Kuhusu Majina na Utambulisho

Ikiwa unataka kufaa kwa ajili ya kutumiwa na Mungu, ni lazima uijue kazi ya Mungu; lazima ujue kazi Aliyofanya awali (katika Agano Jipya na la Kale), na, zaidi ya hayo, lazima uijue kazi Yake ya leo. Ambayo ni kusema, ni lazima uzitambue hatua tatu za kazi ya Mungu ya zaidi ya miaka 6,000. Ukiambiwa ueneze injili, basi hutaweza kufanya hivyo bila kuijua kazi ya Mungu. Mtu fulani anaweza kukuuliza kuhusu kile Mungu wako amesema kuhusu Biblia, Agano la Kale, na kazi na maneno ya Yesu ya wakati huo. Ikiwa huwezi kuzungumza juu ya hadithi ya ndani ya Biblia, basi hawatashawishika. Mwanzoni, Yesu alizungumza mengi kuhusu Agano la Kale na wanafunzi Wake. Kila kitu walichosoma kilitoka Agano la Kale; Agano Jipya liliandikwa tu miongo kadhaa baada ya kusulubiwa kwa Yesu. Ili kueneza injili, mnapaswa hasa kufahamu ukweli wa ndani wa Biblia, na kazi ya Mungu katika Israeli, hivyo ni kusema kazi Aliyoifanya Yehova. Na pia mnapaswa kuelewa kazi aliyoifanya Yesu. Haya ndiyo hasa maswala ambayo watu wote wana wasiwasi nayo, na hadithi ya ndani ya zile hatua mbili za kazi ndiyo hawajasikia. Wakati wa kueneza injili, kwanza weka kando majadiliano juu ya kazi ya Roho Mtakatifu ya leo. Hii hatua ya kazi ipo nje ya uwezo wao, kwa sababu mnachofuatilia ni kile ambacho kipo juu kuliko vyote: maarifa ya Mungu, na maarifa ya kazi ya Roho Mtakatifu, na hakuna kilichotukuka zaidi kuliko vitu hivi viwili. Ukizungumzia kwanza kuhusu kile ambacho ni cha juu, itakuwa ni kubwa mno kwao, kwani hakuna ambaye amepitia kazi kama hiyo ya Roho Mtakatifu; haina historia, na si rahisi kwa mwanadamu kuikubali. Uzoefu wao ni wa mambo ya kale kutoka zamani, pamoja na baadhi ya kazi za Roho Mtakatifu. Wanayopitia si kazi ya leo ya Roho Mtakatifu, ama mapenzi ya Mungu ya leo. Bado wanatenda kulingana na mazoea ya zamani bila mwanga mpya wala mambo mapya.

Katika enzi ya Yesu, Roho Mtakatifu hasa alifanya kazi Yake ndani ya Yesu, wakati wale waliomtumikia Yehova walikuwa wanavaa kanzu za kikuhani hekaluni wakifanya hivyo kwa uaminifu thabiti. Pia walikuwa na kazi ya Roho Mtakatifu, lakini hawakuweza kufahamu matakwa ya wakati huo ya Mungu, na walibaki tu kuwa waaminifu kwa Yehova kulingana na mazoea ya kale, bila uongozi mpya. Yesu alikuja na kuleta kazi mpya. Wale watu waliohudumu hekaluni hawakuwa na uongozi mpya wala hawakuwa na kazi mpya. Wakihudumu hekaluni wangeweza tu kushikilia mazoea ya kale; bila kuondoka hekaluni, hawangeweza kuwa na uingiaji mpya. Kazi mpya ililetwa na Yesu, na Yesu hakuingia hekaluni kufanya kazi Yake. Alifanya kazi yake nje ya hekalu pekee, kwani wigo wa kazi ya Mungu ulikuwa umebadilika kitambo sana. Hakufanya kazi ndani ya hekalu, na mwanadamu alipomtumikia Mungu hapo ingekuwa tu kuweka mambo kama yalivyokuwa, na haingeweza kuleta kazi yoyote mpya. Vivyo hivyo, watu wa kidini bado wanaabudu Biblia leo. Ukieneza injili kwao, watakurushia maelezo ya juujuu ya maneno ya Biblia na watapata ushahidi mwingi, wakikuacha umezubaa na usijue la kusema; kisha watawapachika jina na kuwaona kuwa wapumbavu katika imani yenu. Watasema, “Hujui hata Biblia, neno la Mungu, kwa hiyo unawezaje kusema kwamba unamwamini Mungu?” Kisha watakudharau, na pia watasema, “Kwa kuwa Yule mnayemwamini ni Mungu, kwa nini Hawaambii yote kuhusu Agano la Kale na Jipya? Kwa kuwa Ameleta utukufu Wake kutoka Israeli hadi upande wa Mashariki, kwa nini Hajui kazi iliyofanywa katika Israeli? Kwa nini Hajui kazi ya Yesu? Kama hamjui, basi inathibitisha kwamba hamjaelezwa; sababu Yeye ndiye kupata mwili kwa Yesu kwa mara ya pili, ingewezekanaje kuwa Hajui mambo haya? Yesu alijua kazi aliyoifanya Yehova; Anawezaje kukosa kuijua?” Wakati utakapofika, wote watakuuliza maswali kama haya. Vichwa vyao vimejaa mambo kama haya; watakosaje kuuliza? Wale walio katika mkondo huu hawazingatii Biblia, kwa vile mmeendelea kufahamu kazi ya hatua kwa hatua inayofanywa na Mungu leo, mmeshuhudia kazi hii ya hatua kwa hatua kwa macho yenu wenyewe, na mmeona kwa uwazi hatua tatu za kazi, kwa hivyo mmelazimika kuiweka chini Biblia na kukoma kuitafiti. Lakini hawawezi kuitafiti, kwa kuwa hawana ujuzi wa kazi hii ya hatua kwa hatua. Watu wengine watauliza, “Kuna tofauti gani kati ya kazi iliyofanywa na Mungu mwenye mwili na ile ya manabii na mitume wa zamani? Daudi pia aliitwa Bwana, sawa tu na Yesu alivyoitwa; ingawa kazi walizofanya zilikuwa tofauti, waliitwa kwa jina sawa. Kwa nini unasema, utambulisho wao haukuwa sawa? Kile Yohana alichoshuhudia ni maono, ambayo pia yalitoka kwa Roho Mtakatifu, na aliweza kuyasema maneno ambayo Roho Mtakatifu alikusudia kuyasema; kwa nini utambulisho wa Yohana ni tofauti na ule wa Yesu?” Maneno aliyoyasema Yesu yaliweza kumwakilisha Mungu kikamilifu, na kuwakilisha kikamilifu kazi ya Mungu. Kile alichokiona Yohana kilikuwa maono, na hakuweza kuwakilisha kikamilifu kazi ya Mungu. Ni kwa nini Yohana, Petro na Paulo walizungumza maneno mengi—kama alivyofanya Yesu—lakini bado hawakuwa na utambulisho sawa na Yesu? Ni hasa kwa sababu kazi waliyoifanya ilikuwa tofauti. Yesu alimwakilisha Roho wa Mungu, na Alikuwa Roho wa Mungu Akifanya kazi moja kwa moja. Alifanya kazi ya enzi mpya, kazi ambayo hakuna aliyekuwa amewahi kuifanya hapo awali. Yeye Alifungua njia mpya, Alimwakilisha