Wale Waliokamilishwa Pekee Ndio Wanaoweza Kuishi Maisha Yenye Maana

Kwa kweli, kazi inayofanywa sasa ni kuwafanya watu kumtoroka Shetani, kutoroka babu zao wa kale. Hukumu zote kwa neno zinalenga kufichua tabia potovu ya binadamu na kuwawezesha watu kuelewa kiini cha maisha. Hukumu hizi zinazorudiwa mara kwa mara zote huchoma mioyo ya watu. Kila hukumu inaathiri moja kwa moja hatima yao na inakusudiwa kuumiza mioyo yao ili waweze kuachana na mambo hayo yote na hivyo basi kuja kujua maisha, kuujua ulimwengu huu mchafu, na pia kujua hekima ya Mungu na uweza Wake na kujua mwanadamu huyu aliyepotoshwa na Shetani. Kadiri aina hii ya kuadibu na hukumu inavyozidi, ndivyo moyo wa mwanadamu unavyoweza kujeruhiwa na ndivyo roho yake inavyoweza kuamshwa. Kuziamsha roho za watu hawa waliopotoshwa sana na waliodanganyika sana ndilo lengo la aina hii ya hukumu. Mwanadamu hana roho, yaani, roho yake ilikufa zamani na hajui kwamba kuna Mbingu, hajui kwamba kuna Mungu, na kwa hakika hajui kwamba anahangaika katika shimo la kifo; anaweza kujuaje kwamba anaishi katika kuzimu hii yenye maovu hapa ulimwenguni? Angewezaje kujua kwamba maiti hii yake ambayo imeoza, kwa kupotoshwa na shetani, imeanguka Kuzimuni kwenye kifo? Angewezaje kujua kwamba kila kitu hapa ulimwenguni kimeharibiwa kitambo kiasi cha kutokarabatika na mwanadamu? Na angewezaje kujua kwamba Muumba amekuja duniani leo na anatafuta kikundi cha watu wapotovu ambao Anaweza kuwaokoa? Hata baada ya mwanadamu kupitia kila usafishaji na hukumu inayowezekana, ufahamu wake wa chini unashtuka kwa shida na kwa kweli hauitikii chochote. Binadamu wamezoroteka kweli! Ingawa aina hii ya hukumu ni kama mvua katili ya mawe inyeshayo kutoka mbinguni, ni yenye manufaa makubwa zaidi kwa binadamu. Lau si kwa kuwahukumu watu namna hii, kusingekuwa na matokeo na isingewezekana kabisa kuwaokoa watu kutoka kwenye dimbwi la taabu. Kama isingekuwa kwa kazi hii, ingekuwa vigumu sana kwa watu kutoka Kuzimuni kwa sababu mioyo yao imekufa kitambo na roho zao kukanyagiwa kitambo na Shetani. Kuwaokoa nyinyi ambao mmeanguka kwenye kina kirefu cha uozo kunahitaji kuwaita kwa bidii sana, kuwahukumu kwa bidii sana, na kwa kufanya hivi tu ndipo mioyo hiyo yenu migumu itakapozinduka.

