataweka maneno ya Mungu ndani yake, akibaki ameingia katika maneno ya Mungu ndani na nje. Kwa njia hii, watafanywa kuwa watimilifu. Wale wanaoridhisha nia za Mungu na kuweza kuwa na ushahidi Kwake ndio wale walio na maneno ya Mungu kama uhalisi wao.
Kuingia katika Enzi ya Neno—Enzi ya Ufalme wa Milenia—ndiyo kazi inayotimizwa leo. Kuanzia sasa, jizoeze kufanya ushirika kuhusu maneno ya Mungu. Ni kwa njia ya kula na kunywa pamoja na kupitia maneno ya Mungu pekee ndiyo utaweza kuishi kwa kudhihirisha maneno ya Mungu. Lazima uonyeshe uzoefu fulani wa vitendo ili kuwasadikisha wengine. Ikiwa huwezi kuishi kwa kudhihirisha uhalisi wa maneno ya Mungu, hakuna mtu atakayeshawishika! Wale wote wanaotumiwa na Mungu wanaweza kuishi kwa kudhihirisha uhalisi wa maneno ya Mungu. Ikiwa huwezi kuleta uhalisi huu ili kuwa na ushuhuda kwa Mungu, hili linaonyesha kwamba Roho Mtakatifu hajafanya kazi ndani yako, na kwamba hujafanywa kuwa mtimilifu. Huu ndio umuhimu wa maneno ya Mungu. Je, una moyo ulio na kiu ya maneno ya Mungu? Wale walio na kiu ya maneno ya Mungu wana kiu ya ukweli, na ni watu kama hawa pekee ndio wanaobarikiwa na Mungu. Katika siku za usoni, Mungu atanena maneno zaidi kwa dini zote na madhehebu yote. Yeye kwanza ananena na kutamka sauti Yake miongoni mwenu ili kuwafanya ninyi kuwa kamili kabla ya kuendelea kunena na kutamka sauti Yake miongoni mwa watu wa mataifa ili kuwashinda. Kupitia maneno Yake, wote watasadikishwa kwa dhati na kikamilifu. Kupitia maneno ya Mungu na ufichuzi Wake, tabia potovu ya mwanadamu inapungua, anapata mfano wa binadamu, na tabia yake ya uasi inapungua. Maneno yanafanya kazi juu ya mwanadamu kwa mamlaka na yanamshinda mwanadamu ndani ya nuru ya Mungu. Kazi anayofanya Mungu katika enzi ya wakati wa sasa, na vilevile mabadiliko muhimu ya kazi Yake, yote yanaweza kupatikana ndani ya maneno Yake. Usipoyasoma maneno Yake, hutaelewa chochote. Kupitia kula na kunywa kwako mwenyewe maneno Yake, na kupitia kushiriki na akina ndugu wako na upitiaji wako halisi, utapata maarifa kamili ya maneno ya Mungu. Ni hapo tu ndipo utaweza kuishi kwa kudhihirisha uhalisi wake kwa kweli.