Yehova, na Alimwakilisha Mungu Mwenyewe. Ilhali kwa Petro, Paulo na Daudi, bila kujali walichoitwa, waliwakilisha tu utambulisho wa kiumbe wa Mungu, na walitumwa na Yesu na Yehova. Kwa hivyo bila kujali kiasi cha kazi waliyofanya, bila kujali jinsi walivyofanya miujiza kubwa, walikuwa bado tu viumbe wa Mungu, na hawakuweza kumwakilisha Roho Mtakatifu. Walifanya kazi kwa jina la Mungu ama baada ya kutumwa na Mungu; zaidi ya hayo, walifanya kazi katika enzi iliyoanzishwa na Yesu ama Yehova, na kazi waliyoifanya haikuwa tofauti. Walikuwa, hatimaye, viumbe wa Mungu tu. Katika Agano la Kale, manabii wengi walizungumza utabiri, ama kuandika vitabu vya unabii. Hakuna aliyesema kuwa yeye ni Mungu, lakini punde tu Yesu Alipoanza kufanya kazi, Roho wa Mungu Alimshuhudia kuwa Yeye ni Mungu. Kwa nini ni hivyo? Kwa wakati huu, unapaswa kuwa unajua tayari! Awali, mitume na manabii waliandika nyaraka mbalimbali, na kufanya unabii mwingi. Baadaye, watu walichagua baadhi zao kuziweka katika Biblia, na baadhi zikapotea. Kwa vile kuna watu wanaosema kuwa vitu vyote wanavyozungumza vimetoka kwa Roho Mtakatifu, mbona baadhi yavyo vinachukuliwa kuwa nzuri, na baadhi yavyo vinachukuliwa kuwa vibaya? Na mbona baadhi vilichaguliwa, na sio vingine? Ikiwa kweli yalikuwa maneno Aliyoyasema Roho Mtakatifu, ingekuwa lazima kwa watu kuyachagua? Kwa nini maelezo ya maneno yaliyosemwa na Yesu na kazi Aliyoifanya ni tofauti katika kila moja ya Injili Nne? Je, hili si kosa la walioziandika? Baadhi ya watu watauliza, “Kwa kuwa nyaraka zilizoandikwa na Paulo na waandishi wengine wa Agano Jipya na kazi walizozifanya zilitokana kidogo na matakwa ya mwanadamu, na zilichanganywa na dhana za mwanadamu, basi, je, hakuna uchafu wa kibinadamu katika maneno ambayo Wewe (Mungu) unazungumza leo? Je, kweli hayana dhana hata moja za mwanadamu?” Hii hatua ya kazi aliyoifanya Mungu ni tofauti kabisa na zile walizozifanya Paulo na wengi wa mitume na manabii. Sio tu kwamba kuna tofauti na utambulisho, lakini, hasa, kuna tofauti kati ya kazi inayofanywa. Baada ya Paulo kupigwa chini na kuanguka mbele ya Bwana, aliongozwa na Roho Mtakatifu kufanya kazi, na akawa mtume. Na hivyo akaandikia makanisa nyaraka, na hizi nyaraka zote zilifuata mafundisho ya Yesu. Paulo alitumwa na Bwana kufanya kazi kwa jina la Bwana Yesu, lakini Mungu Mwenyewe alipokuja, Hakufanya kazi kwa jina lolote na Hakumwakilisha yeyote isipokuwa Roho wa Mungu katika kazi Yake. Mungu alikuja kufanya kazi Yake moja kwa moja: Hakukamilishwa na mwanadamu, na kazi Yake haikufanywa juu ya mafundisho ya mwanadamu yeyote. Katika hatua hii ya kazi Mungu haongozi kwa kuzungumza juu ya uzoefu Wake binafsi, bali Anafanya kazi Yake moja kwa moja, kulingana na kile Alicho nacho. Kwa mfano, jaribio la watoa huduma, nyakati za kuadibu, jaribio la kifo, nyakati za kumpenda Mungu…. Hii yote ni kazi ambayo haijawahi kufanywa mbeleni, na ni kazi ya enzi ya sasa, badala ya uzoefu wa binadamu. Katika maneno ambayo Nimezungumza, ni yapi ni uzoefu wa mwanadamu? Je, yote hayatoki moja kwa moja kwa Roho Mtakatifu, na hayatolewi nje na Roho Mtakatifu? Ni kwamba tu hali yako ni duni sana kiasi kwamba huwezi kuuona ukweli! Njia ya kivitendo ya maisha Ninayozungumzia ni ili kuongoza njia, na haijawahi kuzungumzwa na mtu yeyote hapo awali, wala hakuna mtu aliyewahi kupitia njia hii, au kujua uhalisi huu. Kabla Sijatamka maneno haya, hakuna mtu aliyewahi kuyazungumza. Hakuna mtu aliyewahi kuzungumza juu ya uzoefu kama huo, wala hakuna aliyewahi kusema maelezo hayo, na, zaidi ya hayo, hakuna aliyewahi kuonyesha hali kama hizo kufichua mambo haya. Hakuna aliyewahi kuongoza njia Ninayoongoza leo, na kama ingeongozwa na mwanadamu, basi isingekuwa njia mpya. Chukulia Paulo na Petro, kama mfano. Hawakuwa na uzoefu wao binafsi kabla ya Yesu kuongoza njia. Ilikuwa tu baada ya Yesu kuongoza njia ndipo walipopata uzoefu wa maneno aliyoyasema Yesu, na njia Aliyoiongoza; kutokana na hili walipata uzoefu mwingi, na wakaandika nyaraka. Kwa hivyo, uzoefu wa mwanadamu sio sawa na kazi Ya Mungu, na kazi ya Mungu sio sawa na maarifa yalivyoelezwa na dhana na uzoefu wa mwanadamu. Nimesema, tena na tena, kuwa leo Ninaongoza njia mpya, na kufanya kazi mpya, na kazi na matamshi Yangu ni tofauti na yale ya Yohana na wale manabii wengine wote. Kamwe, Sijawahi kupata uzoefu kwanza, na kisha kuzizungumzia kwenu—hivyo sivyo ilivyo hata kidogo. Kama ingekuwa hivyo, je, haingewachelewesha kitambo sana? Hapo awali, maarifa ambayo wengi waliyazungumzia yaliinuliwa pia, lakini maneno yao yote yalizungumzwa tu kulingana na wale wanaoitwa watu wa kiroho. Hayakuiongoza njia, lakini yalitoka kwenye uzoefu wao, yalitoka kwenye yale waliyoyaona, na kwenye maarifa yao. Mengine yalikuwa ni dhana zao, na mengine yalijumuisha uzoefu ambao walikuwa wamefanyia muhtasari. Leo, asili ya kazi Yangu ni tofauti kabisa na ya kwao. Sijawahi kupata uzoefu wa kuongozwa na wengine, wala Sijakubali kukamilishwa na wengine. Zaidi ya hayo, yote ambayo Nimezungumza na kushiriki ni tofauti na yale ya wengine, na hayajawahi kuzungumzwa na mwingine yeyote. Leo, bila kujali ninyi ni nani, kazi yenu inafanywa kulingana na maneno Nisemayo. Bila haya matamshi na kazi, nani angeweza kupata uzoefu wa mambo haya (jaribu la watendaji