Miili yenu, matamanio yenu ya kupita kiasi, ulafi wenu, na ashiki yenu vyote vimekita mizizi ndani yenu. Mambo haya yanaidhibiti sana mioyo yenu kiasi kwamba hamna nguvu za kutupa huo utumwa wa mawazo hayo ya kikabaila na yaliyooza. Hamtamani kubadilisha hali yenu ya sasa, wala kuukimbia ushawishi wa giza. Mmefanywa kuwa watumwa tu wa mambo hayo. Hata kama mnajua kwamba maisha kama hayo ni yenye maumivu sana na kwamba ulimwengu kama huo ni wenye giza la kupindukia, bado, hakuna hata mmoja wenu anao ujasiri wa kubadilisha maisha ya aina hii. Mnatamani tu kutoroka aina hii ya maisha halisi, kuondoa nafsi zenu kutoka kwenye mahali pa mateso ya muda na kuishi katika mazingira yenye amani, furaha na yafananayo na mbinguni. Hamko radhi kuvumilia magumu ili kuweza kubadilisha maisha yenu ya sasa; vilevile hamko radhi kutafuta ndani ya hukumu hii na kuadibu huku maisha ambayo mnafaa kuyaishi. Badala yake, mnaziota ndoto zisizo na uhalisi kabisa kuhusu ulimwengu mzuri wa nje ya miili yenu. Maisha mnayotamani ni yale mnayoweza kupata kwa urahisi bila kupitia maumivu yoyote. Hayo si ya kihalisi kamwe! Kwa sababu kile mnachotumainia si kuishi kwa kudhihirisha maisha ya maana katika mwili na kupata ukweli kwenye harakati ya maisha yenu, yaani, kuishi kwa ajili ya ukweli na kutetea haki. Haya siyo yale maisha ambayo mngedhani ni ya kupendeza, ya kusisimua. Mnahisi kwamba haya hayatakuwa maisha yanayovutia au ya maana. Kwa macho yenu, kuishi maisha kama hayo kutatoa hisia za kudhalilishwa! Hata Ingawa mnakubali kuadibu huku leo, hata hivyo kile mnachofuatilia si kupata ule ukweli au kuishi kwa njia ya ukweli katika wakati wa sasa, bali kuweza kuingia katika maisha yenye furaha nje ya miili yenu baadaye. Hamtafuti ukweli na wala hamtetei ukweli na kwa hakika hamko kwa ajili ya ukweli na kwa hakika hamko kwa ajili ya ukweli. Hamtafuti kuingia leo, lakini badala yake kila wakati mnafikiria “siku moja,” huku mkitazama mbingu ya samawati na kudondokwa na machozi machungu, na mkitarajia kuchukuliwa kuenda mbinguni siku moja. Je, hamjui kuwa mawazo yenu kama hayo tayari hayana uhusiano na uhalisi? Unaendelea kufikiria kwamba Mwokozi mwenye upole na huruma isiyoisha bila shaka atakuja siku moja kukuchukua pamoja na Yeye, wewe ambaye umevumilia ugumu na mateso ulimwenguni humu, na kwamba Yeye bila shaka atalipiza kisasi kwa ajili yako wewe ambaye umedhalilishwa na kunyanyaswa. Je, hujajaa dhambi? Je, wewe pekee ndiye uliyeteseka katika ulimwengu huu? Umemilikiwa na Shetani wewe mwenyewe na kuteseka—je, bado Mungu anahitaji kukulipizia kisasi? Wale wasioweza kutosheleza mahitaji ya Mungu—kwani wao wote si adui wa Mungu? Wale wasioamini katika Mungu mwenye mwili—kwani wao si wapinga Kristo? Matendo yako mazuri yana maana gani? Yanaweza kuchukua nafasi ya moyo unaomwabudu Mungu? Huwezi kupokea baraka za Mungu kwa kufanya baadhi ya matendo mazuri tu, naye Mungu hatakulipizia kisasi yale mabaya uliyofanyiwa kwa sababu tu umeonewa na kukandamizwa. Wale wanaomwamini Mungu ilhali hawamjui Mungu, lakini wanaofanya matendo mazuri—kwani wao nao hawaadibiwi pia? Unamwamini Mungu tu, unataka Mungu akushughulikie na Akulipizie kisasi tu kwa mabaya uliofanyiwa wewe, na unataka Mungu kukupa njia ya kimbilio kutoka kwa umaskini wako. Lakini unakataa kutilia maanani ukweli; wala hutamani kuishi kwa kudhihirisha ukweli. Hata zaidi, huwezi kuyakimbia maisha haya magumu na yasiyo na maana. Badala yake, huku ukiishi maisha yako katika mwili na maisha yako ya dhambi, unamwangalia Mungu kwa matarajio ya kusahihisha manung’uniko yako na kuondoa ukungu wa kuwepo kwako. Haya yanawezekanaje? Ukimiliki ukweli, unaweza kumfuata Mungu. Kama unaishi kwa kudhihirisha, unaweza kuwa onyesho la neno la Mungu. Kama unao uzima, unaweza kufurahia baraka ya Mungu. Ni wale tu walio na ukweli wanaweza kufurahia baraka ya Mungu. Mungu huhakikisha kwamba anawafidia wale wote wanaompenda kwa moyo wao wote pamoja na pia wanaovumilia magumu na mateso, na wala si kwa wale wanaojipenda tu na wamejipata kwenye mtego wa uwongo wa Shetani. Kunawezaje kuwa na wema miongoni mwa wale wasiopenda ukweli? Kunawezaje kuwa na haki miongoni mwa wale wanaopenda mwili tu? Si kweli kwamba haki na wema vyote vinarejelea ukweli? Si kweli kwamba vyote hivi vimehifadhiwa wale wanaompenda Mungu kwa moyo wao wote? Wale wasiopenda ukweli na ambao ni maiti zilizooza—je, watu wote hawa huwa hawafichi maovu? Wale wasioweza kuuishi ukweli—hawa wote si maadui wa ukweli? Na vipi kuhusu ninyi?