huduma, nyakati za kuadibu…), ni nani atakayeweza kuzungumzia maarifa kama haya? Je, kweli huna uwezo wa kuona haya? Bila kujali hatua ya kazi, mara tu maneno Yangu yasemwapo, mnaanza kushiriki kulingana na maneno Yangu, na kufanya kazi kulingana nayo, na sio njia ambayo yeyote kati yenu amefikiria. Baada ya kufika hapa, je, huna uwezo wa kuona swali la wazi na rahisi kama hili? Sio njia iliyofikiriwa na yeyote, wala haijalinganishwa na mtu yeyote wa kiroho. Ni njia mpya, na hata maneno mengi yaliyosemwa mara ya kwanza na Yesu hayatumiki tena. Ninachozungumza ni kazi ya kufungua enzi mpya, na ni kazi inayosimama peke yake; kazi Nifanyayo, na maneno Nizungumzayo, yote ni mapya. Si hii ndiyo kazi mpya ya leo? Kazi ya Yesu pia ilikuwa hivi. Kazi Yake pia ilikuwa tofauti na hizo za watu wengine hekaluni, na pia ilitofautiana na kazi za Mafarisayo, na wala haikufanana na zilizofanywa na watu wote wa Israeli. Baada ya kuishuhudia, watu walishindwa kuamua: “Kweli ilifanywa na Mungu?” Yesu hakuzingatia sheria ya Yehova; Alipokuja kumfunza mwanadamu, yote Aliyoyanena yalikuwa mapya na tofauti na yale yaliyosemwa na watakatifu wa zamani na manabii wa Agano la Kale, na kwa sababu hii, watu walisalia bila uhakika. Hii ndiyo humfanya mwanadamu kuwa mgumu sana kushughulika naye. Kabla ya kukubali hii hatua mpya ya kazi, njia ambayo wengi wenu walitembelea ilikuwa ya kutenda na kuingia katika msingi wa watu hao wa kiroho. Lakini leo, kazi Ninayoifanya ni tofauti sana, na hivyo hamna uwezo wa kuamua kama ni sawa ama sio. Sijali ni njia gani uliyoitembea hapo awali, wala Sijali ulikula “chakula” cha nani, au ni nani ulimchukulia kama “baba” yako. Kwa kuwa Nimekuja na kuleta kazi mpya ya kumwongoza mwanadamu, wote wanaonifuata lazima watende kulingana na Ninachosema. Bila kujali jinsi ulivyotoka “familia” yenye nguvu, lazima unifuate, hupaswi kutenda kulingana na mazoea yako ya awali, “Baba yako mlezi” anapaswa kushuka nawe unapaswa kuja mbele ya Mungu wako kupata mgao wako halali. Ninyi nyote mpo mikononi Mwangu, na hampaswi kutoa sana imani pofu kwa baba yenu mlezi; hawezi kukutawala kabisa. Kazi ya leo inasimama peke yake. Yote Ninayosema leo ni dhahiri kuwa hayatokani na msingi wa zamani; ni mwanzo mpya, na ukisema kuwa imeundwa kwa mkono wa mwanadamu, basi wewe ni kipofu kiasi kwamba huwezi kuokolewa!

Isaya, Ezekieli, Musa, Daudi, Ibrahimu na Danieli walikuwa viongozi ama manabii kati ya wateule wa Israeli. Mbona hawakuitwa Mungu? Mbona Roho Mtakatifu hakuwashuhudia? Mbona Roho Mtakatifu alimshuhudia Yesu punde tu Alipoanza kazi yake na kuanza kuzungumza maneno Yake? Na mbona Roho Mtakatifu hakuwashuhudia wengine? Wao, wanadamu waliokuwa na mwili, wote waliitwa “Bwana.” Bila kujali walivyoitwa, kazi zao zinawakilisha nafsi zao na kiini chao, na nafsi zao na kiini chao zinawakilisha utambulisho wao. Kiini chao hakina uhusiano na majina yao, inawakilishwa na waliyoonyesha, na waliyoishi kwa kudhihirisha. Katika Agano la Kale, hakukuwa na kitu kisicho cha kawaida katika kuitwa Bwana, na mtu angeweza kuitwa kwa njia yoyote ile, lakini kiini chake na utambulisho wake wa asili ulikuwa haubadiliki. Miongoni mwa wale makristo wa uwongo, manabii wa uwongo, na wapotoshaji, je, hakuna wanaoitwa “Mungu” pia? Na mbona hao sio Mungu? Kwa sababu hawana uwezo wa kufanya kazi ya Mungu. Kimsingi, wao ni wanadamu, wanaowadanganya watu, sio Mungu, na hivyo hawana utambulisho wa Mungu. Je, Daudi pia hakuitwa Bwana miongoni mwa makabila kumi na mawili? Yesu pia aliitwa Bwana: kwa nini ni Yesu pekee aliyeitwa Mungu mwenye mwili? Je, Yeremia pia hakujulikana kama Mwana wa Adamu? Na Yesu pia hakujulikana kama Mwana wa Adamu? Kwa nini Yesu alisulubishwa kwa niaba ya Mungu? Je, si kwa sababu kiini chake kilikuwa tofauti? Je, si kwa sababu kazi aliyoifanya ilikuwa tofauti? Je, jina lina umuhimu? Ingawa Yesu pia aliitwa Mwana wa Adamu, Alikuwa kupata mwili kwa Mungu kwa mara ya kwanza. Alikuwa amekuja kuchukua mamlaka, na kukamilisha kazi ya ukombozi. Hii inathibitisha kuwa utambulisho na kiini cha Yesu kilikuwa tofauti na kile cha wengine walioitwa pia Mwana wa Adamu. Leo, ni nani kati yenu anayethubutu kusema kwamba maneno yote yaliyotamkwa na wale waliotumiwa na Roho Mtakatifu yalitoka kwa Roho Mtakatifu? Kuna anayethubutu kusema mambo kama haya? Ikiwa unasema mambo kama haya, basi kwa nini kitabu cha unabii cha Ezra kiliondolewa, na kwa nini jambo hilo pia lilifanywa kwa vitabu vya wale watakatifu na manabii wa kale? Ikiwa zote zilitoka kwa Roho Mtakatifu, basi kwa nini mnathubutu kufanya maamuzi ambayo yanabadilika kama haya? Je, umehitimu kuchagua kazi ya Roho Mtakatifu? Hadithi nyingi kutoka Israeli pia zilitolewa. Na ukiamini kwamba maandishi haya yote ya kale yalitoka kwa Roho Mtakatifu, basi ni kwa nini baadhi ya vitabu vilitolewa? Kama yote yalitoka kwa Roho Mtakatifu, yote yanapaswa kuwekwa, na kutumwa kwa ndugu makanisani kuyasoma. Hayapaswi kuchaguliwa na kutolewa kwa matakwa ya mwanadamu; ni makosa kufanya hivyo. Kwa Kusema kwamba uzoefu wa Paulo na Yohana ulichanganywa na maarifa binafsi hakumaanishi kwamba uzoefu na maarifa yao yalitoka kwa Shetani, ila ni kwamba tu walikuwa na mambo yaliyotokana na uzoefu na maarifa yao binafsi. Maarifa yao yalilingana na asili ya uzoefu halisi kwa wakati huo, na ni nani anayeweza kusema kwa ujasiri kwamba yote yalitoka kwa Roho Mtakatifu? Kama Injili Nne zote zilitoka kwa Roho Mtakatifu, basi ilikuwaje kwamba Mathayo, Marko, Luka na Yohana kila mmoja alisema jambo tofauti kuhusu kazi ya Yesu? Msipoamini haya, basi angalia maelezo tofauti kwenye Biblia ya jinsi Petro alivyomkana Yesu mara tatu: Yote ni tofauti, na kila moja ina sifa yake yenyewe. Wengi walio wajinga husema, “Mungu mwenye mwili pia ni mwanadamu, kwa hivyo je maneno Anayoyazungumza yanaweza kutoka kikamilifu kwa Roho Mtakatifu? Kama maneno ya Paulo na Yohana yalichanganywa na matakwa ya mwanadamu, basi maneno Anayoyasema kweli hayajachanganywa na matakwa ya mwanadamu?” Watu wanaosema mambo kama haya ni vipofu na wajinga! Soma kwa makini Injili Nne; soma yale waliyoandika kuhusu mambo ambayo Yesu alifanya, na maneno Aliyozungumza. Kila maelezo ni tofauti kabisa, na kila moja ina mtazamo wake. Ikiwa kile kilichoandikwa na waandishi wa vitabu hivi vyote vilitoka kwa Roho Mtakatifu, basi vyote vinapaswa kuwa sawa na kulingana. Basi mbona kuna tofauti? Si mwanadamu ni mjinga sana, kutoweza kuona haya? Ukiulizwa kutoa ushuhuda kwa Mungu, ni ushuhuda upi unaoweza kutoa? Je, njia kama hiyo ya kumjua Mungu inaweza kutoa ushuhuda Kwake? Ikiwa wengine watakuuliza, “Kama rekodi za Yohana na Luka zilichanganywa na matakwa ya mwanadamu, basi maneno yanayosemwa na Mungu wenu hayajachanganywa na matakwa ya mwanadamu?” Je, utaweza kutoa jibu la wazi? Baada ya Luka na Mathayo kusikia maneno ya Yesu, na kuona kazi ya Yesu, walizungumza juu ya maarifa yao wenyewe, kwa jinsi walivyokumbuka wakieleza kwa kina baadhi ya ukweli wa kazi iliyofanywa na Yesu. Je, unaweza kusema kwamba maarifa yao yalifichuliwa kabisa na Roho Mtakatifu? Nje ya Biblia, kulikuwa na watu wengi wa kiroho wenye ujuzi wa juu kuliko wao, kwa hivyo kwa nini maneno yao hayakuchukuliwa na vizazi vya baadaye? Je, hawakutumiwa pia na Roho Mtakatifu? Jua kwamba katika kazi ya leo, Sizungumzi juu ya maarifa Yangu mwenyewe kulingana na msingi wa kazi ya Yesu, wala Sizungumzi juu ya maarifa Yangu dhidi ya usuli wa kazi ya Yesu. Ni kazi ipi Aliyofanya Yesu kwa wakati huo? Na ni kazi ipi Ninayofanya leo? Ninachofanya na kusema hakina historia. Njia Ninayotembea leo haijawahi kutembewa kabla, haikuwahi kutembewa na watu wa enzi na vizazi vya kale. Leo, imefunguliwa, na je, hii sio kazi ya Roho? Hata kama ilikuwa kazi ya Roho Mtakatifu, viongozi wote wa kale walifanya kazi zao juu ya msingi wa wengine. Hata hivyo, kazi ya Mungu Mwenyewe ni tofauti. Hatua ya kazi ya Yesu ilikuwa sawa: Aliifungua njia mpya. Alipokuja Alihubiri injili ya ufalme wa mbinguni, na kusema kwamba mwanadamu anapaswa kutubu na kukiri. Baada ya Yesu kukamilisha kazi yake, Petro na Paulo na wengineo walianza kuendeleza kazi ya Yesu. Baada ya Yesu kusulubishwa na kupaa mbinguni, walitumwa na Roho Mtakatifu kueneza njia ya msalaba. Ingawa maneno ya Paulo yaliinuliwa, pia yalilingana na msingi uliowekwa na kile ambacho Yesu alisema, kama vile uvumilivu, upendo, mateso, kufunika kichwa, ubatizo, ama mafundisho mengine yakufuatwa. Haya yote yalikuwa juu ya msingi wa maneno ya Yesu. Hawakuwa na uwezo wa kufungua njia mpya, kwani wote walikuwa wanadamu waliotumiwa na Mungu.

Matamshi na kazi ya Yesu kwa wakati huo hayakushikilia mafundisho, na hakufanya kazi Yake kulingana na kazi ya sheria ya Agano la Kale. Yalilingana na kazi iliyopaswa kufanywa kwa Enzi ya Neema. Alitenda kulingana na kazi Aliyokuwa ameleta mbele, kulingana na mipango Yake, na kulingana na huduma Yake; Hakufanya kazi kulingana na sheria ya Agano la Kale. Hakuna Alichofanya kilicholingana na Agano la Kale, na Hakuja kufanya kazi ili kutimiza maneno ya manabii. Kila hatua ya kazi ya Mungu haikuwa wazi ili kutimiza utabiri wa manabii wa zamani, na Hakuja kuyafuata mafundisho au kutimiza kwa makusudi utabiri wa manabii wa kale. Bado vitendo Vyake havikuvuruga utabiri wa manabii wa kale, wala havikuvuruga kazi Aliyokuwa amefanya awali. Jambo la muhimu katika kazi Yake halikuwa kufuata mafundisho yoyote, na badala yake kufanya kazi ambayo Yeye Mwenyewe alipaswa kufanya. Hakuwa nabii au mwonaji, bali mtendaji, ambaye kwa hakika Alikuja kufanya kazi Aliyopaswa kufanya, na Alikuja kufungua enzi Yake mpya na kufanya kazi Yake mpya. Bila shaka, Yesu alipokuja kufanya kazi Yake, pia Alitimiza maneno mengi yaliyosemwa na manabii wa zamani katika Agano la Kale. Hivyo pia kazi ya leo imetimiza utabiri wa manabii wa zamani wa Agano la Kale. Ni kwamba tu Sishikilii hiyo “kalenda ya zamani,” ni hivyo tu. Kwani kuna kazi zaidi ambayo ni lazima Niifanye, kuna maneno zaidi ambayo ni lazima Niyazungumze kwenu, na kazi hii na maneno haya yana umuhimu mkubwa zaidi kuliko kueleza vifungu kutoka kwenye Biblia, kwa sababu kazi kama hiyo haina umuhimu ama thamani kubwa kwenu, na haiwezi kuwasaidia, au kuwabadilisha. Ninakusudia kufanya kazi mpya sio kwa ajili ya kutimiza kifungu chochote kutoka kwenye Biblia. Ikiwa Mungu anakuja tu duniani ili kutimiza maneno ya manabii wa kale wa Biblia, basi ni nani aliye mkuu zaidi, je, ni Mungu mwenye mwili ama hao manabii wa zamani? Na hata hivyo, je, hao manabii ni wasimamizi wa Mungu, ama Mungu ndiye msimamizi wa manabii? Je, unaelezeaje maneno haya?