Kama unaweza kutoroka ushawishi huu wa giza na kujitenga na mambo hayo machafu, ikiwa unaweza kuwa mtakatifu, ina maana kwamba una ukweli. Si kwamba asili yako imebadilika, bali ni kwamba tu unaweza kuweka ukweli katika matendo na unaweza kuunyima mwili wako. Haya ndiyo yanayopatikana kwa wale waliotakaswa. Shabaha kuu ya kazi ya kushinda ni kuwatakasa binadamu ili mwanadamu aweze kuwa na ukweli, kwa sababu mwanadamu kwa sasa anaelewa ukweli kidogo sana! Kufanya kazi ya kushinda kwa watu hawa ni jambo lenye umuhimu mkubwa mno. Nyote mmeanguka katika ushawishi wa giza na mmeumizwa mno. Shabaha ya kazi hii, basi, ni kuwawezesha kujua asili ya binadamu na hivyo basi muishi kwa ukweli. Kukamilishwa ni kitu ambacho viumbe vyote vinapaswa kukubali. Kama kazi ya awamu hii inahusu tu kufanya watu kuwa wakamilifu, basi inaweza kufanywa Uingereza, au Amerika, au Israeli; inaweza kufanywa kwa watu wa taifa lolote. Lakini kazi ya kushinda inachagua. Hatua ya kwanza ya kazi ya kushinda ni ya muda mfupi; aidha, itatumika kumdhalilisha Shetani na kuushinda ulimwengu mzima. Hii ndiyo kazi ya kwanza ya kushinda. Mtu anaweza kusema kwamba kiumbe yeyote anayemwamini Mungu anaweza kufanywa kuwa kamili kwa sababu kukamilishwa ni kitu ambacho mtu anaweza kufikia tu baada ya mabadiliko ya muda mrefu. Lakini kushindwa ni tofauti. Kielelezo na mwakilishi wa kushinda lazima awe yule anayebaki nyuma zaidi, akiishi kwenye giza totoro kabisa, na vilevile mwenye hadhi ndogo kabisa, na asiyekuwa radhi kumkubali Mungu zaidi, na asiyemtii Mungu zaidi. Huyu ndiye aina ya mtu anayeweza kutoa ushuhuda wa kushindwa. Shabaha kuu ya kazi ya kushinda ni kumshinda Shetani. Shabaha kuu ya kufanya watu kuwa wakamilifu, kwa upande mwingine, ni kuwapata watu. Ni kwa ajili ya kuwawezesha watu kuwa na ushuhuda baada ya kushindwa ndio maana kazi ya kushinda imewekwa hapa, kwa watu kama ninyi. Lengo ni kuwafanya watu kutoa ushuhuda baada ya kushindwa. Watu hawa walioshindwa watatumika kufikia shabaha ya kumdhalilisha Shetani. Kwa hivyo, mbinu kuu ya kushinda ni ipi? Kuadibu, kuhukumu, kutoa laana, na kufichua—kutumia tabia ya haki katika kuwashinda watu ili waweze kushawishika kabisa kwa sababu ya tabia ya haki ya Mungu. Ili kutumia uhalisi wa neno na kutumia mamlaka ya neno ili kuwashinda watu na kuwashawishi kabisa—hii ndiyo maana ya kushindwa. Wale waliofanywa kuwa wakamilifu sio tu kwamba wanakuwa watiifu baada ya kushindwa, lakini wanaweza pia kuwa na maarifa ya kazi ya hukumu, kubadilisha tabia yao na kumjua Mungu. Wanapitia njia ya kumpenda Mungu na wamejawa na ukweli. Wanajua namna ya kupitia kazi ya Mungu, wanaweza kuteseka kwa ajili ya Mungu, na wana hiari zao wenyewe. Wale waliokamilishwa ni wale