Mwanzoni, wakati Yesu alikuwa bado Hajaanza rasmi kufanya huduma Yake, kama wanafunzi waliomfuata, wakati mwingine Yeye pia alihudhuria mikutano, na Akaimba nyimbo, Akasifu, na kusoma Agano la Kale hekaluni. Baada ya Yeye kubatizwa na kuinuka, Roho alishuka rasmi juu Yake na kuanza kufanya kazi, Akifichua utambulisho Wake na huduma Aliyokuwa aifanye. Kabla ya haya, hakuna aliyejua utambulisho Wake, na mbali na Maria, hata Yohana hakujua. Yesu alikuwa na umri wa miaka 29 Alipobatizwa. Baada ya ubatizo wake kukamilika, mbingu zilifunguliwa, na sauti ikasema: “Huyu ni Mwana wangu Mpendwa, ambaye Ninapendezwa naye.” Mara baada ya Yesu kubatizwa, Roho Mtakatifu alianza kumshuhudia kwa njia hii. Kabla ya kubatizwa, Akiwa na umri wa miaka 29, Alikuwa ameishi maisha ya mtu wa kawaida, Akila wakati Alipotakiwa kula, Akilala na kuvaa kwa kawaida, na hakuna kitu chochote kumhusu kilichokuwa tofauti na wengine. Bila shaka, hii ilikuwa tu kwa macho ya nyama ya mwanadamu. Wakati mwingine Alikuwa mnyonge sana, na wakati mwingine Hakuweza kupambanua mambo, kama tu ilivyoandikwa katika Biblia: Akili zake zilikua pamoja na umri Wake. Maneno haya yanaonyesha tu kwamba Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, na kwamba Hakuwa tofauti hasa na watu wengine ambao ni wa kawaida. Alikuwa pia amelelewa kama mtu wa kawaida, na hakuwa na chochote maalum kumhusu. Hata hivyo Alikuwa chini ya utunzaji na ulinzi wa Mungu. Baada ya kubatizwa, Alianza kujaribiwa, kisha Akaanza kufanya huduma Yake na kufanya kazi, na Alimiliki nguvu, hekima, na mamlaka. Hii haimaanishi kwamba Roho Mtakatifu hakufanya kazi ndani Yake kabla ya ubatizo Wake, ama Hakuwa ndani Yake. Kabla ya ubatizo Wake Roho Mtakatifu pia aliishi ndani Yake lakini Hakuwa ameanza rasmi kazi Yake, kwani kuna mipaka ya wakati ambapo Mungu anafanya kazi Yake, na zaidi ya hayo, watu wa kawaida wana mchakato wa kawaida wa kukua. Roho Mtakatifu daima alikuwa Akiishi ndani Yake, Yesu alipozaliwa, Alikuwa tofauti na wengine, na nyota ya asubuhi ilionekana; kabla ya kuzaliwa Kwake, malaika alimtokea Yusufu katika ndoto na kumwambia kwamba Mariamu atajifungua mtoto wa kiume, na kwamba mtoto huyo alipatwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Baada ya Yesu kubatizwa, Roho Mtakatifu Alianza kazi Yake, lakini hili halimaanishi kwamba Roho Mtakatifu alikuwa tu amemshukia Yesu wakati huo. Huo msemo kwamba Roho Mtakatifu alishuka kama njiwa juu yake inamaanisha kuanza rasmi kwa huduma Yake. Roho wa Mungu alikuwa ndani yake hapo awali, lakini Hakuwa ameanza kufanya kazi, kwani wakati haukuwa umefika, na Roho hakuanza kazi upesi. Roho alimshuhudia kupitia ubatizo. Alipoinuka kutoka kwenye maji, Roho alianza rasmi kufanya kazi ndani Yake, ambayo iliashiria kwamba mwili wa Mungu mwenye mwili ulikuwa umeanza kutimiza huduma Yake, na alikuwa ameanza kazi ya ukombozi, hiyo ni, Enzi ya Neema ilikuwa imeanza rasmi. Na kwa hivyo, kuna wakati wa kazi Ya Mungu, bila kujali kazi Anayoifanya. Baada ya ubatizo Wake, hakukuwa na mabadiliko fulani kwa Yesu; Alikuwa bado ndani ya mwili Wake wa kawaida. Ni kwamba tu Alianza kazi Yake na kufichua utambulisho Wake, na Alijawa na mamlaka na nguvu. Kwa swala hili, Alikuwa tofauti na hapo awali. Utambulisho Wake ulikuwa tofauti, ambayo ni kusema kwamba kulikuwa na mabadiliko makubwa katika hadhi Yake; huu ulikuwa ushahidi wa Roho Mtakatifu, na haikuwa kazi iliyofanywa na mwanadamu. Mwanzoni, watu hawakujua, na walikuja kujua kidogo wakati Roho Mtakatifu alipomshuhudia Yesu kwa njia hiyo. Kama Yesu angekuwa amefanya kazi kubwa kabla ya Roho Mtakatifu kumshuhudia, lakini bila ushuhuda wa Mungu Mwenyewe, basi bila kujali jinsi kazi Yake ilivyokuwa kubwa, watu hawangejua kuhusu utambulisho Wake, kwani jicho la mwanadamu halingekuwa na uwezo wa kuiona. Bila hatua ya ushuhuda wa Roho Mtakatifu, hakuna ambaye angemtambua kama Mungu mwenye mwili. Kama, baada ya Roho Mtakatifu kumshuhudia, Yesu angeendelea kufanya kazi kwa njia ile ile, bila tofauti yoyote, basi haingekuwa na athari hiyo, na katika hili hasa inaonyeshwa kazi ya Roho Mtakatifu pia. Baada ya Roho Mtakatifu kutoa ushuhuda, Roho Mtakatifu alipaswa kujionyesha Mwenyewe, ili uweze kuona wazi kuwa Alikuwa Mungu, kwamba kulikuwa na Roho wa Mungu ndani Yake; ushuhuda wa Mungu haukukosea, na hii ingethibitisha kwamba ushuhuda Wake ulikuwa sahihi. Iwapo kazi ya kabla na baada ya ushuhuda wa Roho Mtakatifu ingekuwa sawa, basi huduma Yake katika mwili na kazi ya Roho Mtakatifu isingeweza kutambulika, na hivyo mwanadamu hangekuwa na uwezo wa kutambua kazi ya Roho Mtakatifu, kwani hakuwa na tofauti ya wazi. Baada ya kuwa na ushuhuda, Roho Mtakatifu alilazimika kutetea huu ushuhuda, na hivyo ilimlazimu kuonyesha hekima na mamlaka Yake ndani ya Yesu, ambayo ilikuwa tofauti na wakati wa mwanzo. Bila shaka, hii haikuwa matokeo ya ubatizo—ubatizo ni utaratibu tu, ni kwamba tu ubatizo ulikuwa njia ya kuonyesha kwamba ulikuwa wakati wa kufanya huduma Yake. Kazi hiyo ilikuwa ya kuweka wazi nguvu kubwa za Mungu, kuweka wazi ushuhuda wa Roho Mtakatifu, na Roho Mtakatifu angechukua jukumu la ushuhuda huu mpaka mwisho. Kabla ya kufanya huduma Yake, Yesu pia alisikiliza mahubiri, Alihubiri na kueneza injili katika maeneo mbalimbali. Hakufanya kazi yoyote kubwa kwa sababu muda ulikuwa bado haujafika ili Afanye huduma Yake, na pia kwa sababu Mungu Mwenyewe alijificha kwa unyenyekevu ndani ya mwili, na Hakufanya kazi yoyote hadi wakati ulipofika. Hakufanya kazi kabla ya ubatizo kwa sababu mbili: Kwanza, kwa sababu Roho Mtakatifu hakuwa ameshuka rasmi juu Yake kufanya kazi (ambavyo ni kusema, Roho Mtakatifu hakuwa amempa Yesu nguvu na mamlaka ya kufanya kazi kama hii), na hata kama Angekuwa anajua utambulisho Wake Mwenyewe, Yesu hangeweza kufanya kazi Aliyonuia kufanya baadaye, na ingembidi kusubiri hadi siku Yake ya ubatizo. Huu ulikuwa wakati wa Mungu, na hakuna ambaye angeweza kuikiuka, hata Yesu Mwenyewe; Yesu Mwenyewe hangeweza kuipinga kazi Yake Mwenyewe. Bila shaka, huu ulikuwa unyenyekevu wa Mungu, na pia sheria ya kazi ya Mungu; Kama Roho wa Mungu hangefanya kazi, hakuna ambaye angeweza kufanya kazi Yake. Pili, kabla ya Yeye kubatizwa, Alikuwa tu mwanadamu wa kawaida sana, bila tofauti na watu wa kawaida; hiki ni kipengele kimoja cha jinsi Mungu mwenye mwili Alivyokuwa wa kawaida. Mungu mwenye mwili hakukiuka mipango ya Roho wa Mungu; Alifanya kazi kwa utaratibu na kwa kawaida sana. Ilikuwa tu baada ya ubatizo ndipo kazi Yake ilikuwa na mamlaka na nguvu. Ambavyo ni kusema, hata kama alikuwa Mungu mwenye mwili, Hakufanya matendo yasiyo ya kawaida, na Alikua kwa njia sawa na watu wa kawaida. Kama Yesu angekuwa Ameshafahamu utambulisho Wake mwenyewe, kama Angekuwa amefanya kazi kubwa katika nchi yote kabla ya ubatizo Wake, na kama Angekuwa tofauti na watu wa kawaida, Akijionyesha mwenyewe kuwa wa ajabu, basi haingewezekana tu kwa Yohana kufanya kazi yake, lakini pia hakungekuwa na njia ya Mungu kuanza hatua ifuatayo ya kazi Yake. Kwa hivyo hii ingethibitisha kwamba kile ambacho Mungu alifanya kilikuwa kimeenda kinyume, na kwa mwanadamu, ingeonekana kwamba Roho wa Mungu na mwili wa Mungu mwenye mwili hawakutoka kwenye chanzo kimoja. Hivyo, kazi ya Yesu iliyorekodiwa katika Biblia ni kazi iliyofanywa baada ya Yeye kubatizwa, kazi iliyofanywa katika kipindi cha miaka mitatu. Biblia haijarekodi Alichofanya kabla ya kubatizwa kwa sababu Hakufanya kazi hii kabla ya kubatizwa. Alikuwa tu mtu wa kawaida, na Alimwakilisha mtu wa kawaida; kabla ya Yesu kuanza kufanya huduma Yake, Hakuwa tofauti na watu wa kawaida, na wengine hawakuweza kuona tofauti Kwake. Ni baada tu ya Yeye kufikisha umri wa miaka 29 ndipo Yesu alijua kwamba Alikuwa amekuja kukamilisha hatua ya kazi ya Mungu; kabla; Yeye Mwenyewe hakujua, kwani kazi Aliyoifanya Mungu ilikuwa ya kawaida. Alipohudhuria mkutano katika sinagogi Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili, Mariamu alikuwa akimtafuta, na Alisema tu sentensi moja kwa namna sawa kama mtoto mwingine yeyote: “Mama! Hujui kwamba ni lazima Niyaweke mapenzi ya Baba Yangu juu ya mengine yote?” Bila shaka, kwa vile Alitungwa mimba kwa Roho Mtakatifu, je, Yesu hangekuwa maalum kwa njia fulani? Lakini umaalumu Wake haukumaanisha kwamba Hakuwa wa kawaida, bali ni kwamba tu Alimpenda Mungu zaidi ya mtoto mwingine mdogo. Ingawa Alionekana kama mwanadamu, kiini Chake bado kilikuwa maalum na tofauti na cha wengine. Lakini, ilikuwa tu baada ya ubatizo ndipo Alipohisi Roho Mtakatifu akifanya kazi ndani Yake, ndipo Alipohisi kuwa alikuwa ni Mungu Mwenyewe. Ni baada tu ya Yeye kufikisha miaka 33 ndipo Alipotambua kweli kuwa Roho Mtakatifu alinuia kufanya kazi ya kusulubishwa kupitia Yeye. Akiwa na umri wa miaka 32, Alikuja kujua baadhi ya ukweli wa ndani, kama tu ilivyoandikwa katika Injili ya Mathayo: “Naye Simoni Petro akajibu na kusema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aishiye. … Kutoka wakati huo kuendelea Yesu alianza kuwaonyesha wanafunzi Wake, jinsi ilivyompasa kwenda Yerusalemu, na kupitia mateso mengi ya wazee na makuhani wakuu na waandishi, na kufishwa, na afufuke tena siku ya tatu.” Hakujua awali kazi Aliyotakiwa kufanya, lakini kwa wakati maalum. Hakujua kwa kina punde tu Alipozaliwa; Roho Mtakatifu alifanya kazi polepole ndani Yake, na kulikuwa na mchakato wa kazi. Kama, hapo mwanzo, Alijua kwamba Alikuwa Mungu, na Kristo, na Mwana wa Adamu mwenye mwili, kwamba Alikuwa akamilishe kazi ya kusulubiwa, basi ni kwa nini Hakufanya kazi hapo awali? Kwa nini ilikuwa tu baada ya kuwaambia wanafunzi Wake kuhusu huduma Yake ndipo Yesu alipohisi huzuni, na kuomba kwa bidii kwa ajili ya hili? Kwa nini Yohana alimfungulia njia na kumbatiza kabla ya Yeye kuelewa mambo mengi ambayo Hakuwa ameyaelewa? Kile ambacho hii inathibitisha ni kwamba ilikuwa ni kazi ya Mungu mwenye mwili, na hivyo ili Aielewe, na kuitimiza, kulikuwa na mchakato, kwa kuwa Alikuwa mwili wa Mungu mwenye mwili, na kazi Yake ilikuwa tofauti na ile iliyofanywa moja kwa moja na Roho.