walio na ufahamu halisi wa ukweli kutokana na kupitia neno la Mungu. Wale walioshindwa ni wale wanaojua kuhusu ukweli lakini hawajakubali maana halisi ya ukweli. Baada ya kushindwa, wanatii, lakini utiifu wao wote unatokana na hukumu waliyopokea. Hawana uelewa kabisa wa maana halisi ya ukweli mwingi. Wanautambua ukweli kwa matamshi, lakini bado hawajapitia ukweli; wanauelewa ukweli, lakini hawajapitia ule ukweli. Kazi inayofanywa kwa wale wanaokamilishwa inajumuisha kuadibiwa na kuhukumiwa, pamoja na kupokea uzima. Mtu anayethamini kuingia katika ukweli ni mtu anayefaa kukamilishwa. Tofauti kati ya wale watakaofanywa kuwa wakamilifu na wale walioshindwa ni iwapo wanaingia katika ukweli. Wale wanaouelewa ukweli, walioingia katika ukweli, na wanauishi ukweli huo ndio wale waliokamilishwa; wale wasioelewa ukweli, hawauingii ukweli, yaani, wale wasioishi ukweli, ni watu wasioweza kukamilishwa. Ikiwa watu kama hao wanaweza sasa kutii kabisa, basi wameshindwa. Kama wale walioshindwa hawatafuti ukweli—kama wanafuata lakini hawauishi ukweli, ikiwa watauona na kuusikia ukweli lakini hawathamini kuuishi ukweli—basi hawawezi kukamilishwa. Watu ambao watafanywa kuwa wakamilifu wanatenda ukweli kulingana na mahitaji ya Mungu kwao katika njia ya kuelekea kukamilishwa. Kupitia haya, wanatimiza mapenzi ya Mungu, na wanapata kufanywa kuwa wakamilifu. Yeyote anayefuata hadi mwisho kabla ya kazi hiyo ya ushindi kuhitimishwa ni aliyeshindwa, lakini hawezi kusemwa kuwa ndiye aliyekamilishwa. Waliokamilishwa hurejelea wale ambao, baada ya kumalizika kwa kazi ya ushindi, wanaweza kufuatilia ukweli na kumilikiwa na Mungu. Inarejelea wale ambao, baada ya kukamilika kwa kazi ya ushindi, wanasimama imara katika majaribio na wanaishi kwa kudhihirisha ukweli. Kile kinachotofautisha kushindwa na kukamilishwa ni zile tofauti katika hatua za kufanya kazi na tofauti katika kiwango ambacho watu huelewa na kuingia katika ukweli. Wale wote ambao hawajaingia katika njia ya kukamilishwa, kumaanisha wale wasio na ukweli, mwishowe bado wataondolewa. Ni wale tu walio na ukweli na wanaouishi ukweli wanaoweza kumilikiwa kabisa na Mungu. Yaani, wale wanaoishi kwa kudhihirisha mfano wa Petro ndio wanaofanywa kuwa wakamilifu, wakati wengine wote ndio ambao wameshindwa. Kazi inayofanywa kwa wale wote wanaoshindwa inajumuisha tu kuweka laana, kuadibu, na kuonyesha hasira, na yale yanayowajia ni haki na laana tu. Kufanya kazi kwa mtu kama huyo ni kufichua waziwazi—kufichua tabia potovu iliyo ndani yake ili aweze kuitambua mwenyewe na kushawishika kabisa. Punde binadamu anapokuwa mtiifu kabisa, kazi ya ushindi inakamilika. Hata kama watu wengi wangali hawatafuti kuelewa ukweli, kazi ya ushindi itakuwa imekamilika.

Kuna vigezo vya kufikiwa ikiwa utakamilishwa. Kupitia kwa uamuzi wako, ustahimilivu wako, na dhamiri yako, na kupitia ufuatiliaji wako, utaweza kupitia maisha na kutimiza mapenzi ya Mungu. Haya ndiyo kuingia kwako na kile kinachohitajika kwenye njia ya kuwa mkamilifu. Kazi ya kukamilisha inaweza kufanywa kwa watu wote. Yeyote anayemfuatilia Mungu anaweza kufanywa kuwa mkamilifu na anayo fursa na sifa za kufanywa kuwa mkamilifu. Hakuna sheria ngumu na ya haraka hapa. Ikiwa mtu anaweza kukamilishwa hasa kunategemea kile anachofuatilia. Watu wanaopenda ukweli na walio na uwezo wa kuishi kwa kudhihirisha ukweli bila shaka wanaweza kufanywa kuwa wakamilifu. Watu wasioupenda ukweli hawasifiwi na Mungu; hawamiliki maisha ambayo Mungu anahitaji, na hawawezi kufanywa kuwa wakamilifu. Kazi ya kufanya kuwa kamili ni kwa ajili tu ya kuwapata watu, na wala si hatua katika kupigana na Shetani; kazi ya ushindi tu ndio kwa ajili ya kupigana na Shetani, kumaanisha kwamba ni kutumia kumshinda mwanadamu ili kumshinda Shetani. Sehemu hii ya baadaye ndiyo kazi kuu, ni, kazi mpya zaidi ambayo haijawahi kufanywa katika enzi zote. Mtu anaweza kusema kwamba malengo ya hatua hii ya kazi kimsingi ni kuwashinda watu wote ili kuweza kumshinda Shetani. Kazi ya kufanya watu kuwa wakamilifu—hiyo si kazi mpya. Kazi yote katika kipindi ambacho Mungu anafanya kazi katika mwili ina malengo yake makuu kama kuwashinda watu. Hii ni sawa na Enzi ya Neema. Kuwakomboa wanadamu wote kupitia kwa kusulubishwa ndiyo iliyokuwa kazi kuu. “Kuwapata watu” kulikuwa nyongeza katika kazi ya mwili na kulifanywa tu baada ya kusulubishwa. Wakati Yesu alipokuja na kufanya kazi Yake, shabaha Yake ilikuwa hasa kutumia kusulubishwa Kwake ili kushinda vifungo vya mauti na Kuzimu, kuweza kushinda ushawishi wa Shetani, kumaanisha kumshinda Shetani. Ilikuwa tu baada ya kusulubishwa kwa Yesu ndipo Petro alipoanza hatua kwa hatua kushika njia ya kuwa mkamilifu. Bila shaka alikuwa miongoni mwa wale waliomfuata Yesu wakati Yesu alipokuwa akifanya kazi, lakini hakufanywa kuwa mkamilifu wakati huo. Badala yake, ilikuwa ni baada ya Yesu kumaliza kazi Yake ndipo Petro alipoanza kuelewa taratibu ukweli na kisha akafanywa kuwa mkamilifu. Mungu mwenye mwili huja ulimwenguni tu kukamilisha hatua muhimu na ya maana sana ya kazi katika kipindi kifupi cha muda, si kuishi kwa kipindi kirefu miongoni mwa watu duniani kwa nia ya kuwakamilisha. Huwa hafanyi kazi hiyo. Hasubirii mpaka wakati ule ambao binadamu amefanywa kuwa mkamilifu kabisa ili kuhitimisha kazi Yake. Hayo siyo malengo na maana ya kupata mwili Kwake. Yeye huja tu ili kufanya kazi ya kipindi kifupi ya kuwaokoa binadamu, na wala si kufanya ile kazi ya kipindi kirefu sana ya kuwafanya binadamu kuwa wakamilifu. Kazi ya kuwaokoa binadamu ni ya uwakilishi, inayoweza kuzindua enzi mpya na inaweza kukamilishwa katika kipindi kifupi cha muda. Lakini kuwafanya binadamu kuwa wakamilifu kunahitaji kuwaleta binadamu hadi kiwango fulani na ni kazi inayoweza kuchukua muda mrefu. Kazi hii lazima ifanywe na Roho wa Mungu, lakini inafanywa kwa msingi wa ukweli unaozungumzwa wakati wa kazi Yake akiwa katika mwili. Ama kwa kuongezea, Yeye huwainua mitume kufanya kazi ya uchungaji ya kipindi kirefu, ili kufikia shabaha Yake ya kuwafanya binadamu kuwa wakamilifu. Mungu mwenye mwili hafanyi kazi hii. Anazungumza tu kuhusu njia ya maisha ili watu waweze kuelewa na kuwapatia tu binadamu ukweli, badala ya kuendelea kuandamana na mwanadamu katika kutenda ukweli kwani kufanya hivyo hakumo ndani ya huduma Yake. Kwa hivyo Hatakuwa akiandamana na mwanadamu mpaka siku ile ambayo mwanadamu ataelewa kabisa ukweli na kupata kabisa ukweli. Kazi Yake akiwa katika mwili inahitimishwa wakati mwanadamu anapoingia rasmi kwenye njia sahihi ya kumwamini Mungu, wakati mwanadamu anapoingia kwenye njia sahihi ya kufanywa kuwa mkamilifu. Hapa, bila shaka ndipo pia wakati ambapo atakuwa Ameshinda Shetani kabisa na kuutawala ulimwengu. Yeye hajali kama mwanadamu atakuwa hatimaye ameingia katika ukweli kwa wakati huo, wala Hajali kama maisha ya binadamu ni makubwa au madogo. Hakuna kati ya hayo ambayo Yeye akiwa katika mwili anafaa kusimamia; hakuna kati ya hayo yaliyo ndani ya huduma ya Mungu mwenye mwili. Punde Anapomaliza kazi aliyonuia, Yeye huhitimisha kazi Yake katika mwili. Kwa hiyo, kazi ambayo Mungu mwenye mwili anafanya ni kazi ile tu ambayo Roho wa Mungu hawezi kufanya moja kwa moja. Aidha, ni ile kazi ya wokovu ya kipindi kifupi, na wala si kazi ya kipindi kirefu hapa ulimwenguni.

Kukuza ubora wa tabia zenu hakumo ndani ya mawanda ya kazi Yangu. Ninawaambia mfanye hivi tu kwa sababu ubora wa tabia zenu upo chini sana. Kwa ukweli hii si sehemu ya kazi ya kukamilisha; badala yake, ni kazi ya ziada mnayofanyiwa ninyi. Kazi inayokamilishwa kwenu leo inafanywa kulingana na kile mnachohitaji. Imebinafsishwa, na wala si njia fulani inayofaa kuingiwa na kila mtu ambaye anafanywa kuwa mkamilifu. Kwa sababu ubora wenu wa tabia uko chini zaidi kuliko wa yeyote yule aliyefanywa kuwa mkamilifu kitambo, kazi hii, inapokuja kwenu, inakabiliwa na vizuizi vingi. Nipo miongoni mwenu Nikifanya kazi hii ya ziada kwa sababu walengwa wa kuwakamilisha ni tofauti. Kimsingi, wakati Mungu anapokuja duniani, Anabaki ndani ya eneo Lake linalofaa na kutekeleza kazi Yake, bila kujishughulisha sana na mambo mengine yasiyohusiana. Hajihusishi na masuala ya kifamilia au kushiriki katika maisha ya watu. Hajali kabisa kuhusu mambo hayo madogomadogo; yote haya si sehemu ya huduma Yake. Lakini ubora wako wa tabia uko chini zaidi kuliko vile Nilivyohitaji—hakuna ulinganifu kabisa—kiasi cha kwamba unakuwa kizuizi katika kazi. Aidha, kazi hii lazima ifanywe miongoni mwa watu katika nchi hii ya Uchina. Hamjapata elimu sana kiasi cha kwamba Sina chaguo lolote ila kuamuru kwamba muweze kupata elimu. Nimewaambieni kwamba hii ni kazi ya ziada, lakini pia ni kitu ambacho lazima muwe nacho, kitu ambacho kitawasaidia nyinyi katika kufanywa kuwa mkamilifu. Kwa hakika, mnafaa kupata elimu, maarifa ya msingi kuhusu mienendo yenu binafsi, na maarifa ya msingi kuhusu maisha yaliyo mbele yenu; Sipaswi kuwazungumzia kuhusu mambo haya. Lakini kwa sababu hamna mambo haya, Sina chaguo jingine ila kufanya kazi ya kutia vitu hivi ndani yenu baada ya kuzaliwa humu ulimwenguni. Hata kama mna dhana nyingi kunihusu, bado Ninahitaji hiki kutoka kwenu, bado Nahitaji kwamba muinue ubora wenu wa tabia. Si nia Yangu kuja na kufanya kazi hii, kwa sababu kazi Yangu ni kuwashinda tu, kupata imani yenu kamili kwa kuwahukumu nyinyi tu, hivyo basi kuonyesha njia ya maisha mnayofaa kuingia. Nikisema kwa njia nyingine, vile ambavyo mmeelimika na kama mna maarifa kuhusu maisha visingenihusu Mimi kamwe kama isingekuwa kwamba Nahitaji kuwashinda kwa neno Langu. Vyote hivi vinaongezewa ili kuhakikisha kuwa kuna matokeo yanayopatikana kutoka kwenye kazi ya ushindi na kwa minajili ya kufanywa kwenu kuwa wakamilifu kutakakofuata. Si hatua ya kazi ya ushindi. Kwa sababu ubora wenu wa tabia ni wa hali ya chini, na nyie ni wavivu, na wazembe, wajinga, na wapumbavu, na wagumu na washenzi—kwa sababu ninyi mmepitiliza kukosa ukawaida—Nahitaji kwanza muinue ubora wenu wa tabia. Yeyote anayetaka kufanywa mkamilifu lazima afikie vigezo fulani. Ili kufanywa kuwa mkamilifu, lazima mtu awe na akili timamu na yenye umakinifu, na awe tayari kuishi maisha yenye maana. Kama wewe ni mtu usiye tayari kuishi maisha matupu, ni mtu unayefuatilia ukweli, mtu uliye na bidii katika kila kitu unachofanya, na mtu aliye na ubinadamu wa kawaida kabisa, basi wewe una sifa zinazostahili kufanywa kuwa mkamilifu.

Kazi hii miongoni mwenu inatekelezwa kwenu kulingana na ile kazi inayohitajika kufanywa. Baada ya ushindi wa watu hawa, kundi la watu litafanywa kuwa kamilifu. Kwa hivyo, kazi nyingi za sasa pia zipo katika maandalizi kwa ajili ya lengo la kuwafanya kuwa wakamilifu, kwa sababu kuna watu wengi wenye shauku ya ukweli ambao wanaweza kukamilishwa. Kama kazi ya ushindi ilitakiwa ifanywe kwenu na baada ya hapo kusiwe na kazi zaidi iliyofanywa, basi je, haitakuwa kwamba baadhi ya wale wanaoutamani ukweli watakuwa hawajaupata? Kazi ya sasa inalenga kufungua njia ya kuwafanya watu kuwa wakamilifu baadaye. Ingawa kazi Yangu ni ya ushindi tu, njia ya maisha iliyotamkwa na Mimi hata hivyo inatayarisha kuwafanya watu kuwa wakamilifu baadaye. Kazi inayokuja baada ya ushindi inajikita katika kuwakamilisha watu, na hivyo ushindi unafanywa ili kuweka msingi wa kazi ya kukamilisha. Mwanadamu anaweza kufanywa kuwa mkamilifu baada ya kushindwa tu. Sasa hivi kazi kuu ni kushinda; baadaye wale wanaotafuta na kutamani ukweli watafanywa kuwa wakamilifu. Kufanywa kuwa mkamilifu kunahusisha vipengele chanya vya watu vya kuingia: Je, una moyo wa kumpenda Mungu? Je, kina cha uzoefu wako ni kipi unapotembea katika njia hii? Je, ni vipi ambavyo upendo wako kwa Mungu ni safi? Je, utendaji wako wa ukweli upo vipi hasa? Ili kufanywa kuwa mkamilifu, ni lazima mtu awe na maarifa ya msingi ya vipengele vyote vya ubinadamu. Hili ni hitaji la msingi. Wale wote wasioweza kufanywa kuwa wakamilifu baada ya kushindwa hugeuka na kuwa vyombo vya huduma na hatimaye bado watatupwa kwenye ziwa la moto na kibiriti na bado wataanguka ndani ya shimo lisilokuwa na mwisho kwa sababu ya tabia yao ambayo haijabadilika na wangali ni wa Shetani. Mtu akikosa sifa za kukamilishwa, basi hana maana—hana manufaa, ni chombo, kitu ambacho hakiwezi kustahimili majaribio ya moto! Je, una moyo wa kumpenda Mungu kwa kiwango gani sasa? Je, una moyo wa kujichukia kwa kiwango gani? Je, kweli ni kwa kiasi gani unamjua Shetani kwa undani? Je, mmeimarisha azimio lenu? Je, maisha yako ndani ya ubinadamu wako yamedhibitiwa vyema? Je, maisha yako yamebadilika? Je, unaishi maisha mapya? Je, mtazamo wenu wa maisha umebadilika? Kama mambo haya hayajabadilika, huwezi kufanywa kuwa mkamilifu hata kama hurudi nyuma; badala yake, wewe umeshindwa tu. Wakati ukifika wa kukujaribu, unakosa ukweli, ubinadamu wako si wa kawaida, na wewe ni wa kiwango cha chini kama mnyama. Umeshindwa tu, umekuwa tu mtu aliyeshindwa na Mimi. Kama vile punda, akishapata mjeledi wa bwana wake, yeye huwa na woga na hofu ya kufanya chochote kila wakati anapomwona bwana wake, ndivyo pia wewe ulivyo kama punda huyo aliyedhibitiwa. Kama mtu anakosa vipengele hivyo vizuri na badala yake yeye ni wa kutoonyesha hisia na mwenye woga, mwepesi kutishwa na wa kusitasita katika mambo yote, asiyeweza kutambua chochote kwa njia iliyo wazi, asiyeweza kukubali ukweli, ambaye bado hana njia ya kutenda, na hata zaidi asiye na moyo wa kumpenda Mungu—kama mtu hana uelewa wa namna ya kumpenda Mungu, namna ya kuishi maisha yenye maana, au namna ya kuwa mtu halisi—mtu kama huyu anawezaje kumshuhudia Mungu? Hii inaonyesha kwamba maisha yako yana thamani ndogo na wewe si chochote ila punda aliyedhibitiwa. Wewe umeshindwa, lakini hilo linamaanisha tu kwamba umelikataa lile joka kuu jekundu na umekataa kumilikiwa nalo; hiyo inamaanisha kwamba wewe unaamini kuwa kuna Mungu, unataka kutii mipango yote ya Mungu na huna malalamiko yoyote. Lakini je, katika vipengele chanya, je, unaweza kuliishi neno la Mungu na kumdhihirisha Mungu? Ikiwa huna lolote kati ya haya, inamaanisha kwamba hujamilikiwa na Mungu, na kwamba wewe ni punda aliyedhibitiwa tu. Hakuna chochote cha kutamanika ndani yako, na Roho Mtakatifu hayumo kazini ndani yako. Ubinadamu wako unakosa mengi na Mungu hawezi kukutumia. Lazima uidhinishwe na Mungu na kuwa bora zaidi mara mia moja kuliko wanyama wasioamini na kuliko wanaotembea wakiwa wafu—ni wale tu wanaofikia kiwango hiki ndio wanaostahili kufanywa kuwa wakamilifu. Ni iwapo tu mtu anao ubinadamu na dhamiri ndio anafaa kutumiwa na Mungu. Ni wakati tu ambapo mnakamilishwa ndio mnaweza kufikiriwa kuwa binadamu. Wale waliofanywa kuwa wakamilifu tu ndio wale wanaoishi maisha yenye maana. Watu kama hawa tu ndio wanaoweza kumshuhudia Mungu hata pakubwa.

Iliyotangulia:  Kuhusu Majina na Utambulisho

Inayofuata:  Mnapaswa Kuweka Pembeni Baraka za Hadhi na Kuelewa Mapenzi ya Mungu ya Kumletea Mwanadamu Wokovu

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Connect with us on Messenger