Kila hatua ya kazi ya Mungu inafuata mkondo huo huo, na hivyo katika mpango wa usimamizi wa Mungu wa miaka elfu sita, kila hatua imefuatwa kwa karibu na inayofuata, kuanzia kwenye msingi wa ulimwengu hadi leo. Kama kusingekuwa na mtu wa kutengeneza njia, basi kusingekuwa na mtu wa kuja baadaye; kwa kuwa wapo wanaokuja baadaye, basi kuna wale wanaotengeneza njia. Kwa njia hii kazi imepitishwa chini, hatua kwa hatua. Hatua moja inafuata nyingine, na bila mtu wa kufungua njia, haitawezekana kuanza kazi, na Mungu angekosa namna ya kupeleka kazi Yake mbele. Hakuna hatua inayopingana na nyingine, na kila hatua inafuata nyingine katika mfuatano ili kuunda mkondo; hii yote inafanywa na Roho Yule Yule. Lakini bila kujali iwapo mtu atafungua njia ama kuendeleza kazi ya mwingine, hii haiamui utambulisho wao. Je, hii si sawa? Yohana aliifungua njia, na Yesu akaendeleza kazi yake, hivyo hii inathibitisha kwamba utambulisho wa Yesu ni wa chini kuliko ule wa Yohana? Yehova alitekeleza kazi Yake kabla ya Yesu, kwa hivyo unaweza kusema kwamba Yehova ni mkuu kuliko Yesu? Ikiwa walitengeneza njia ama kuendeleza kazi za wengine sio muhimu; kilicho muhimu ni kiini cha kazi zao, na utambulisho unaowakilishwa. Hii si sawa? Kwa vile Yesu alinuia kufanya kazi miongoni mwa wanadamu, ilimbidi Awainue wale ambao wangefanya kazi ya kutengeneza njia. Yohana alipoanza tu kuhubiri, alisema, “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito Yake.” “Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.” Alizungumza hivi tangu mwanzo kabisa, na kwa nini aliweza kuyasema maneno haya? Kwa suala la utaratibu ambao maneno haya yalisemwa, ni Yohana aliyezungumzia kwanza injili ya ufalme wa mbinguni, na Yesu aliyezungumza baadaye. Kulingana na dhana za mwanadamu, ni Yohana aliyeifungua njia mpya, na bila shaka Yohana alikuwa mkuu kuliko Yesu. Lakini Yohana hakusema yeye ni Kristo, na Mungu hakumshuhudia kama Mwana mpendwa wa Mungu, lakini Alimtumia tu kufungua na kuandaa njia ya Bwana. Alimtengenezea Yesu njia, lakini hangefanya kazi kwa niaba ya Yesu. Kazi zote za mwanadamu pia zilidumishwa na Roho Mtakatifu.

Katika enzi ya Agano la Kale, ni Yehova aliyeongoza njia, na kazi ya Yehova iliwakilisha enzi nzima ya Agano la Kale, na kazi zote zilizofanywa Israeli. Musa tu alizingatia tu hizi kazi duniani, na kazi zake zinachukuliwa kuwa ushirikiano uliotolewa na mwanadamu. Wakati huo, Yehova ndiye aliyezungumza, na Alimwita Musa, na Alimwinua Musa miongoni mwa watu wa Israeli, na kumfanya awaongoze nyikani na kuendelea hadi Kanaani. Hii haikuwa kazi ya Musa mwenyewe, bali ile ambayo ilielekezwa kibinafsi na Yehova, na hivyo Musa hawezi kuitwa Mungu. Musa pia aliweka sheria, lakini sheria hiyo iliamrishwa kibinafsi na Yehova. Ilikuwa tu kwamba Yeye alimfanya Musa aitamke. Yesu pia alitoa amri, na Aliifuta sheria ya Agano la Kale na kuweka amri za enzi mpya. Kwa nini Yesu ni Mungu Mwenyewe? Kwa sababu haya si mambo sawa. Wakati huo, kazi aliyoifanya Musa haikuwakilisha enzi, wala haikufungua njia mpya; alielekezwa mbele na Yehova, na alikuwa tu anatumiwa na Mungu. Yesu alipokuja, Yohana alikuwa ametekeleza hatua ya kazi ya kutengeneza njia, na alikuwa ameanza kueneza injili ya ufalme wa mbinguni (Roho Mtakatifu alikuwa Ameanzisha hii). Yesu alipokuja, Alifanya moja kwa moja kazi Yake Mwenyewe, lakini kulikuwa na tofauti kubwa kati ya kazi Yake na kazi ya Musa. Isaya pia alizungumza unabii mwingi, lakini mbona yeye hakuwa Mungu Mwenyewe? Yesu Hakuzungumza unabii mwingi lakini mbona Alikuwa Mungu Mwenyewe? Hakuna aliyethubutu kusema kwamba kazi zote za Yesu wakati huo zilitoka kwa Roho Mtakatifu, wala hawakuthubutu kusema kuwa zote zilitokana na matakwa ya mwanadamu, ama kwamba zilikuwa kabisa kazi za Mungu Mwenyewe. Mwanadamu hakuwa na njia yoyote ya kuchambua mambo haya. Inaweza kusemwa kwamba Isaya alifanya kazi kama hiyo, na kuzungumza unabii huo, na yote yalitoka kwa Roho Mtakatifu; hayakutoka moja kwa moja kwa Isaya mwenyewe, lakini yalikuwa ufunuo kutoka kwa Yehova. Yesu hakufanya kazi nyingi sana, na Hakusema maneno mengi sana, wala Hakuzungumza unabii mwingi. Kwa mwanadamu, mahubiri Yake hayakuonekana hasa yaliyoinuliwa juu, lakini alikuwa Mungu Mwenyewe, na mwanadamu hawezi kueleza haya. Hakuna aliyewahi kumwamini Yohana, ama Isaya, ama Daudi, wala hakuna aliyewahi kuwaita Mungu, ama Daudi Mungu ama Yohana Mungu, hakuna aliyewahi kuzungumza hivi, na ni Yesu tu aliyewahi kuitwa Kristo. Uainishaji huu umefanywa kulingana na ushuhuda wa Mungu, kazi Aliyoifanya, na huduma Aliyoifanya. Kuhusu watu wakuu wa Biblia—Ibrahimu, Daudi, Yoshua, Danieli, Isaya, Yohana na Yesu—kupitia kazi walizofanya, unaweza kusema ni nani aliye Mungu Mwenyewe, na ni watu wapi walio manabii, na ni wapi walio mitume. Ni nani aliyetumiwa na Mungu, na nani aliyekuwa Mungu Mwenyewe, inatofautishwa na kuamuliwa na asili na aina za kazi walizozifanya. Iwapo huwezi kutofautisha, basi hii inadhihirisha kwamba hujui maana ya kumwamini Mungu. Yesu ni Mungu kwa sababu Alizungumza maneno mengi, na kufanya kazi nyingi sana, maonyesho Yake ya miujiza nyingi. Vivyo hivyo, Yohana, pia alifanya kazi nyingi, na kuzungumza maneno mengi, Musa pia; mbona hawakuitwa Mungu? Adamu aliumbwa moja kwa moja na Mungu; mbona hakuitwa Mungu, badala tu ya kuitwa kiumbe? Mtu akikwambia, “Leo, Mungu amefanya kazi nyingi sana, na kuzungumza maneno mengi; Yeye ni Mungu Mwenyewe. Basi, vile Musa alivyozungumza maneno mengi, lazima yeye pia ni Mungu Mwenyewe!” inapaswa uwarudishie swali, “Wakati huo, kwa nini Mungu alimshuhudia Yesu, na sio Yohana, kama Mungu Mwenyewe? Je, Yohana hakumtangulia Yesu? Ni ipi iliyokuwa kubwa, kazi ya Yohana ama ya Yesu? Kwa mwanadamu, kazi ya Yohana inaonekana kuwa kuu kuliko ya Yesu, lakini kwa nini Roho Mtakatifu alimshuhudia Yesu, na sio Yohana?” Jambo hilo hilo linafanyika leo! Wakati huo, Musa alipokuwa akiwaongoza watu wa Israeli, Yehova alisema naye kutoka katikati ya mawingu. Musa hakuzungumza moja kwa moja lakini badala yake aliongozwa moja kwa moja na Yehova. Hii ilikuwa kazi ya Israeli ya Agano la Kale. Ndani ya Musa hakukuwa na Roho, wala nafsi ya Mungu. Asingeweza kufanya kazi hiyo, na hivyo kuna tofauti kubwa kati ya kazi aliyoifanya na kazi iliyofanywa na Yesu. Na hiyo ni kwa sababu kazi walizozifanya zilikuwa tofauti! Iwapo mtu anatumiwa na Mungu, ama ni nabii, mtume, ama Mungu Mwenyewe, inaweza kubainishwa na asili ya kazi yake, na hii itakomesha mashaka yenu. Katika Biblia imeandikwa kwamba Mwana-Kondoo pekee ndiye anayeweza kufungua mihuri saba. Katika zama zote kumekuwa na wachambuzi wengi wa maandiko miongoni mwa watu wakuu, na hivyo unaweza kusema kwamba wote ni Mwana Kondoo? Unaweza kusema kwamba maelezo yao yote yalitoka kwa Mungu? Walikuwa tu wachambuzi; hawana utambulisho wa Mwana Kondoo. Wanastahilije kuivunja mihuri saba? Ni ukweli kwamba “Mwana Kondoo pekee ndiye Anayeweza kuifungua ile mihuri saba,” lakini Yeye haji tu ili kuivunja ile mihuri saba; hakuna umuhimu wa kazi hii, inayofanywa kwa bahati. Yuko wazi kabisa kuhusu kazi Yake Mwenyewe; je, ni muhimu Kwake kutumia muda mwingi kufasiri maandiko? Je, ni lazima “Enzi ya Mwana Kondoo Anayefasiri Maandiko” iongezwe kwenye ile miaka elfu sita ya kazi? Anakuja kufanya kazi mpya, lakini pia Anatoa baadhi ya ufunuo kuhusu kazi za nyakati zilizopita, Akiwafanya watu waelewe ukweli wa miaka elfu sita ya kazi. Hakuna haja ya kueleza vifungu vingi kutoka kwenye Biblia; ni kazi ya leo ndiyo iliyo kuu, ambayo ni muhimu. Unapaswa kujua kwamba Mungu haji hasa ili kuivunja mihuri saba, bali kufanya kazi ya wokovu.

Unajua tu kwamba Yesu atashuka wakati wa siku za mwisho, lakini je, Atashuka kwa njia gani hasa? Mwenye dhambi kama wewe, ambaye umetoka tu kukombolewa, na haujabadilishwa bado, ama kukamilishwa na Mungu, je, unaweza kufuata nia za Mungu? Kwa wewe, wewe ambaye ni wa nafsi yako ya zamani, ni kweli kuwa uliokolewa na Yesu, na kwamba huhesabiwi kama mwenye dhambi kwa sababu ya wokovu wa Mungu, lakini hii haithibitishi kwamba wewe si mwenye dhambi, na si mchafu. Unawezaje kuwa mtakatifu kama haujabadilishwa? Ndani, umezingirwa na uchafu, ubinafsi na ukatili, na bado unatamani kushuka na Yesu—huwezi kuwa na bahati namna hiyo! Umepitwa na hatua moja katika imani yako kwa Mungu: umekombolewa tu, lakini haujabadilishwa. Ili uweze kuwa sawa na nia za Mungu, lazima Mungu Mwenyewe afanye kazi ya kukubadilisha na kukutakasa; ikiwa umekombolewa tu, hautakuwa na uwezo wa kufikia utakatifu. Kwa njia hii hautahitimu kushiriki katika baraka nzuri za Mungu, kwani umepitwa na hatua kwa kazi ya Mungu ya kumsimamia mwanadamu, ambayo ni hatua muhimu ya kubadilisha na kukamilisha. Na basi wewe, mwenye dhambi uliyetoka tu kukombolewa, huna uwezo wa kurithi urithi wa Mungu moja kwa moja.

Bila kuanza kwa hatua hii mpya ya kazi, ni nani anayejua ninyi wainjilisti, wahubiri, wachambuzi na wale wanaoitwa watu wakuu wa kiroho mngefikia wapi! Bila kuanza kwa hatua hii mpya ya kazi, kile ambacho mngezungumza kukihusu kingekuwa cha zamani! Ingekuwa kuhusu kupaa kwenye kiti cha enzi, au kuandaa kimo cha kuwa mfalme; ama kujinyima au kuutiisha mwili wa mtu; ama kuwa na subira au kujifunza masomo kutoka kwenye mambo yote; ama unyenyekevu au upendo. Je, huku si kuimba wimbo ule ule wa zamani? Ni suala tu la kuita kitu kilekile kwa jina tofauti! Iwe ni kufunika kichwa na kumega mkate, au kuweka mikono na kuomba, na kuponya wagonjwa na kutoa mapepo. Je, kunaweza kuwa na kazi yoyote mpya? Je, kunaweza kuwa na matarajio yoyote ya maendeleo? Ukiendelea kwa njia hii, utayafuata mafundisho kwa upofu, ama ufuate utaratibu. Mnaamini kazi yenu kuwa ya juu mno, lakini hamjui kwamba yote yalipitishwa na kufundishwa na hao “watu wazee” wa nyakati za zamani? Je, hayo yote mnayoyasema na kuyafanya si maneno ya mwisho ya wazee hao? Je, hayo siyo maagizo yaliyotolewa na wazee hao kabla ya kuaga dunia? Je, unafikiri kuwa matendo yako yanapita yale ya Mitume na Manabii wa vizazi vilivyopita, na hata kupita kila kitu? Kuanza kwa hatua hii ya kazi kumeleta mwisho wa kuabudu kwenu kazi ya Witness Lee ya kutafuta kuwa mfalme, na kupaa kwenye kiti cha enzi, na kumekamata kiburi na kujigamba kwenu, ili kwamba msiweze kuingilia hatua hii ya kazi. Bila hatua hii ya kazi, mngezama hata zaidi hadi msiweze kukombolewa. Kuna mengi sana ambayo ni ya zamani miongoni mwenu! Kwa bahati nzuri, kazi ya leo imewarudisha; vinginevyo, ni nani anayejua ni mwelekeo gani ambao mgechukua! Kwa kuwa Mungu ni Mungu ambaye daima ni mpya na kamwe si mzee, kwa nini hutafuti mambo mapya? Kwa nini unashikilia mambo ya zamani kila wakati? Kwa hivyo, kuijua kazi ya Roho Mtakatifu leo kuna umuhimu mkubwa!

Iliyotangulia:  Unapaswa Kujua Namna Ambavyo Binadamu Wote Wameendelea Hadi Siku ya Leo

Inayofuata:  Wale Waliokamilishwa Pekee Ndio Wanaoweza Kuishi Maisha Yenye Maana

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger